Tuesday, May 22, 2018

TBF YATANGAZA TAREHE YA KUANZA MASHINDANO YA MPIRA WA KIKAPU

Na Zainab Nyamka, Globu ya jamii

SHIRIKISHO la Mpira Kikapu Tanzania(TBF) imetangaza rasmi tarehe ya mashindano ya kikapu ya FIBA Zone V U18 (Wanawake na Wanaume ) kuwa yanatarajiwa kuanza June 17 hadi 22 2018 hapa Jijini Dar Es Salaam, Tanzania. 

Rais wa TBF Pharess Magesa amesema matarajio yao ni kuwa mmoja kati viongozi wetu wakuu wa nchi ndyie atakuwa mgeni rasmi wa mashindano hayo na yatarushwa mubashara (live) siku zote za mashindano na vituo vyote vikubwa vya TV na Radio ambavyo wametuma maombi.

Magesa amesema gharama za maandalizi ya timu zetu mbili za Taifa  na gharama za kuandaa mashindano haya ni kubwa, na tayari kuna wadau wameshajitokeza kutoa ahadi na wengine wameshasaidia. 

"Hadi sasa hivi TBF ina upungufu wa takribani Sh.milioni 100, kati ya hizo Sh.milioni 60 ni za kuandaa mashindano na Sh.milioni 40 ni za kuweka timu zetu 2 za wanawake na wanaume kambini na kununua vifaa vya michezo zikiwemo Jersey za kucheza na za mazoezi, truck suits, viatu, socks, mipira na madawa,"amesema Magesa. 

"Pia, tuna mahitaji mengi ili kufanikisha matengenezo ya uwanja wa ndani wa Taifa (indoor) ukiacha kuvuja paa na kukatika kwa umeme ambako kutadhibitiwa na msaada ulitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda,"amesema.

Katika uwanja huu wa Taifa bado kunahitajika matengenezo ya mfumo wa taa na vifaa vya umeme, mabomba, vyoo na mfumo wa maji, mabenchi ya kukalia, mfumo wa kutoa na kuingiza hewa (ventilation), na rangi ya kupaka ndani na nje ili kuweka mazingira ya uwanja yawe ya kuvutia. 

Uwanja wa ndani wa Taifa utatumika kwa mashindano haya ya U18 June na pia baadae utatumika kwa mashindano ya kutafuta Klabu Bingwa wa Kikapu FIBA Zone V yanayotarajiwa kufanyika mwezi Septemba, 2018 hapa hapa Dar Es Salaam. 

Ameelezea, kuna gharama za usafiri, posho na malazi ya Kocha wa Kigeni ambaye anatoka Minneapolis, Marekani, Coach Matthew McCollister ambaye anatarajia atafika nchini walau majuma 2 kabla ya kuanza mashindano haya ili kuzinoa timu zetu 2 kwa kushirikiana na jopo la makocha Wazalendo wakiongozwa na Coach Bahati Mgunda. 

"Tunatarajia mashindano ya FIBA Zone V U18 yatakayofanyika mwezi ujao yatashirikisha timu za Taifa 24, za wanawake na wanaume, kutoka nchi 12 za Misri, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Ethiopia, Eritrea, Djibouti, Sudan, Somalia, Sudani Kusini na wenyeji Tanzania. Bingwa wa mashindano haya atapata nafasi ya kushiriki mashindano ya kutafuta bingwa wa Afrika (Afrobasket 2018) baadae mwaka huu,"amesema.

Rais TBF amesema wanatarajia kutakuwa na wageni takribani 400 kutoka nchi mbali mbali ikiwa ni pamoja na maofisa kutoka FIBA, waandishi na wadau kutoka nchi husika. 

Ametoa mwito kwa wapenzi wote wa michezo nchini, Serikali, taasisi za umma na binafsi, wafanyabiashara, wanasiasa, wafanyakazi na wananchi wote kwa ujumla kujitokeza na kushirikiana na TBF kufanikisha maandalizi mashindano haya ili ikiwezekana vikombe vyote vibaki nchini na kuzipatia nafasi timu zetu za Tanzania kushiriki Mashindano makubwa ya Kikapu ya FIBA Afrika. 

Ameomba tumuunge mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli kwa kila mtu kuwajibika katika eneo lake, kujenga Tanzania ya viwanda ili kusaidia ukuaji wa uchumi na hatimaye kuifanya nchi yetu kuwa na uchumi wa kipato cha kati haraka zaidi ya ilivyotarajiwa.

Ameongeza "Michezo ni moja ya viwanda vikubwa vinavyotengeneza ajira nyingi za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kama tutafanya uwekezaji sahihi. Mchezo wa kikapu ni mchezo pekee nchini unaopendwa na watu wengi wa rika na jinsia zote kwa usawa. Hivyo basi kusaidia mchezo huu utakuwa umefanya sehemu kubwa ya kusaidia jitihada za Serikali za kusaidia na kuendeleza vijana wetu na kuchangia katika maendeleo ya Taifa letu kwa ujumla,".

No comments:

Post a Comment