Friday, June 1, 2018

BancABC yazindua tawi jipya Dodoma



Naibu WAZIRI WA Fedha, Mipango na Uchumi Dr. Ashatu Kijaji (wa pili kushoto), Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi Ajira na Vijana Anthony Mavunde (wa kwanza kushoto), Kaimu Mkurungenzi benki ya BANCABC Imani John (wa pili kulia) na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dr. Binilith Mahenge wakifungua pazia kuashiria uzinduzi rasmi wa Tawi jipya la Benki ya BANCABC Jijini Dodoma leo.


Naibu Waziri Fedha, Uchumi na Mipango Dr. Ashatu Kijaji (kushoto) akifungua akaunti katika Tawi jipya la Benki ya BANCABC Jijini Dodoma mara baada ya kulifungua rasmi jana, kulia ni Frida Mmmari wa huduma kwa wateja wa benki hiyo.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dr. Binilith Mahenge akiongea wakati wa ufunguzi wa tawi jipya la Benki ya BANCABC jjijini Dodoma jana. Kulia ni Naibu Waziri wa Fedha, Mipango na Uchumi Dr. Ashatu Kijaji na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi Ajira na Vijana Anthony Mavunde (kushoto).
Naibu WAZIRI WA Fedha, Mipango na Uchumi Dr. Ashatu Kijaji akisisitiza jambo wakati wa ufunguzi wa tawi jipya la Benki ya BANCABC jjijini Dodoma jana. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa BANCABC Imani John (kulia).
Naibu WAZIRI WA Fedha, Mipango na Uchumi Dr. Ashatu Kijaji (wa pili kulia) akikata utepe kuashiria ufunguzi wa tawi jipya la Benki ya BANCABC Jijini Dodoma jana. Wengine ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi Ajira na Vijana Anthony Mavunde (wa kwanza kushoto) na Kaimu Mkurungenzi benki ya BANCABC Imani John (wa pili kushoto) pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dr. Binilith Mahenge.




Benki ya BancABC imezindua tawi jipya jijini Dodoma kwa lengo la kukidhi mahitaji ya huduma za kibenki kwa wateja hivyo kusaidia ukuaji wa uchumi katika kanda ya kati. Hilo ni tawi la saba kwa BancABC nchini Tanzania.

Akizungumza wakati wa hafla ya kuzindua tawi hilo, mgeni rasmi Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt Ashatu Kijaji amesema ufunguzi wa tawi hilo umekuja wakati muafaka kwa kuwa ofisi za serikali zimehamia Dodoma na Dodoma imepandishwa hadhi na kuwa jiji hivyo mahitaji ya huduma za kibenki yameongezeka ili kuwawezesha wananchi kupata mitaji kwa ajili ya biashara na shughuli mbalimbali na pia kuhamasisha watanzania wengi kuendelea kujenga hulka ya kuweka amana.

“Napenda kuchukua fursa hii kuwapongeza BancABC kwa kuona umuhimu wa kuleta huduma za kibenki kwa kufungua tawi jipya jijini Dodoma. Ninaamini bado kuna watu wengi ambao hawajanufaika na huduma za kibenki na ni imani yangu kwamba mtafanya kazi kwa bidii ili kuwafikia wananchi na wafanyabiashara wengi mjini na vijijini katika ukanda huu”, alisema.

Dkt. Kijaji ameonyesha kufurahishwa na hatua ya benki hiyo ya kupunguza riba. “Hii itawavutia wafanyabiashara wengi hivyo kukuza biashara zao na kuwekeza katika miradi mbalimbali ikiwa ni pamoja na ujenzi wa majengo ya biashara na nyumba za kuishi. Upatikanaji wa mikopo kwa riba nafuu pia utasaidia kuboresha hali ya maisha ya wakazi wa mkoa wa Dodoma”, alisema

Ametoa wito kwa wakazi wa Dodoma na Watanzania kwa ujumla kujenga utamaduni wa kukopa katika benki ili kukuza biashara zao na kukamilisha kwa wakati miradi mbalimbali ya maendeleo. Naibu waziri huyo amewakumbusha wananchi kutumia mikopo kwa malengo kusudiwa na kurejesha kwa wakati ili kujiweka katika nafasi ya kuendelea kukopesheka.

Amezitaka taasisi nyingine za fedha kuangalia uwezekano wa kupunguza riba zao ili kuwafanya Watanzania wengi kuweza kukopa. Ni ukweli usipingika kwamba riba kubwa imekuwa ni kikwazo kikubwa kwa wakopaji.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa BancABC Tanzania Imani John amesema uzinduzi wa tawi hilo ni sehemu ya mpango mkakati wa benki hiyo wa kupeleka huduma za kibenki karibu zaidi na wakazi wa Dodoma na wananchi kwa ujumla na kuahidi kuendelea kufungua matawi zaidi nchini.

“Kwetu sisi leo ni siku ya kihistoria na hatua muhimu katika kutufanya kuwa taasisi kubwa siyo tu nchini Tanzania bali katika bara la Afrika na kusini mwa jangwa la Sahara. Vilevile tuna mpango wa kufungua huduma za mawakala katika robo ya nne ya mwaka ambao watawawezesha wateja wetu wengi kutufikia kirahisi na kupata huduma zilezile zinazotolewa na benki yetu”, alisema. 
 

“Vituo vya mikopo kwa wafanyakazi vitatoa huduma zaidi na tunazidi kuboresha huduma ya kibenki kwa kutumia simu ya kiganjani ili kuwawezesha wateja kupata huduma wakati wowote mahali popote”, alisema.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji huyo ametoa rai kwa wakazi wa jiji la Dodoma kuchangamkia huduma zinazotolewa na benki hiyo ili kufanikisha ndoto zao za miradi mbalimbali ya maendeleo.

No comments:

Post a Comment