Monday, June 11, 2018

UWEKEZAJI WENYE MTAZAMO ENDELEVU WA BIASHARA UTAFANIKISHA MPANGO WA KUJENGA TANZANIA YA VIWAND

Lisa akiwa (kushoto) akiwa na mwenzake katika mpango wa GMT, Raj Chandarana wakipanda mti wilayani Hai katika mradi wa mazingira wa TBL.
Lisa (wa pili kutoka kushoto) akiwa na baadhi ya wafanyakazi wenzake wa TBL baada ya kushiriki katika mradi wa mazingira mkoani Kilimanjaro hivi karibuni “Wakati serikali ya Tanzania inakwenda kasi katika kutekeleza mpango wa kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda,kunahitajiwa uwekezaji wenye mipango mikubwa ya kuvifanya viwanda vilivyopo na vinavyoanzishwa kuwa endelevu.

Sio tu kuwekeza kwenye fedha na teknolojia bali kunahitajika kuwekeza katika kupata wataalamu wa kuviendesha kwa kipindi cha sasa na miaka ya mbele ili viweze kuwa endelevu”,anasema Lisa Cheche, mhitimu wa Chuo Kikuu ambaye kwa sasa yupo katika programu ya kipekee, ya mafunzo ya kuwandaa wahitimu wa vyuo vikuu kushika nafasi za uongozi ijulikanayo kama, Global Management Trainee Program (GMT), ya kampuni ya kimataifa ya ABinBev ambayo ni kampuni mama ya Tanzania Breweries Limited Group (TBL Group) akiwa anafanyika kazi katika kiwanda cha (TBL).

Lisa, anaeleza kuwa bila kufanya uwekezaji wenye mtazamo wa kujenga biashara endelevu kwa miaka mingi, kuna hatari ya biashara nyingi hususani viwanda vinavyoanzishwa kutofika mbali; badala yake historia ya nyuma kujirudia ambapo Tanzania ilikuwa na viwanda vingi kuanzia katika awamu ya kwanza ya utawala ambapo vingi vilikufa kutokana na sababu mbalimbali mojawapo ikiwa ni kukosekana kwa mipango endelevu katika uwekezaji. 

 Akiwa msomi aliyehitimu Shahada ya Kwanza ya Sayansi katika mchepuo wa Viwanda, Utawala,Uhusiano katika masuala ya kazi na Kifaransa, kutoka Chuo Kikuu cha Cornell nchini, Marekani, anashauri kuwa kuna haja ya kuanzishwa Progamu mbalimbali za kuwanoa vijana wa kitanzania wahitimu wa vyuo vikuu na vyuo vya ufundi kwa kuwapatia mafunzo ya vitendo kwa ajili ya kuwaanda kushika nafasi za uongozi katika miaka ya mbele. 

 Akiongea kuhusu kupata nafasi ya kujiunga na Programu ya kuwaandaa vijana wahitimu wa vyuo vikuu kushika nafasi za uongozi ya ABInBev na TBL, Lisa, anaeleza kuwa anajivunia kuwa miongoni mwa wahitimu waliochaguliwa kwenye programu hii kwa kuwa ushindani wa kuipata nafasi ulikuwa mkubwa sambamba na mchujo mkali uliofanywa na wataalamu mbalimbali ili kuhakikisha na kujiridhisha kuwa wanachukua watu wenye uwezo,, makini na waliopo tayari kujifunza.

 “Kwa muda mfupi ambao nimeanza mafunzo ya vitendo katika kampuni ya TBL nimegundua kuwa programu hii ni muhimu sana kwa kuwa katika kipindi cha muda mfupi nimejifunza mambo mengi ambayo huko nyuma sikupata kukumbana nayo na kila kukicha nakutana na mambo mengi mageni ya kujifunza”, anasema Lisam

Anasema moja ya ndoto kubwa aliyokuwa nayo katika maisha yake ni kufanya kazi katika kampuni kubwa na yenye mifumo mizuri ya kazi, jambo ambalo limetimia kutokana na mazingira ya kazi aliyoyakuta kwenye kampuni ya TBL,amekuta na timu ya wafanyakazi waliobobea katika fani mbalimbali na ambao wako tayari kutoa utaalamu wao kwa wengine wanaojifunza. 

 Kitu kingine ambacho kinamfurahisha Lisa ,katika safari yake ya mafunzo kupitia programu ya GMT ni kukuta kampuni aliyojiunga nayo, ina mifumo thabiti iliyotokana na uwekezaji makini,kuanzia mifumo ya uzalishaji,usambazaji wa bidhaa,masoko na mauzo na kuwa na sera zenye mtazamo wa kujenga jamii endelevu zinazoenda sambamba na utekelezaji wa malengo endelevu ya milenia ya umoja wa mataifa.

 “Inafurahisha kuona kampuni inayapa kipaumbele masuala ya msingi katika kujenga biashara endelevu kama vile utunzaji wa mazingira na vyanzo vya maji,usalama wa wafanyakazi wake ,kushirikiana na jamii zilizopo katika maeneo inakofanyia biashara zake kama ambavyo inafanya kazi na wakulima wa zao la Shahiri na mazao mengine,kuhakikisha inapata malighafi zake nchini ,kuendesha mafunzo ya ujasiriamali wadogo wanaosambaza biashara zake ili nao biashara zao ziwe endelevu bila kusahau kufanikisha miradi mbalimbali ya kusaidia jamii mojawapo ikiwa ni miradi ya maji ,kelimisha jamii matumizi ya vinywaji kistaarabu na kushirikiana na serikali na wadau wengine kutoa elimu ya usalama barabarani” .

Anaeleza kuwa katika safari yake ya mafunzo atafanya kazi katika vitengo mbalimbali vya kampuni ndani na nje ya nchi ili kupata ujuzi,na katika kipindi cha muda mfupi tayari ameshiriki katika miradi ya mazingira,ukuzaji wa vipaji vya wanafunzi na mradi wa promosheni ya bia ya Kilimanjaro inayowezesha washindi kwenda nchini Urusi,kushuhudia mashindano ya kombe la Dunia mubashara. 

 Lisa, anaeleza kuwa anaamini kuwa hadi kufikia mwishoni mwa programu hii ya mafunzo atakuwa amejifunza mambo mengi yatakayomsaidia katika safari yake ndefu ya kukabiliana na changamoto za uongozi sambamba na ubunifu na kutoa mawazo ya kitaalamu yanayowezesha kukabili changamoto na kusonga mbele kibiashara kwa mafanikio.

 Lisa,alimalizia kwa kutoa ushauri kwa wawekezaji wengine nchini kuwa na mtazamo wa kujenga biashara endelevu sambamba na kuwa na programu za kuandaa wataalamu wa kuendesha biashara wanaopata mafunzo ya vitendo kutoka kwa wataalamu waliopo kama ilivyo programu ya GMT ya ABInBev na TBL.”Programu kama hii ni muhimu kwa kuwanoa vijana wasomi kupata ujuzi na uzoefu zaidi,natamani kuona pia idadi ya vijana wanaochukuliwa katika Programu hii kuongezwa zaidi ya sasa ili inufaishe vijana wengi zaidi”alisisitiza. 

 Akiongea juu ya Programu ya Global Management Trainee (GMT),Mkurugenzi wa Raslimali Watu wa TBL,David Magese,alisema hii ni progamu inayolenga vijana wasomi ambapo wanaobahatika kujiunga nayo hupatiwa mafunzo ya vitendo kwa kipindi cha miezi 10 kwa ajili ya kuwaandaa kushika nafasi za juu za uongozi ndani ya biashara za kampuni mama ya TBL ya ABIn Bev. 

 Alisema programu ni moja ya mkakati wa kampuni wa kuendeleza vipaji vya vijana na kuongeza kuwa waliochaguliwa kwenye GMT mwaka huu ambao ni 2 kwa hapa nchini mbali na kupata mafunzo ndani ya nchi pia watapata mafunzo kwenye viwanda mbalimbali vya kampuni vilivyopo nje ya nchi kwa kuwa wanaandaliwa kuwa viongozi sio kwa hapa Tanzania bali wanaweza kufanya kazi katika nchi yoyote. 

 Magese,alimalizia kwa kusema kuwa kampuni itaendelea na mpango wa kuendeleza wahitimu wa vyuo vikuu nchini kwa kuwapatia fursa za kukuza vipaji vyao kupitia programu hii ya GMT ambayo imepata mafanikio makubwa katika nchi mbalimbali zilipo biashara za kampuni ya ABInBev.

No comments:

Post a Comment