Thursday, June 28, 2018

Jumia yaadhimisha miaka 6 ya mapinduzi ya biashara za mtandaoni Afrika

Takribani wateja 500,000 wanatembelea Jumia ndani ya mwezi katika mwaka huu 2018, kutoka wastani wa wateja 250,000 kwa mwezi mwaka 2017.Makampuni ya Kiafrika zaidi ya 60,000 na wafanyabiashara wamejiunga na Jumia. 

Ikiwa na dhamira ya kutengeneza mustakabali wa mazingira mazuri ya masoko na fursa za kuuza na kununua bidhaa pamoja na huduma za mtandaoni na kifedha, Jumia inaadhimisha miaka 6 ya mapinduzi ya huduma za manunuzi ya mtandaoni barani Afrika.

Ikiwa imeanzishwa mwaka 2012, Jumia inajivunia kufanya kazi na makampuni zaidi ya 60,000 ya Afrika pamoja na wafanyabiashara wa kiafrika kwenye mtandao wake.

Akizungumzia juu ya shamrashamra za maadhimisho haya yakatakayodumu kuanzia Julai 2 mpaka Julai 15 mwaka 2018, Mkurugenzi Mkuu wa Jumia Tanzania, Bw. Zadok Prescott amebainisha kuwa sherehe za mwaka huu zimekuja sambamba na sikukuu za Sabasaba hivyo kutoa fursa zaidi kwa wateja kununua bidhaa mbalimbali kwa gharama nafuu na ofa lukuki.

“Sabasaba ni maonyesho makubwa ya kibiashara siyo tu nchini Tanzania bali kwenye ukanda wa Afrika ya Mashariki kwa ujumla. Ni muhimu kwa wafanyabiashara na wateja ambapo hupata fursa ya kufanya maonyesho ya bidhaa na huduma tofauti, kuuza na kununua bidhaa mbalimbali. Kwa maneno mengine, Jumia ni kama maonyesho ya Sabasaba yanayofanyika kwa njiaya mtandao. 

Siku zote Jumia ina aina tofauti za bidhaa zinazopatikana kwa bei nafuu kabisa. Kwa hiyo sherehe za Jumia kwa mwaka huu itashiriki maonyesho ya Sabasaba, na kuwapatia wateja (watakaokuwepo Sabasaba na maeneo mengine) fursa ya kununua bidhaa kwa punguzo kubwa la bei, kujishindia zawadi, vocha za manunuzi na ofa kemkem kutoka mtandaoni na washirika wetu,” alisema Bw. Prescott.

Katika kunogesha sherehe hizi kwa mwaka 2018, Jumia imeshirikiana na wadau wake kama vile: Infinix, Samsung, Tecno, LG, Star X, TCL, Aborder, Philips, Fero, HP, Dell, Maybelline, Revlon and Nippotech. Washirika hawa watakuwepo kwenye viwanja vya maonyesho ya Kimataifa ya Biashara ya Sabasaba kwenye banda la Jumia ili kuwapatia wateja fursa ya kununua bidhaa kwa punguzo la bei, zawadi na elimu zaidi juu ya namna ya kufanya manunuzi mtandaoni. 

“Jumia inajivunia kuwa kinara katika mapinduzi ya biashara kwa njia ya mtandao barani Afrika, ikiwa ni sehemu pekee kabisa ya kuuza na kununua bidhaa halisi na zenye ubora wa hali ya juu. Japokuwa biashara ya mtandaoni haijashika kasi Tanzania, takribani wateja 500,000 hutembelea Jumia kwa mwezi. Idadi hii inaongezeka kila mwezi, mwaka jana idadi ya waliokuwa wanatembelea mtandao wetu walikuwa ni nusu ya idadi ya sasa!” aliongezea Mkuu Mkuu wa Jumia Tanzania.

Ikiwa imejitanua katika nchi takribani 13 barani Afrika, Jumia imechangia kwa kiasi kikubwa katika kuunga mkono uchumi wa nchi hizo kupitia biashara kwa njia ya kidigitali. Jumia imejizatiti katika kujenga mustakabali  katika nchi za Kiafrika kwa kufungua milango ya ajira - ikiwa na wafanyakazi takribani 3,000, kuendeleza na kukuza ujuzi kwa waafrika na katika sekta nzima kwa ujumla. 

“Ningependa kutoa wito kwa Watanzania kujumuika nasi katika maadhimisho ya miaka 6 ya Jumia kwa kufurahia punguzo la bei kwa bidhaa tofauti, zawadi na ofa hususani katika msimu huu wa Sabasaba.

 Tutakuwepo kwenye viwanja vya maonyesho na washirika wetu, wateja wataweza kufanya huduma za manunuzi, kujishindia zawadi na kufahamu chochote kuhusu masuala ya biashara za mtandaoni. Hii ni fursa kwa wafanyabiashara na wateja kututembelea ili kupata elimu zaidi,” alihitimisha Bw. Prescott. 

Naye kwa upande wake mwakilishi kutoka Atsoko, Bi. Lisa Kamecha ameongezea kuwa, “Tunayo furaha kuwa sehemu ya maadhimisho ya miaka 6 ya Jumia. Ni fursa kubwa kufanya kazi na kampuni ambayo imejizatiti kufanya mapinduzi ya biashara kwa njia ya mtandao nchini na Afrika kwa ujumla. Kwa Watanzania wengi bado dhana hii ni ngeni kwao lakini ina faida kubwa kama ikitumika ipasavyo.” 

“Biashara yetu imenufaika kwa kiasi kikubwa kuwa kwenye mtandao huu. Tumeweza kutanua soko letu kwa kuwafikia wateja wengi zaidi, hapo kabla tulikuwa tunategemea wateja kuja moja kwa moja dukani. Hakuna gharama za kujitangaza kupitia Jumia, ni rahisi wateja wetu kuperuzi bidhaa zetu, kuagiza, kufanya na kupelekewa popote walipo. 

Haya yote tusingeweza kama tungeamua kufanya wenyewe. Nawasihi wafanyabiashara wengine nchini kuitumia fursa kwa kujiunga kwani ndipo dunia ilipo sasa na inapoelekea siku za usoni,” alihitimisha Bi. Kamecha

  Mkuu wa Kitengo cha Masoko cha Jumia Tanzania, Bw. Albany James (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa maadhimisho ya miaka 6 ya Jumia barani Afrika na uzinduzi wa kampeni ya Sabasaba. Kulia ni wawakilishi kutoka kampuni ya simu ya FERO, ambao ni mojawapo ya washirika wa Jumia katika maonyesho ya Sabasaba mwaka 2018.
  Bw. Hemraj Bhardaraj, Meneja Ufundi wa kampuni ya simu ya FERO, akionesha mojawapo ya simu kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) zitakazopatikana kwenye viwanja vya maonesho ya Sabasaba katika banda  la Jumia. Wakifuatilia kwa umakini katikati ni muwakilishi mwenza kutoka FERO Javid Bapu huku kushoto ni  Mkuu wa Kitengo cha Masoko cha Jumia Tanzania, Bw. Albany James.
 Bw. Hemraj Bhardaraj, Meneja Ufundi wa kampuni ya simu ya FERO, akionEsha mojawapo ya simu kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) zitakazopatikana kwenye viwanja vya maonyesho ya Sabasaba katika banda  la Jumia. Wakifuatilia kwa umakini kutoka kulia ni  Meneja Mauzo wa kutoka FERO  Javid Bapu huku akifuatiwa na Mkuu wa Kitengo cha Masoko cha Jumia Tanzania, Bw. Albany James na Msimamizi wa Atsoko, Bi. Lisa Kameja.

No comments:

Post a Comment