Friday, June 29, 2018

SERIKALI YAUTAKA MFUKO WA TAIFA WA BIMA YA AFYA KUONGEZA KASI YA KUBUNI MIKAKATI NA MABORESHO


Na Mwandishi Wetu, Morogoro

SERIKALI imeutaka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), kuongeza kasi katika kubuni mikakati na maboresho ikiwemo taratibu za kujiunga ambazo zitawawezesha wananchi wengi zaidi kunufaika na huduma zake.

Agizo hilo limetolewa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile wakati akizindua Baraza la Pili la Wafanyakazi wa NHIF mjini Morogoro ambapo amesema kuwa mwelekeo wa Serikali kwa sasa ni kuhakikisha watu wote wanakuwa na bima ya afya.

"Serikali ya Awamu ya Tano imeweka nguvu kubwa katika utoaji wa huduma bora za matibabu kwa wananchi hivyo ninawaagiza muongeze kasi katika ubunifu na maboresho mbalimbali ambayo yatakwenda sambamba na matarajio ya Serikali yanayolenga wananchi wengi zaidi kuwa katika mfumo wa kupata huduma za matibabu kwa mfumo wa bima ya afya,” amesema Dk. Ndugulile.

Amewataka watumishi wa Mfuko hususan Mameneja wa Mikoa kutokaa maofisini mwao na badala yake watoke nje kwa ajili ya kuhamasisha wananchi, kuangalia huduma wanazopata katika vituo vya kutolea huduma pamoja na kushughulikia changamoto zinazojitokeza katika maeneo mbalimbali.

Akizungumzia utendaji kazi wa Baraza, amewataka wajumbe wa baraza hilo kutambua wajibu wao ndani ya baraza kwa kuwa ni chombo muhimu katika kubuni na kuweka mipango thabiti ya kuendesha taasisi ambayo ina dhamana kubwa ya kuangalia ama kushughulikia huduma za matibabu kwa wanachama.

Amesema kwa sasa Serikali iko katika mchakato wa kuwasilisha muswada wa sheria ambao utawezesha wananchi wote kuwa katika utaratibu wa kupata huduma za matibabu kwa mfumo wa bima ya afya.

Akitoa salaam za NHIF, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko huo Bernard Konga amemhakikishia Naibu Waziri kuwa, Mfuko unaendelea kutekeleza na kuunda mipango ya kuongeza wigo wa wananchi kunufaika na huduma zake.

Amesema Julai mwaka huu, Mfuko unatarajia kuzindua ‘Ushirika Afya’ ili kuwezesha wakulima katika vyama vyao vya ushirika kunufaika na bima ya afya huku uundaji wa vifurushi mbalimbali ukiendelea.

"Mathalan, Mpango wa kulipa michango ya bima kidogo kidogo kwa kudunduliza kwa lengo la kuwawezesha wananchi wengi zaidi kunufaika na huduma za Mfuko. “Tumejipanga na hivi karibuni tutazindua huduma mbalimbali na hii yote ni mikakati ya kuelekea bima ya afya kwa wote kwa lengo la kuwahakikishia wananchi upatikanaji wa huduma za matibabu wakati wowote,” alisema Konga.

Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile akizindua Baraza la Pili la Wafanyakazi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), mkoani Morogoro.
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile akimkabidhi nyaraka za kuongoza Baraza hilo, Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bernard Konga.
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile akisisitiza jambo kwa wajumbe wa Baraza hilo.
Wajumbe wa Baraza la Pili la NHIF, wakionyesha ishara ya mshikamano baada ya kuzinduliwa rasmi kwa Baraza hilo.
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile akiteta jambo na Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bernard Konga.
Sehemu ya Wajumbe wa Baraza wakionyesha ishara ya mshikamano
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile katika picha ya pamoja na Mameneja wa NHIF Mikoani.
 

No comments:

Post a Comment