Monday, June 25, 2018

MKURUGENZI MTENDAJI WA TASAF AWAFUNDA MAAFISA UFUATILIAJI-TMOs.

Na Estom Sanga-TASAF.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF-bwana Ladislaus Mwamanga amewataka Maafisa Ufuatiliaji wa Mfuko huo –TMOs- kutekeleza majukumu yao kwa uaminifu na kuzingatia maslahi ya taifa .

Akifungua mafunzo ya Maafisa Ufuatiliaji kutoka mikoa ya Arusha, ,Kilimanjaro,Singida,Tanga , Mbeya ,Iringa,Katavi,Njombe,Songwe ,Ruvuma na Rukwa katika ofisi za TASAF jijini Dar es salaam ,Mwamanga amesema utendaji kazi wa Watumishi hao unapaswa kuendana na matakwa ya Serikali ya kuhimiza uwajibikaji na kufanya kazi kwa kujituma kwa maslahi ya Wananchi.

Aidha Mkurugenzi Mtendaji huyo wa TASAF amesema maeneo ya Utekelezaji wa Shughuli za Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini nchini kote yameonyesha mafanikio ya kujivunia na hivyo kinachotakiwa kwa sasa ni kuandaa mazingira wezeshi na kuwapatia mbinu sahihi Walengwa za kuendesha shughuli za uzalishaji mali ili hatimaye waweze kuondokana na umaskini. 

Bwana Mwamanga pia amewaagiza Maafisa Ufuatiliaji hao kujenga mahusiano mema na Idara nyingine zilizoko kwenye maeneo yao ya kazi ili kuweka mazingira rafiki kwao kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi unaokusudiwa.Ameonya kuwa pale ambapo utendaji kazi wa Maafisa hao utabainika kutoridhisha , Uongozi hautasita kuchukuwa hatua zinazopaswa kulingana na taratibu za utumishi wa Umma , kwani amesema Wananchi hususani Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wanahitaji huduma bora na si vinginevyo.

Mafunzo hayo yanayotolewa kwa Kanda ,yanaendeshwa na Wataalamu kutoka Chuo cha Uhasibu Arusha yanalenga kuwapatia Maafisa Ufuatiliaji hao stadi sahihi za uongozi na kuboresha usimamizi mzuri wa shughuli za Taasisi, mbinu bora ya usimamizi wa shughuli za Mpango na kutatua changamoto zinazojitokeza kwa wakati na ufanisi .

Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF unaendesha Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaohudumia takribani Kaya Milioni Moja na Laki Moja nchini kote kwa lengo la kuboresha maisha ya kaya husika huku mkazo maalum ukiwekwa katika sekta za Elimu, Afya,Lishe na Uzalishaji Mali ili kuongeza kipato cha Walenga na jamii inayowazunguka.
Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF,Ladislaus Mwamanga (aliyesimama) akitoa hotuba ya ufunguzi kwenye mafunzo ya Maafisa Ufuatiliaji wa TASAF yanayofanyika kwenye ukumbi wa taasisi hiyo jijini Dar es salaam.
Baadhi ya Maafisa Ufuatiliaji wa TASAF –TMOs wakisikiliza hotuba ya ufunguzi wa Mafunzo ikitolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo Ladislaus Mwamanga(hayupo pichani)
Baadhi ya Maafisa Ufuatiliaji wa TASAF –TMOs wakisikiliza hotuba ya ufunguzi wa Mafunzo ikitolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo Ladislaus Mwamanga (hayupo pichani)
Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Ladislaus Mwamanga (katikati walioketi) akiwa katika picha ya pamoja na wakurugenzi,meneja na Maafisa Ufuatiliaji wa TASAF baada ya kufungua mafunzo yao kwenye Ofisi za taasisi hiyo jijini Dar es salaam leo.

No comments:

Post a Comment