Monday, June 25, 2018

Rock City Marathon yazinduliwa jijini Mwanza

Rock City Marathon yazinduliwa jijini Mwanza 

Mwanza, 24 Juni, 2018: Msimu wa tisa wa mbio za Rock City Marathon umezinduliwa rasmi jijini Mwanza mwishoni mwa wiki hii huku wito ukitolewa kwa wadau wa utalii na michezo nchini hususani Kanda ya Ziwa kutumia mbio hizo kutangaza fursa na vivutio vya utalii vinavyopatikana katika kanda hiyo. 

Uzinduzi wa mbio hizo zinazoratibiwa na kampuni ya Capital Plus International kwa kushirikiana na Chama cha Riadha Mkoa wa Mwanza (MWAA) ulihusisha pia wawakilishi wa wakuu wa mikoa yote ya kanda ya Ziwa ikiwa ni mikoa ya Simiyu, Geita, Shinyanga, Mara na Kagera. 

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Bw Mongella katika hafla fupi ya uzinduzi huo iliyofanyika ukumbi wa Rock City Mall jijini humo, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Bi. Merry Tesha alisema ipo haja ya wadau wa utalii na michezo katika kanda hiyo kuhakikisha kwamba wanayatumia vizuri mashindano hayo katika kuhakikisha fursa na vivutio vya utalii vilivyopo kwenye ukanda huo vinatangazwa ipasavyo. 

“Ndio maana serikali tunafarijika sana tunapoona sekta binafsi inajiinua na kubuni mbinu bora kabisa hasa kupitia michezo ili kuiboresha zaidi sekta hii ya utalii hususani kwa kanda yetu ya Ziwa ambayo kwa sasa ipo kwenye mabadiliko makubwa,’’ Alisema. 

Akizungumzia maendeleo ya mchezo huo Bi Tesha alisema ipo haja kwa wadau kuhakikisha wanatumia vizuri mwamko wa mkubwa mashirika na taasisi mbalimbali hapa nchini ambazo zimeamua kuunga mkono mchezo huo katika kuinua vipaji vipya. 

“Niombe sana kila kiongozi mwenye dhamana ya kusimamia mchezo huu katika ngazi tofauti tofauti, idara mbali mbali na vyama mbali mbali, tulirudishe taifa kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.’’ Alisema. 

Mbio hizo zinazozidi kujiongezea umaarufu kila mwaka tayari zimefanikiwa kuwavutia baadhi ya wadhamini ikiwa ni pamoja na kampuni za TIPER, PUMA Energy Tanzania, New Mwanza Hotel, Precision Air, KK Security, CF Hospital, Rock City Mall, Dasani, Metro Fm, Global Education Link, Barmedas TV, Gold Crest Hotel, NSSF, EF Outdoor, na SDS huku wengine wakionyesha nia ya kudhamini mbio hizo. 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati ya Maandalizi ya mbio hizo Bw Zenno Ngowi alisema uzinduzi wa mbio hizo zinazotarajia kufanyika Oktoba 28 mwaka huu kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza umefanyika mapema ili kuruhusu wadau wote wapate muda wa kutosha katika kujiandaa kwa ajili ya ushiriki. 

“Lakini pia katika msimu huu wa mbio hizi tumefungua milango zaidi kwa wadau wa maliasili na utalii ambapo si tu kwamba wataweza kushiriki katika mbio hizo bali pia watapata fursa ya kufanya maonyesho ya utalii pamoja kutoa elimu zaidi kuhusu fursa za kitalii pamoja na kutangaza vivutio vya utalii vinavyopatikana katika kanda hiyo.’’ Alisema. 

Alisema kanda ya Ziwa kwa ujumla ina vivutio vingi vya kihistoria ambavyo vinaweza kutumika kuimarisha sekta ya utalii wa ndani na nje huku akiongeza kuwa ukaribu uliopo baina ya jiji la Mwanza na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ni sababu tosha ya mji huo kuvutia watalii wengi zaidi ikilinganishwa na mikoa mingine iliyo nje ya kanda ya Ziwa.
 Mgeni rasmi ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Bi. Merry Tesha (katikati) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa msimu wa tisa wa mbio za Rock City Marathon 2018  kwenye hafla fupi iliyofanyika ukumbi wa Rock City Mall jijini Mwanza mwishoni mwa wiki. Wanaoshuhudia ni pamoja na Mwenyekiti wa mbio hizo, Zenno Ngowi, (Kushoto kwake), Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Filbert Bayi (alievaa suti nyeusi) pamoja na Mwakilishi wa Chama cha Riadha Mkoa wa Mwanza (MWAA), Benjamini Nyagabona (alivaa kofia). 
 Mgeni rasmi ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Bi. Merry Tesha akizungumza kwenye uzinduzi huo pamoja na mambo mengine alitoa wito kwa wadau wa utalii na michezo nchini hususani Kanda ya Ziwa kutumia mbio hizo kutangaza fursa na vivutio vya utalii vinavyopatikana katika kanda hiyo.
 Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Filbert Bayi akizungumza kwenye uzinduzi huo.
 Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya mbio za Rock City Marathon Bw Zenno Ngowi akizungumza kwenye hafla hiyo.
 Mgeni rasmi ambaye Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Bi. Merry Tesha akiwa kwenye picha ya pamoja na wawakilishi wa mikoa yote ya Kanda ya Ziwa waliohudhuria uzinduzi huo.
 Mgeni rasmi ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Bi. Merry Tesha (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya wadhamini wa mbio hizo. Miongoni mwao ni pamoja na mwakilishi wa KK Security Bw Meshack Richard (wapili kushoto),  Mwakilishi wa Bodi ya Utalii Tanzania Bi Gloria Munhambo (wa kwanza kushoto) pamoja na Mwakilishi wa Radio Metro fm, Bw Maganga James (wa pili kulia).
 Wawakilishi wa klabu za wakimbiaji katika mkoa wa Mwanza wakiwa kwenye picha ya pamoja na mgeni rasmi.
 Wawakilishi wa klabu za wakimbiaji katika mkoa wa Mwanza wakiwa kwenye picha ya pamoja na mgeni rasmi.
Wageni waalikwa wakifuatilia kwa umakini uzinduzi huo.

No comments:

Post a Comment