Saturday, June 23, 2018

DK. KIGWANGALLA ATIMUA WAVAMIZI KWENYE PORI LA AKIBA SWAGASWAGA

Video
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akizungumza na wananchi wa kijiji cha Handa katika wilaya ya Chemba mkoani Dodoma jana, alipotembelea kijiji hicho kwa ajili ya kutatua mgogoro kati yake na Pori la Akiba Swagaswaga. 

Na Hamza Temba-WMU-Chemba, Dodoma

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla ametoa siku 30 kwa wananchi waliovamia Pori la Akiba Swagaswaga na kuendesha shughuli zao ikiwemo kilimo, makazi na ufugaji ndani ya pori hilo kinyume cha Sheria waondoke mara moja kwa hiari yao kabla ya kuondolewa kwa nguvu.

Ametoa agizo hilo jana kwenye mkutano wa hadhara katika kijiji cha Handa Wilaya ya Chemba mkoani Dodoma wakati wa ziara yake ya kikazi ya kutatua mgogoro wa ardhi kwenye hifadhi hiyo wilayani humo.

"Tunawapa siku 30 muanze kutoka wenyewe, baada ya siku 30 tunatoa notisi ya siku nyingine 30 za kutumia nguvu, kwahiyo kuanzia sasa hivi anzeni kujipanga wenyewe na kuondoka wakati Halmashauri ikifanya tathmini ya maeneo ya vijiji ambavyo ni halali ya kuwagawia kwa wale watakaopenda kupewa maeneo huko", alisisitiza Dk. Kigwangalla.

Alisema sheria za uhifadhi haziruhusu mtu yeyote kuingia ndani ya maeneo ya hifadhi na kuendesha shughuli za kibinadamu na kwamba kufanya hivyo ni kudharau Sheria na Malmlaka zilizopo.

Alisema kwa upande wa wananchi wa kijiji cha Handa ambacho kilianzishwa kimakosa ndani ya pori hilo wataendelea kubaki mpaka pale wizara yake kwa kushirikiana na Wizara ya Tamisemi na Ardhi zitakapoamua hatma yao ikiwemo ama kulipwa fidia kupisha eneo hilo au waendelee kubaki na mipaka ya hifadhi isogezwe.

Katika hatua nyingine, Dk. Kigwangalla ameiagiza Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania TAWA kujenga miundombinu ya kuvuta maji kutoka katika chemchem iliyopo ndani ya hifadhi hiyo na kuyasogeza kwenye makazi ya wananchi ili kulinda chanzo hicho kwa kuzuia uharibifu unaofanywa na wananchi wanaofuata huduma katika eneo hilo.

Mkuu wa Wilaya ya Chemba, Saimon Odunga alisema atasimamia ipasavyo maagizo yaliyotolewa na Dk. Kigwangalla na kwamba endapo wanavamizi hao walioingia ndani ya pori hilo kinyume cha sheria watakaidi agizo hilo atatoa notisi ya siku 30 na hatimaye kuwaondoa kwa nguvu ili kupisha eneo hilo liendelee kuhifadhiwa.

Kwa upande wake mbunge wa Chemba, Juma Nkamia alimshukuru Dk. Kigwangalla kwa kutembelea eneo hilo kwa ajili ya kutafuta suluhu ya mgogoro huo na kuwataka wananchi kutii sheria na kuepuka kuvamia maeneo yaliyohifadhiwa kisheria ili kuepuka usumbufu na mamlaka zinazosimamia eneo hilo.

Viongozi wengine walioongozana na Dk. Kigwangalla katika utatuzi wa mgogoro huo ni Mbunge wa Hanan'g, Dk. Marry Nagu, Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Mhandisi Jackson Masaka, na viongozi wengine wa Chama na Serikali wa wilaya za Chemba na Mkalama.

Kijiji cha Handa kilisajiliwa tarehe 16 Agosti, 2004 kikiwa na ukubwa kilomita za mraba 72.23 na vitongoji vitano, vinne kati yake vikiwa ndani ya Pori la Akiba Swagaswaga. Vitongoji hivyo ambavyo ni Ilala A, Ilala B, Mbugani na Mnang'ana vina ukubwa wa kilomita za mraba 7.85 na kaya 1,169 zenye watu zaidi  ya 5,291.

Pori la Akiba Swagaswaga lilianzishwa kwa Tangazo la Serikali namba 72 la tarehe 21 Februari, 1997 likiwa na ukubwa wa kilomita za mraba 871. Pori hilo lipo katika wilaya za Chemba na Kondoa mkoani Dodoma na wilaya ya Singida Vijijini mkoani Singida.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akizungumza na wananchi wa kijiji cha Handa katika wilaya ya Chemba mkoani Dodoma jana, alipotembelea kijiji hicho kwa ajili ya kutatua mgogoro kati yake na Pori la Akiba Swagaswaga.
Mkuu wa Wilaya ya Chemba, Saimon Odunga akizungumza katika mkutano huo.
Mbunge wa Chemba, Juma Nkamia akizungumza katika mkutano huo katika kijiji cha Handa wilaya ya Chemba mkoani Dodoma jana.
Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Handa katika wilaya ya Chemba mkoani Dodoma wakimsikiliza Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla alipotembelea kijiji hicho jana kwa ajili ya kutatua mgogoro kati yake na Pori la Akiba Swagaswaga. 
Mbunge wa Hanan'g, Dk. Marry Nagu akizungumza na wananchi katika mkutano huo.
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla na viongozi wengine wa wilaya ya Chemba na Mkalama wakikagua mpaka wa Pori la Akiba Swagaswaga ambalo lina mgogoro na kijiji cha Handa alipotembelea eneo hilo jana katika wilaya ya Chemba mkoani Dodoma kwa ajili ya kutatua mgogoro huo. 
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla, Mbunge wa Chemba, Juma Nkamia, Mbunge wa Hanang, Dk. Marry Nagu, Mkuu wa Wilaya ya Chemba, Saimon Odunga, Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Mhandisi Jackson Masaka, na viongozi wengine wa wilaya ya Chemba na Mkalama wakiangalia ramani ya mpaka Pori wa Pori la Akiba Swagaswaga alipotembelea eneo hilo jana kwa ajili kutatua mgogoro wa hifadhi na vijiji.
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla na viongozi wengine wa wilaya ya Chemba na Mkalama wakikagua mpaka wa Pori la Akiba Swagaswaga ambalo lina mgogoro na kijiji cha Handa alipotembelea eneo hilo jana katika wilaya ya Chemba mkoani Dodoma kwa ajili ya kutatua mgogoro huo. 
  Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Handa katika wilaya ya Chemba mkoani Dodoma wakimsikiliza Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla alipotembelea kijiji hicho jana kwa ajili ya kutatua mgogoro kati yake na Pori la Akiba Swagaswaga. 
 Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Handa katika wilaya ya Chemba mkoani Dodoma wakimsikiliza Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla alipotembelea kijiji hicho jana kwa ajili ya kutatua mgogoro kati yake na Pori la Akiba Swagaswaga.

No comments:

Post a Comment