Monday, June 18, 2018

TASAF YAIVUTIA NIGERIA NA SUDAN KUSINI,WAJA NCHINI KUJIFUNZA UTEKELEZAJI WA MPANGO WA KUNUSURU KAYA MASKINI.

Na.Estom Sanga-TASAF. 

Mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Tano katika kutekeleza Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii –TASAF yameanza kuvutia Mataifa mbalimbali ya kiafrika kuja nchini kujifunza namna Mpango huo unavyotekelezwa. 

Miongoni mwa nchi ambazo zimetuma wataalamu kujifunza namna serikali ya Tanzania kupitia TASAF inavyotekeleza Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaohudumia takribani kaya Milioni Moja na Laki Moja ni pamoja na Sudan Kusini na Nigeria. 

Wakizungumza kwa nyakati tofauti viongozi wa Ujumbe huo ambao umeanza ziara katika Ofisi za TASAF jijini Dar es salaam,wamepongeza hatua ya Serikali ya Tanzania kutekeleza Mpango huo ambao wamesema unawagusa moja kwa moja wananchi wanaokabiliwa na umaskini. 

Wamesema mkakati huo wa kupunguza umaskini kwa njia ya hifadhi ya jamii unaonyesha mafanikio makubwa nchini Tanzania na hivyo kuvutia nchi nyingine kuja kujifunza namna Mpango huo uliyofanikiwa. 

Aidha wajumbe hao kutoka Sudan Kusini na Nigeria wamesema utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaofanywa na Serikali ya Tanzania kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF umefanikiwa kwa kiwango kikubwa kutokana na dhamira ya dhati inayoonyeshwa na serikali katika kupambana na umaskini kwa kuwashirikisha wananchi. 

Akitoa maelezo kwa Wageni hao,Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF,Ladislaus Mwamanga amesema mafanikio ya shughuli za Mpango yametokana kwa kiasi kikubwa na ushirikishaji wa Wananchi tangu katika hatua za awali hadi sasa,huku akiipongeza Serikali kwa kuratibu kwa ufanisi utekelezaji wa shughuli za Mpango huo. 

Ametaja baadhi ya mafanikio ya Mpango kuwa ni kuhamaisha walengwa wa Mpango kufanya kazi za uzalishaji mali kwa kutumia ruzuku wanayoipata na kuboresha makazi yao kwa kujenga nyumba bora, huku msisitizo pia ukiwekwa katiamsekta za elimu, afya na lishe hususani kwa watoto na mama wajawazito. 

Ujumbe huo utapata fursa ya kutembelea mkoa wa Dar es salaam na Pwani ambako utakutana na Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini na kujionea namna wanavyonufaika na Mpango huo.
Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Ladislaus Mwamanga (aliyesimama) akizungumza na wageni kutoka Sudan Kusini na Nigeria (hawapo pichani) kwenye ukumbi wa mikutano wa TASAF jijijini Dar es salaam,wageni hao wako nchini kujifunza namna TASAF inavyotekeleza Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini.
Mmoja wa wageni kutoka Sudan Kusini akizungumza kwenye ukumbi wa mikutano wa TASAF jijini Dar es salaam juu ya azma ya serikali yao kujifunza utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ili kwenda kuutekeleza nchini kwao.
Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Ladislaus Mwamanga (aliyesimama) akizungumza na wageni kutoka Sudan Kusini na Nigeria (hawapo pichani) kwenye ukumbi wa mikutano wa TASAF jijijini Dar es salaam,wageni hao wako nchini kujifunza namna TASAF inavyotekeleza Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini
Wajumbe kutoka Sudan Kusini,Nigeria,na baadhi ya Watumishi wa TASAF makao makuu wakiwa katika picha ya pamoja nje ya ofisi za TASAF jijini Dar es salaam.

No comments:

Post a Comment