Tuesday, June 5, 2018

WALINZI WA HIFADHI WATAKIWA KUWA MAKINI NA WADILIFU KUTOKANA NA WANYAMA KUTOKA NJE YA HIFADHI


WALINZI wa wanyamapori katika maeneo yanayozunguka Pori ya Akiba la Maswa yanayopakana na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti wametakiwa kuwa makini na waadilifu kutokana na kuongezeka kwa wanyama adimu wanaofika maeneo yao.

Rai hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi ya Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori nchini (TAWA).Meja Jenerali mstaafu Hamisi Semfuko alipokua akikagua shughuli za uhifadhi na ulinzi katika maeneo hayo.

Meja Jenerali Semfuko, alisema kazi ya kupambana na ujangili inahitaji uvumilivu, uadilifu na ujasiri mkubwa kutokana na mazingira hatarishi yaliyopo."La muhimu kuna taatifa maeneo haya wameanza kuja wanyama adimu hivyo ningependa muongeze jitihada hizi mara dufu wanyama hao wasidhurike," alisema.

Katika ziara hiyo wajumbe wa Bodi ya TAWA walipokea taarifa ya timu ya pamoja kati ya TAWA, Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA), Frankfurt Zoological Society ( FZS), TAWIRI na Friedkin Conservation Fund (FCF) katika kuhifadhi na kulinda na kuhifadhi wanyama adimu.Taarifa hiyo iliyowasilishwa na wataalamu Philbert Ngoti wa TANAPA na Gerald Nyaffi wa FZS katika eneo la kitalu kilichopo Maswa Mbono kinachoendeshwa na kampuni ya Tanzania Game Tracker Safaris (TGTS).

Wataalam hao walisema wamefanikiwa katika mradi huo kwa ufadhili wa familia ya Friedkin inayomiliki TGTS ililiyofadhili fedha, vifaa pamoja na helikopta, kazi ijayotarajiwa kuendelea katika maeneo mengine.Katika ziara hiyo TAWA imeridhishwa na utendaji wa Makampuni ya uwindaji na upigaji picha za kitalii, yaliyopo katika maeneo yake kwa kusimamia uhifadhi na ulinzi pamoja na kuchangia miradi ya maendeleo ya wananchi yenye thamani zaidi ya sh 40 bilioni.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori nchini (TAWA), Dk James Wakibara akizungumza na waandishi wa habari juu ya mchango kwa jamii, uhifadhi na kiuchumi wa makampuni ya uwindaji wa kitalii zilizowekeza katika maeneo yao.Maeneo yaliyotembelewa na TAWA ni pamoja na Hifadhi ya Jamii ya Wanyamapori(WMA) ya Makao wilayani Meatu inayosimamiwa na kampuni ya Mwiba Holdings Limited.

Dk Wakibara alisema, licha mchango wa makampuni kwenye jamii, pia TAWA kupitia malipo ya kampuni hizo, imekuwa ikitoa takriban sh 6.5 bilioni kila mwaka kwa vijiji vyenye wawekezaji hao na halmashauri.Makampuni hayo yamewekeza katika baadhi ya maeneo ya vitalu 159 vilivyopo nchini na maeneo ya hifadhi za jamii za wanyamapori (WMA) 38 zilizopo nchini.

"Hizi kampuni za kitalii zina mchango mkubwa sana pia katika uhifadhi wa maeneo haya, hasa katika vita dhidi ya ujangili ikizingatiwa asilimia 95 ya maeneo yaliyohifadhiwa nchini yapo chini ya TAWA"alisema.Alisema kwa sasa mapato ya TAWA kutokana na shughuli za uhifadhi, yamefikia dola 20 lakini kuna mikakati ya kuongeza mapato hayo mara nne zaidi hadi kufikia dola 80.

"kuna dhana potofu kuwa uwindaji wa kitalii ni kumaliza wanyama hili sio kweli, kwani haya makampuni hayajawahi kufikia hata robo kiwango cha kuwinda wanyama ambacho kinatolewa kila mwaka na TAWA na mashirika ya kimataifa"alisema

Mwenyekiti wa bodi ya TAWA, Meja Jenerali mstaafu Hamisi Semfuko alisema mamlaka hiyo ipo katika mabadiliko makubwa ili kuhakikisha jamii inanufaika zaidi ya uhifadhi wa wanyamapori,katika kusaidia miradi ya kijamii ya maji, afya Elimu na uhifadhi.

Mwenyekiti huyo na bodi yake ambao walitembelea pori la Makao, lilipo mpakani mwa Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro na Meatu,alisema wameridhishwa na utendaji wa kampuni ya Mwiba Holding katika eneo hilo
Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi ya Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori nchini (TAWA) Meja Jenerali mstaafu Hamisi Semfuko, Akikagua Gwaride la Askari wa Wanyamapori wa pori la akiba Maswa.
Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi ya Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori nchini (TAWA),Meja Jenerali mstaafu Hamisi Semfuko akiwa katika picha ya pamoja na watendaji waandamizi wa Wizara ya Maliasili washirika wake

No comments:

Post a Comment