Wednesday, June 13, 2018

KAMISHNA MKUU WA TRA AWASHUKURU WAFANYABIASHARA JIJINI DODOMA

Na Veronica Kazimoto,Dodoma 

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Charles Kichere amewashukuru wafanyabiashara jijini Dodoma kwa mchango wao wa kulipa kodi na kuiwezesha Serikali kutekeleza wajibu wake wa kukuza uchumi na kutoa huduma mbalimbali za jamii hapa nchini. 

Akizungumza wakati akifuturisha wafanyabiashara na wafanyakazi wa TRA katika ukumbi wa LAPF jijini hapa, Kichere alisifia uhusiano mzuri uliopo kati ya wafanyabiashara hao na ofisi ya TRA Mkoa wa Dodoma. 

"Nachukua nafasi hii kuwashukuru wafanyabiashara wa Dodoma kwa kuwa walipakodi wazuri na kuonyesha ushirikiano wa hali ya juu na ofisi yetu ya TRA hapa mkoani Dodoma ambapo kutokana na uhusiano huu uliopo, tunapata urahisi wa kutekeleza jukumu letu la kukusanya mapato ya Serikali kwa manufaa ya watanzania wote," alisema Kichere. 

Kichere amewaahidi wafanyabiashara hao kuwa, TRA itaendelea kudumisha ushirikiano huo na kukaribisha mazungumzo ya pamoja na viongozi wa TRA mkoani hapa ili kufikia muafaka wa masuala mbalimbali yanayohusu kodi badala ya kulalamika mitaani bila kupata suluhisho. 

Aidha, Kamishna Mkuu Kichere amewahimiza wafanyabiashara hao kuendelea kulipa kodi mbalimbali kwa wakati kwani kodi hizo hutumika katika kujenga uchumi wa nchi na kutoa huduma mbalimbali za jamii ikiwa ni pamoja na huduma za afya, maji safi na salama, elimu, kulipa mishahara ya watumishi wa Umma, miundombinu ya barabara na umeme. 

"Nachukua fursa hii kutoa rai kwenu wafanyabiashara kuendelea kulipa kodi zote kwa wakati ikiwa ni pamoja na Kodi ya Majengo na Kodi ya Mapato awamu ya pili ambapo mwisho wa kulipa kodi hizi ni tarehe 30 Juni, mwaka huu. Kodi nyingine ni Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ambayo hulipwa tarehe 20 ya kila mwezi. Hivyo, uhiari wenu wa kulipa kodi hizi kwa wakati ndio chachu ya kujenga uchumi wetu na kuharakisha kutoa huduma za jamii kwa watanzania wote", alisema Kichere. 

Naye Katibu Mtendaji wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA) mkoani Dodoma ambaye pia ni Katibu wa Sekta Binafsi mkoani hapa Idd Senge amesema kwamba, sekta binafsi itaendelea kushirikiana na TRA kwa ajili ya kuhakikisha kuwa wafanyabiashara wanalipa kodi kwa wakati ili kuepuka faini ambazo zinarudisha nyuma maendeleo ya biashara zao. 

"Sisi kama wafanyabiashara wa hapa mkoani Dodoma tutaendelea kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania na pale patakapotokea sintofahamu yoyote tutafanya mawasiliano na viongozi wa TRA ili kupata muafaka wa pamoja," alieleza Senge. 

Mamlaka ya Mapato Tanzania imejiwekea utaratibu wa kufuturisha wafanyabiashara na wafanyakazi wake kila ifikapo Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa lengo la kumshukuru Mwenyezi Mungu katika shughuli mbalimbali wanazozifanya hususani za ukusanyaji mapato ya Serikali.



Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Charles Kichere akitoa hotuba fupi kwa Wafanyabiashara wa Jijini Dodoma wakati wa hafla fupi ya Iftar aliyowaandalia wafanyabiashara hao ikiwa ni sehemu ya kuwathamini walipakodi nchini.
Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Charles Kichere (aliyevaa miwani) akiwekewa futari wakati wa hafla fupi ya Iftar aliyowaandalia wafanyabiashara wa Jijini Dodoma ikiwa ni sehemu ya kuwathamini walipakodi nchini.
Baadhi ya Wafanyabiashara wa Jijini Dodoma wakichukua futari wakati wa hafla fupi ya Iftar iliyoandaliwa na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Charles Kichere kwa wafanyabiashara hao ikiwa ni sehemu ya kuwathamini walipakodi nchini.
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Charles Kichere (aliyevaa kofia kulia) akiwa na baadhi ya wafanyabiashara na watumishi wa TRA wakifuturu wakati wa hafla fupi ya Iftar iliyoandaliwa na Kamishna Mkuu huyo ikiwa ni sehemu ya kuwathamini walipakodi nchini.
Baadhi ya watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), wakiwa katika hafla fupi ya Iftar jijini Dododma aliyoiandaa Kamishna Mkuu wa Mamlaka hiyo Bw. Charles Kichere ikiwa ni sehemu ya kuwathamini walipakodi nchini.
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Charles Kichere (wa nne kulia) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wafanyabiashara na watoto yatima wa Kituo cha kulelea watoto yatima cha Rahman kilichopo jijini Dodoma wakati wa hafla fupi ya Iftar aliyowaandalia wafanyabiashara na watumishi wa TRA ikiwa ni sehemu ya kuwathamini walipakodi nchini. Hafla hiyo ilifanyika katika Ukumbi la LAPF jijini Dodoma.
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Charles Kichere (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wafanyabiashara na watumishi wa TRA mara baada ya hafla ya Iftar aliyowaandalia wafanyabiashara hao ikiwa ni sehemu ya kuwathamini walipakodi nchini. Hafla hiyo ilifanyika katika Ukumbi la LAPF jijini Dodoma. (PICHA ZOTE NA TRA)

No comments:

Post a Comment