Friday, June 22, 2018

SUDAN KUSINI NA NIGERIA WAPONGEZA SERIKALI YA TANZANIA KWA KUANZISHA MPANGO WA KUNUSURU KAYA MASKINI KUPITIA TASAF.


Na Estom Sanga- TASAF.


Wataalam wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii kutoka nchini Sudan Kusini na Nigeria wameipongeza Serikali ya Tanzania kwa uamuzi wake wa kukuza sekta hiyo inayolenga kuzikwamua kaya za wananchi ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakikabiliwa na umaskini mkubwa wa kipato.


Wataalamu hao ambao wako nchini kuona namna sekta hiyo inavyotekelezwa kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF-ambayo inatekeleza Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini –PSSN-wamesema Mpango huo unawagusa moja kwa moja wananchi hususani wanaoishi katika mazingira ya umaskini uliokithiri.


Wamesema hamasa waliyoiona baada ya kuwatembelea baadhi ya Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika Wilaya za Temeke,Ilala jijini Dar es salaam na Kibaha na Bagamoyo mkoani Pwani katika kujiletea maendeleo kwa kutumia fursa zilizoko kwenye Mpango huo zimeonyesha kuwa katika kipindi kifupi cha utekelezaji wa Mpango huo maisha yao yameanza kuboreshwa.


Miongoni mwa mambo yaliyowavutia Wataalam hao ni namna TASAF inavyoshirikisha Sekta nyingine za serikali kuwafikia Walengwa na uwezo  wa Watumishi wa Taasisi hiyo katika kuwatembelea Walengwa na kuwahamasisha kufanya kazi za uzalishaji mali ili kufikia malengo na kuboresha maisha ya Walengwa hao.


Aidha suala la ujenzi wa makazi ya Walengwa kwa kutumia ruzuku wanayopata kutoka TASAF limewashangaza Wataalamu hao kwani katika maeneo waliyotembelea wamebaini kuwa Sehemu kubwa ya Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wamekuwa wakidunduliza fedha na kisha kununua vifaa vya ujenzi wa nyumba hususani mabati,na saruji ili kuboresha makazi yao.


“Hili ni jambo jema ambalo nchi nyingine barani Afrika zinapaswa kuliiga kwani suala la makazi bora kwa wananchi wetu ni changamoto kubwa katika nchi nyingi za kiafrika” amesema mmoja wa Wataalam hao kutoka Sudan Kusini.Kuhusu suala la Elimu, Afya na Lishe, wataalam hao wamesema Serikali ya Tanzania Kupitia TASAF imefanya uamuzi sahihi wa kufanya mambo hayo kuwa miongoni mwa masharti ya kutekelezwa na Walengwa wa Mpango huo wa Kunusuru Kaya ,mambo ambayo wamesema ni ya msingi katika kujenga rasilimali Watu. 


Akizungumza na Wataalamu hao Mkuu wa wilaya ya Kibaha Bi. Assumpta Mshama amesema Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaotekelezwa na TASAF umekuwa chachu muhimu katika kuwahamasisha wananchi kufanya kazi na kujiletea maendeleo na kusema wilaya yake imejipanga kikamilifu kufuatilia utekelezaji wa Mpango huo wa aina yake kupata kutekelezwa nchini.


Wataalam hao wa Sekta ya Hifadhi ya Jamiii kutoka Sudan Kusini na Nigeria wamekuwapo nchini kwa takriban wiki moja kwa lengo la kujifunza namna Tanzania ilivyofanikiwa kutekeleza Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kupitia TASAF ili kwenda kutekeleza katika nchi hizo.

 Baadhi ya Walengwa wa TASAF katika kijiji cha Disunyala wilaya ya Kibaha wakiwa katika kitalu cha miche ya mboga (nyanya,pilipili hoho) wanazozalisha kwa lengo la kujiongezea kipato.
 Baadhi ya Wataalam wa sekta ya hifadhi ya Jamii kutoka Sudan Kusini wakiangalia matuta yaliyolimwa na Walengwa wa TASAF yanayotarajiwa kupangwa miche ya mboga mboga ikiwa ni mojawapo ya shughuli za uzalishaji mali ili kujiongezea kipato.
 Mmoja wa Walengwa wa TASAF akiwa amebeba sehemu ya kuku wa kienyeji anaowafuga kwa kutumia sehemu ya ruzuku anayoipata kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya maskini.
 Baadhi wageni kutoka Sudan Kusini wakiangalia tanki lililojengwa na TASAF katika kijiji cha Disunyala wilaya ya Kibaha kwa lengo la kuvuna maji ya mvua yanayotumika kumwagilia bustani ya mboga mboga ikiwa ni mojawapo ya miradi ya kuwaongezea kipato Walengwa wake. 
 Pichani ni baadhi ya Wataalamu wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii kutoka nchini Sudan Kusini wakiwa katika eneo la Shamba darasa la Muhogo lililoanzishwa na TASAF kwa lengo la kuhamasisha walengwa na wananchi wa eneo hilo kuzalisha muhogo kwa wingi kama njia mojawapo ya kujiongezea kipato. 
Mkuu wa wilaya ya Kibaha,Bi. Assumpta Mshama(Watatu  kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wataalam wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii kutoka Sudan Kusini walimtembelea ofisini kwake kabla ya kwenda kukutana na Walengwa wa Mpango huo.


No comments:

Post a Comment