Sunday, June 3, 2018

KIJANA WA SAUDIA ASHINDA DOLA 5,000 TUZO YA KIMATAIFA YA KUHIFADHI QURAN

KIJANA wa miaka 18 kutoka Saudi Arabia, Ibn Rayizah Hatim Abdullah ameibuka na kitita cha dola za Marekani 5,000 kwenye fainali za 26 za tuzo ya Kimataifa ya Quran tukufu.

Kijana Rayizah ameibuka na kitita hicho baada ya kuwashinda wenzake sita waliofanikiwa kuingia fainali hizo ambao walitoka Yemen, Zanzibar, Malaysia, Mali, Marekani na Tanzania Bara.

Nafasi ya pili imechukuliwa na kijana Hamza Soukouna (25) kutoka Mali ambaye amejishindia dola za Marekani 4,000 na ya tatu imechukuliwa na Hamza El-Habashiy (18) kutoka Marekani ambaye amejishindia dola za Marekani 3,000. Mashindano hayo yaliyoandaliwa na Jumuiya ya Kuhifadhisha Quran Tanzania, mwaka huu yalishirikisha vijana 16 kutoka nchi 16 duniani.

Akizungumza na mamia ya waumini wa Kiislamu waliofurika kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee leo mchana (Jumapili, Juni 3, 2018), Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka viongozi wa dini hiyo waendelee kuwakamata vema vijana waliohifadhi Quran na kuwaendeleza kitaaluma katika fani nyingine za elimu ya kimazingira.

“Leo hii nimefarijika sana kusikia kwamba tunao vijana wetu ambao si tu wamehifadhi Quran bali pia wamehitimu fani mbalimbali katika elimu ya juu. Uwepo wa vijana wa namna hii ni muhimu katika kujenga jamii bora na yenye kuzingatia uadilifu katika kutekeleza majukumu yao,” amesema.

Amesema kazi ya kuhifadhisha Quran haiishii katika kujua kuisoma pekee. “Kuhifadhisha Quran kunapaswa kuwa msingi imara katika kujenga jamii bora kupitia mafunzo sahihi ya tabia njema, utii lakini pia kujua mipaka katika maisha yetu ya kila siku. Kwa kufanya hivyo, tutawasaidia vijana hawa tunaowahifadhisha Quran kuwa raia wema, wazalendo, wanaotambua  wajibu wao, majukumu yao, kwao wenyewe na kwa nchi yao pia,” amesema.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ametoa wito kwa wanaoendesha taasisi za kuhifadhi Quran wakae pamoja na watengeneze ratiba ya mashindano ya kitaifa na kimataifa ili waweze kuwa na mashindano yanayoanzia ngazi za chini hadi za juu.

“Kaeni pamoja, mtenge ratiba ya kuanzia ngazi ya kimataifa hadi kimataifa, ratiba hizi zipangwe na kutambulika kitaifa. Wekeni ratiba ili washiriki washindane kuanzia mikoani, ushindani uwepo na tuwaone wakipanda kutoka mkoa, Taifa, Afrika Mashariki, Afrika hadi ya Dunia,” amesema.

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na hadhira hiyo, Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir bin Ali alisema wameanza kuona matunda ya kazi ya kuhifadhisha Quran kwani vijana wa Kitanzania wamesoma elimu ya mazingira (circular education) na elimu ya dini na wamefaulu vizuri sana.

“Sasa hivi tunataka watoto wetu wafikie elimu ya juu ya dini na hii ya mazingira. Tunawapongeza hawa vijana wa Kitanzania ambao walienda hadi nje ya nchi kutafuta elimu ya juu na sasa wamerudi nyumbani kuasaidia ndugu zao,” alisema. 

Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kuhifadhisha Quran Tanzania, Sheikh Othman Ali Kaporo alisema jumuiya ilianza kazi zake kimyakimya mwaka 1984 lakini ilianza kujulikana mwaka 1992 

Alisema walianzisha jumuiya kwa sababu walibaini kuwa jamii ina kiu ya kupata watu wema watakaochangia maendeleo wa Taifa. “Ukiangalia mwelekeo wa vijana wetu wa Kiislamu si mzuri. Hebu fanya utafiti wa kina wa wale waliokuwemo magerezani. Je tunaumizwa na jambo hili? Na kama tunaumizwa tunafanya nini ili kuwaokoa vijana hawa? Haya ndiyo tunayalenga sisi, na kwa kupitia Quran, tuweze kuwaokoa na majanga yale,” alisema. 

“Kuna vijana wengi wana vipaji lakini vinakufa kwa sababu hakuna wa kuviendeleza vipaji vyao. Kupitia Quran tukufu, tunahitaji kuwabadilisha wote hawa ili tuwe na jamii imara, inayomjua Mwenyezi Mungu, iliyobora na inayoishi kwa amani,” alisema.


IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, JUNI 3, 2018.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubary Zubeir (kulia) na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kuhifadhisha Qur-aan Tanzania, Sheikh Othman Kaporo (watatu kulia) wakiwa na washindi wa Tuzo ya Kimataifa ya Kuhifadhi Qur-aan Tanzania baada ya Waziri Mkuu kuwakabidhi washindi hao zawadi zao kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es salaam, Juni 3, 2018. Kutoka kushoto ni mshindi wa kwanza Ibn Rayizah Hatim Abdullah wa Saudi Arabia, Mshindi wa pili Hamza Soukouna kutoka Mali na Mshindi wa tatu Hamzah El- Habashiy kutoka Marekani.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa na baadhi ya viongozi waliofika kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es salaam ambako Mheshimiwa Waziri Mkuu alikabidhi Tuzo ya Kimataifa ya Kuhifadhi Qur-aan Tukufu Tanzania, Juni 3,2018. Kutoka kushoto ni Katibu Mkuu wa CCM Mstaafu, Abdulrahman Kinana, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Hussein Mwinyi, Mwenyekiti wa Haj Trust Fund, Sheikh, Swaleh Misky, Makamu wa Rais Mstaafu, Dkt, Mohammed Bilal, Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakary Zubeir, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kuhifadhisha Qur-aan Tanzania, Sheikh Othman Kaporo na Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiteta na Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakary Zubeir kabla ya kukabidhi Tuzo ya Kimataifa ya Kuhifadhi Qur-aan Tukufu kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es salaam, Juni 3, 2018
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipokabidhi Tuzo ya Kimataifa ya Kuhifadhi Qur-aan Tukufu Tanzania kwenye ukumbi wa Dimond Jubilee jijini Dar es salaam, Juni 3, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipokabidhi Tuzo ya Kimataifa ya Kuhifadhi Qur-aan Tukufu Tanzania kwenye ukumbi wa Dimond Jubilee jijini Dar es salaam, Juni 3, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipokabidhi Tuzo ya Kimataifa ya Kuhifadhi Qur-aan Tukufu Tanzania kwenye ukumbi wa Dimond Jubilee jijini Dar es salaam, Juni 3, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakary Zubeir (wapili kushoto), Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kuhifadhisha Qur-aan Tanzania, Sheikh Othman Kaporo (kulia) na Sheikh wa Mkoa wa Dar es salaam, Alhadi Mussa Salum (wapili kulia) baada ya kukabidhi Tuzo ya Kimataifa ya Kuhifadhi Qur-aan Tukufu Tanzania kwenye  ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es salaam. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)


No comments:

Post a Comment