Wednesday, June 20, 2018

TAARIFA KUHUSU KUHAMISHWA SOKO LA KATENGELE WILAYANI ILEJE KUPISHA MSITU WA HIFADHI YA MITI



HALMASHAURI YA WILAYA YA ILEJE

Simu.  Na. 25 -   2570063
Ofisi ya Mkurugenzi
Mtendaji (W)
S. L. P.  2,
ILEJE.

19/06/ 2018
Faksi. Na.  25 - 2570042
Barua Pepe:  ded-ileje@iwayafrica.com                  
              : mipangoilejedc@yahoo.co

JIOGRAFIA/MAHALI LILIPO SOKO

Soko la Katengele linapatikana katika vilele vya milima yenye msitu ujulikanao
kama Iyondo - Mswima wenye miti ya asili na ile ya kupandwa ukizungukwa na
Kata za Kalembo, Sange, Ibaba, Ngulugulu na Kufule.
Pia soko hili hupitiwa na  Barabara ya Mkoa ya Ibungu - Ileje hadi  
KKK Wilayani Rungwe ikiligawa katikati na kuacha upande mmoja kuwa  
Kata ya Sange na upande mwingine Kata za Kafule na Sange.

HISTORIA YA SOKO:

Soko hili limekuwepo kwa muda mrefu likianzia kabla ya wakoloni,
wakati wa ukoloni na baada ya Uhuru wa wetu mnamo 1961 hadi sasa.
Katengele awali palijulikana kama Katengele Bhalindu (yaani mabinti)
ikielezwa kuwa ndipo palikutanisha vijana waliotaka kuoa au kuolewa
kwa kabila la Wandali ambalo ni kubwa kwa Wilaya hii na maarufu kwa
Mkoa wa Songwe na Mbeya kutokana na uchapaji kazi
hususani zile za kutumia nguvu.
Kuhusu “Katengele Bhalindu” hapa ndipo palipokuwa soko la awali
pakiwa na msitu mdogo ambapo inasemekana kuwa mabinti wawili
walipotea bila kupatikana katika mazingira ya kutatanisha kwa muda
mrefu na imebaki kuwa simulizi inayoendelea  kila linapotajwa neno katengele.
Awali lilikutanisha watu wa maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Ileje na
Wilaya za Mbozi, Rungwe na Kyela wakiuza bidhaa kwa fedha tasilimu
pamoja na biashara ya kubadilishana bidhaa kwa bidhaa.  
Kwa miaka ya hivi karibuni limekuwa maarufu sana kwa biashara
ya ng’ombe, bidhaa za asili pamoja na zile za viwandani likiwavutia
hata raia wa Nchi jirani ya Malawi.

KUANZISHWA KWA MRADI WA SHAMBA LA MITI

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wakala wa Misitu (TFS) imeamua
kuanzisha Shamba la Miti la Iyondo - Mswima ukiwa ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi
ya 2015/2020 ibara ya 31 vifungu vya b,c,d,e na f kuhusiana sekta ya Maliasili.
Kwa mujibu wa Meneja wa Mradi wa Iyondo-Mswima Ndg. Deograsian Kavishe
upandaji miti utaanza rasmi katika mwaka wa Fedha 2018/2019 ikiwa baadhi ya
kazi zilianza kutekelezwa na Mradi katika mwaka wa fedha 2017/2018.
Kuanzishwa kwa shamba hili la Katengele kunaifanya Tanzania kuwa na
mashamba ya miti ya kupandwa 23 yakiwa yanapatikana katika Kanda
mbalimbali kati ya hayo manne yapo katika hatua ya uanzishwaji likiwemo
hilo la Iyondo – Mswima (Ileje).

KUHAMISHWA KWA MNADA WA SOKO LA KATENGELE

Kutokana na soko hili kuwa ndani ya msitu wa hifadhi na kuweza kufikia
malengo yaliyokusudiwa kwa kufuata Kanuni, Sheria na taratibu za
uanzishwaji na uendeshaji wa miradi ya upandaji miti hapa Nchini, soko
hilo halistahili  kuendelea kuwepo mahali lilipo, hivyo linatakiwa
kuhamishiwa sehemu nyingine nje ya hifadhi zikiwemo kaya 13
zinazoishi ndani ya eneo hilo. Ujenzi wa miundombinu katika eneo
lililochaguliwa utafanywa na serikali kupitia wakala wa Misitu (TFS).

MICHAKATO YA KUHAMISHA SOKO

Ili kuendeleza mahusiano mazuri na wadau mbalimbali wa maendeleo TFS imeshirikisha
Baraza la Madiwani, wataalam wa Halmashauri pamoja na Serikali Kuu.
Michakato hiyo ilianzia kwenye vikao vya CMT, Kamati ya Uchumi Ujenzi na
Mazingira, Kamati ya Fedha Uongozi na Mipango pamoja na Baraza la
Madiwani ambalo liliridhia kuhama kwa Mnada wa Soko hilo kutoka mahali
lilipo na kwenda sehemu nyingine.
KIKAO CHA BARAZA LA MADIWANI
Baraza la Madiwani baada ya kujadili na kupitia mapendekezo ya vikao vilivyotangulia
kisheria liliridhia juu ya kuhama kwa soko la Katengele kutoka mahali lilipo na kwenda
Njiapanda ya Shule ya Msingi Mbangala katika barabara ya Ibaba - Katengele ili
kupisha uanzishwaji wa Mradi wa Shamba la Miti la Iyondo - Mswima.

Makubaliano hayo yalifikiwa baada ya upigaji kura kufanyika ambapo Wah.
Madiwani wane waliliridhia mnada wa Katengele uhamishiwe eneo la Ghala - Sange
huku Madiwani 18 wakiridhia Mnada wa Katengele uhamishiwe Njiapanda ya Shule
ya Msingi Mbangala.

MAONI YA BARAZA LA MADIWANI

Baraza lilishauri kuwa wakati wa kuhamisha Mnada wa Katengele ufanyike utaratibu
wa kukutanisha wananchi waliokuwa katika eneo la mnada pamoja na wadau wa
mnada huo wakiwemo viongozi wa maeneo yanayozunguka mnada, machifu na Wah.
Madiwani ili kuwajengea uelewa na kuwajulisha mchakato wa kuhamisha mnada.
Aidha ilishauriwa kutoa mwaliko kwa wadau kutoka maeneo mbalimbali ili
kuwajulisha juu ya mabadiliko ya eneo jipya la mnada

GHARAMA ZA UJENZI WA MIUNDO MBINU KWENYE ENEO JIPYA LA MNADA

Serikali kupitia Wakala wa Misitu (TFS) inatarajia kujenga miundombinu katika
eneo jipya la mnada ili kutoathiri bajeti ya Halmashauri ambayo tayari ilishatekelezwa
kwenye soko la awali ukiwemo ujenzi wa machinjio.

MANUFAA YA MRADI WA UPANDAJI MITI WA IYONDO MSWIMA-ILEJE

Meneja wa Mradi huu Ndg. Deograsian Kavishe alibainisha faida kadha zitakazotokana
na kuwepo kwa Mradi huu kiwilaya, kitaifa na kimataifa ambazo ni pamoja na:
Ajira kwa jamii ambapo mpaka sasa wananchi wa maeneo hayo wameshaanza
kufanya kazi za awali katika Mradi huo, ongezeko la viwanda ndani na nje ya Wilaya
vinavyochakata mazao ya magogo, kukabiliana na ongezeko la uvunaji miti michanga
(pre mature) na  jamii kupata elimu ya upandaji miti.
Faida zingine ni uanzishwaji na uboreshaji wa huduma za jamii, kuwezesha
Mashamba Darasa ya miti kwa Taasisi za Serikali kama vile shule na magereza
pamoja na kugawa miche ya miti kwa jamii ikiwa ni njia mojawapo ya
uhamasishaji wa upandaji miti.
Kuanzishwa kwa Mradi huu kutaitangaza Ileje kitaifa na kimataifa
kutokana na shughuli za kitalii zinazoweza kufanywa katika eneo hilo
lenye jiografia ya kipekee katika Mkoa wa Songwe pamoja na uwepo wa
nyani aina ya mbega ambao hupatikana sehemu zenye baridi kali.

CHANGAMOTO ZA UANZISHWAJI WA SHAMBA LA IYONDO MSWIMA


Zipo chanagamoto kadhaa zinazokabili juu ya kuanzishwa kwa Mradi huu, moja ni
mshituko na hofu kwa watumiaji wa soko hilo ambao wanaona giza mbele yao
hili linatokana na mazoea ya uendeshaji wa mambo.
Pia hofu nyingine ni juu ya hatima ya miti ya watu binafsi ambayo imebainika
kuwa ipo ndani ya hifadhi ya Msitu wa Iyondo – Mswima ambao walitumia
gharama kubwa katka kuipanda ikiwa ni sehemu ya uwekezaji.

HITIMISHO

Kila jambo linapoanzishwa huwa na changomoto zake, hata ujenzi wa barabara ya
Mpembe - Isongole ambayo kwa muda mrefu tumekuwa tukiihitaji imeshawathiri
baadhi ya watu hata kuhamia kwa Serikali yetu huko Dodoma kumewaathiri baadhi ya watu.
Kinachotakiwa ni kutathmini faida na hasara juu ya jambo tunalolihitaji si lazima
tulio hai sasa tukanufaika bali twaweza kuwa washiriki wa ujenzi wa
misingi imara kwa vizazi vijavyo kama walivyofanya babu zetu ambao
licha ya kutokuwa na “Elimu ya Kimagharibi” kuna mambo walifanya
ambayo mpaka leo tunayafaidi ukiwemo ulinzi wa mazingira.
Kamwe tusikubali ujio wa miradi kama hii kutugawa  bali tukae
pamoja kwa kujadiliana ili tuweze kuimba wimbo mmoja kwa kufuata midundo
ya ngoma inayopigwa.

Imeandaliwa na Daniel J. Mwambene
KITENGO CHA HABARI, ILEJE
 Sehemu ya Msitu wa Iyondo-Mswima ikionesha msitu wa asili na  kupandwa.
 Eneo la Mnada wa Katengele Wilayani Ileje mkoani Songwe unaotakiwa kuhamishwa ili kupisha Mradi wa Upandaji Miti.
 Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje Ndugu Haji Mnasi (aliyesimama) akizungumza kwenye Baraza Maalum kuhusu Mnada wa Katengele
 Eneo la Njiapanda ya Shule ya Msingi Mbangala panapotarajiwa kuhamishiwa Mnada wa Katengele.
 Askari Jeshi USU Deograsian Kavishe ambaye ni Meneja Mradiwa Upandaji Miti wa Iyondo-Mswima  akizungumza kwenye kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Ileje.

 Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje  Mhe.Ubatizo Songa akiongoza Wahe. Madiwani na Wataalam  wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje walipotembelea eneo la Mradiwa Upandaji Miti la Iyondo-Mswima

Kitalu cha miti kilichopo Katengele-Ileje kikitarajiwa kubadilisha sura ya msitu wa Iyondo-Mswima wiyani Ileje

No comments:

Post a Comment