Tuesday, June 26, 2018

Uwezo wa Wataalam Kupandikiza Figo Waimarishwa Muhimbili

Katika kipindi cha miezi minane Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imefanikiwa kupandikiza figo wagonjwa 10 kwa mafanikio makubwa ambapo katika kambi ya tatu ya upandikizaji figo, upasuaji umefanywa na watalaam wa MNH kwa zaidi ya silimia 80, huku wakisimamiwa na watalaam kutoka Hospitali ya Saifee ya nchini India.

Akizungumza na waandishi wa habari leo tarehe 26 Juni, 2018 jijini Dar es salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Prof. Lawrence Museru amesema MNH ilianza upandikizaji figo Novemba 2017 kwa kupandikiza mgonjwa mmoja ambapo Aprili 2018 wagonjwa wanne walipandikizwa figo na Juni 24 hadi 25, 2018 wagonjwa watano wamepandikizwa figo.

‘‘Pamoja na upasuaji huo kufanyika, mwaka 2016 hospitali ilipeleka watalaam wake nchini India kujengewa uwezo wa kupandikiza figo hivyo napenda kuwafahamisha kuwa tangu tumeanza upandikizaji wa figo tunaendelea kupata mafanikio makubwa kwa baadhi ya watalaam wetu wa ndani kuwa na uwezo wa kushika hatamu ya kufanya wenyewe katika mchakato mzima wa uchunguzi hadi kupandikiza figo,’’amesema Prof. Museru.

‘‘Tunaamini katika kambi mbili zinazokuja za upasuaji wa kupandikiza figo, madaktari wa upasuaji wazalendo watafikia kiwango cha asilimia 100. Hii ni hatua kubwa sana katika kipindi cha miezi minane kwani mara ya kwanza walikuja watalaam wote wanaohitajika wapatao 15, tulipofanya mara ya pili walipungua wakaja watalaam saba na safari hii mara ya tatu wamepungua wamekuja watano tu, tunaamini wataendelea kupungua katika kambi tatu zijazo na hatimaye kusimama wenyewe na kufanya kwa viwango na ubora uleule,” amesisitiza Prof. Museru.

Kwa upande wake Daktari Bingwa wa magonjwa ya figo kutoka hospitali ya Saifee ya nchini India Dkt. Mustafa Khokhawala amesema Madaktari wa Muhimbili wameshiriki upasuaji huo kwa asilimia kubwa ambapo kati ya wagonjwa watano waliopandikizwa figo, mgonjwa mmoja amepandikizwa na wataalam wa ndani na kwamba hatua hiyo ni nzuri na inaonesha kuwa watalaam wa MNH wanauwezo mkubwa wa kuendelea na upandikizaji.

Naye Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Figo kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili, Onesmo Kisanga amesema wagonjwa wote waliopandikizwa figo pamoja na wale waliochangia figo wanaendelea vizuri na wanafuatiliwa na wataalam kwa ukaribu zaidi.

Pia amesema mahitaji ya wagonjwa wanaohitaji kupandikizwa figo ni makubwa kwani kuna wagonjwa karibu 1000 nchi nzima ambao wanahitaji huduma ya kupandikizwa figo.Upasuaji wa kupandikiza figo kwa wagonjwa 10 hadi hivi sasa umegharimu kiasi cha shilingi milioni 210 sawa na milioni 21 kwa mgonjwa mmoja ambapo kama wangeenda nje ya nchi ingegharimu kiasi cha shilingi Bilioni moja sawa na shilingi milioni 100 kwa kila mgonjwa.

Kabla ya kuanza upandikizaji wa figo hapa nchini Serikali ilipeleka wagonjwa takribani 230 katika kipindi cha miaka 15 iliyopita, hivyo kuanza kwa huduma hii nchini kutaongeza idadi zaidi ya hiyo kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Lawrence Museru akizungumza na waandishi wa habari leo tarehe 26 Juni, 2018 kuhusu wagonjwa watano kupandikizwa figo katika hospitali hii. Kushoto ni Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Figo na Mfumo wa Mkojo, Dkt. Mustafa Khokhawala, Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Mishipa ya Damu, Dkt. Aliasgar Behranwala na Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Figo na Mfumo wa Mkojo, Dkt. Raval Ashiq Ali Ahmad, wote kutoka Hospitali ya Saifee iliyopo Mumbai nchini India. 
Kulia ni Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Figo na Mfumo wa Mkojo, Dkt. Njiku Kim, Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Figo na Mfumo wa Mkojo, Dkt. Victor Sensa naDkt. Isaack Mlatie ambaye pia ni Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Figo na Mfumo wa Mkojo- wote wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) wakiwa kwenye mkutano na waandishi wa habari.
Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Figo na Mfumo wa Mkojo, Dkt. Isaack Mlatie akizungumza na waandishi wa habari leo kuhusu hospitali hii kufanikiwa kupandikiza figo kwa wagonjwa watano.
Baadhi ya wakurugenzi wa Muhimbili wakifuatilia mkutano huo leo.
Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Mishipa ya Damu, Dkt. Aliasgar Behranwala kutoka Hospitali ya Saifee iliyopo Mumbai nchini India na Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Figo na Mfumo wa Mkojo, Dkt. Njiku Kim wa Hospitali ya Taifa Muhimbili wakipandikiza figo mmoja wa wagonjwa watano walipatiwa huduma hiyo.

No comments:

Post a Comment