Tuesday, June 12, 2018

KILIMO CHA UMWAGILIAJI TATUZI MUAFAKA LA CHANGAMOTO ZA MABADILIKO YA TABIA NCHI.

Mwandishi Maalum - Dar es Salaam

Imeelezwa kuwa Kilimo kinachotumia teknolojia ya kisasa ya umwagiliaji ndiyo tatuzi muafaka la changamoto zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi katika sekta ya kilimo.

Hayo yameelezwa leo jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Uendelezaji wa Teknolojia ya Uwagiliaji Bwana. Anthon Nyarubamba, kutoka tume ya Taifa ya Umwagiliaji, alipokuwa akiongea na waandishi wa habari Ofisini kwake.

Bw. Nyarubamba Amesema kuwa, Kilimo hiki cha Umwagiliaji kinatumia teknolojia ya kisasa ya njia ya matone ya maji pamoja na kuvuna maji ya mvua katika mwabwawa maalum, yaliyojengwa katika maeneo ya mashamba ya umwagiliaji, maji ambayo yanatumika kwa kilimo katika kipindi chote cha mwaka bila kujali upatikanaji wa mvua za msimu.

Aidha Bw. Nyarubamba aliendelea kusema kuwa , uvunaji huu wa maji ya mvua unapelekea kuzuia mafuriko mengi yanayosabishwa na kubadilika kwa hali ya hewa kunakoharibu kwa kiasi kikubwa miundombinu mingine kama vile madaraja na barabara.

“Serikali iongeze Rasilimali za kutosha katika kilimo cha umwagiliji, ili kuweza kujenga mabwawa ya kutosha kupokea maji katika maeneo yenye skimu za umwagiliaji na kupunguza athari zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi, Alisisitiza.”

Akiongelea suala ya skimu za kilimo zinazotumia aina hiyo ya umwagiliaji wa maji ya mabwawa, Nyarubamba amesema kuwa skimu nyingi zilizopo katika kanda zote nane za Mbeya, Mtwara, Morogoro, Kilimanjaro, Dodoma, Tabora Katavi na Mwanza, zimefanikiwa kwa kiasi kikubwa na kuongeza Uzalishani, Ajira na Kipato kwa vijana wengi, hasa kutokana na ukulima wa vitunguu katika kanda ya Mbeya na Mpunga katika kanda ya Kilimanjaro.

“Huko nyuma, Vijana wengi walikuwa wakikimbilia mjini kutafuta ajira, lakini kwa sasa ajira ziko vijijini ndo maana vijana wanarudi mashambani kulima, labda kwa mfano kilimo cha vitungu peke yake katika kijiji cha Igomelo Mbalali Mkoani Mbeya. beya kinaweza kumpatia mtu takribani Milioni 30 - 40 kwa mwaka, sasa kwa nini kijana akimbilie mjini . Alisema.”

Kwa upande Mwingine, Bw. Nyarubamba amesema Tume ya Taifa ya umwagiliaji inakabiliana na changamoto mbali mbali zitokanazo na kilimo hiki ikiwa ni pamoja na kupata lawama ya matumizi mengi ya maji kutoka katika baadhi ya taasisi ili hali tume imekuwa ikifanya tafiti muhimu za awali kabla ya ujenzi wa miundombinu ya umwagiliji.

“Awali palikuwa na ujenzi wa baadhi ya miundombinu ya umwagiliaji iliyokuwa chini ya kiwango hali iliyopelekea kuanzishwa kwa tume ya Taifa ya Umwagiliaji na miongozo yake, tunaamini kwa sasa miundombinu hii ya umwagiliaji itakuwa ya kiwango kinachotakiwa kupitia kitengo cha udhibiti ubora wa miundombinu ya umwagiliaji.” Alisisitiza.
Sehemu Picha shamba la vitunguu lililopo katika eneo la skimu ya umwagiliaji la Mbalali Mkoani Mbeya.
sehemu ya Shamba la umwagiliaji lililopo katika skimu ya umwagiliaji ya Lemkuna Manyara.
Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Uendelezaji wa Teknolojia ya Uwagiliaji kutoka katika Tume ya taifa ya Umwagiliaji,Anthon Nyarubamba akifafanua jambo kuhusu kilimo cha umwagiliaji alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Jijini Dar es Salaam leo.

No comments:

Post a Comment