Sunday, May 27, 2018

DC KAKONKO APIGA MARUFUKU UNYWAJI POMBE ZA KIENYEJI ASUBUHI,ATOA MAAGIZO KWA POLISI

Na Rhoda Ezekiel Kigoma ,

MKUU wa Wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma Kanali Hosea Ndagala ameagiza kukamatwa watu wote wanajihusisha na unywaji wa pombe za kienyeji nyakati za kazi huku akifafanua ulevi kupita kiasi ni moja ya mambo yanayochangia kukwamisha maendeleo.

Amesema inasikitisha kuona baadhi ya wananchi kunywa asubuhi badala ya kwenda kwenye shughuli za kimaendeleo.

Hali hiyo ilimlazimu Kanali Ndagala kuagiza Ofisa wa Polisi kuwakamata watu wote waliokuwa wanakunywa pombe katika vilabu vya pombe ya kienyeji nyakati za asubuhi. Pia ametoa maagizo ya Mgambo wawili kunyang'anywa vitambulisho vyao katika Kijiji cha Muhange baada ya kuwashuhudia wakinywa pombe asubuhu.

Ametoa maagizo hayo jana alipokwenda kijijini hapo kwa ajili ya kukagua na kuunga mkono shughuli za maendeleo ikiwemo ujenzi wa shule ya Sekondari katika eneo hilo.Amesema anasikitishwa kuona watu wana shindwa kufanya shughuli za maendeleo na kuanza kunywa pombe asubuhi na wengi wao wakiwa ni vijana.

"Wakati wenzao wakijitolea katika ujenzi wa shule ya Sekondari ili kutatua changamoto ya wanafunzi wa kata hiyo kutembea umbali mrefu ili kufuata shule ilipo ambapo wananchi wameanza juhudi zao na serikali itaendelea kuunga mkono jitihada za wananchi,wao wanakwenda kwenye ulevi na hili hatuwezi kulivumilia," amesema.

Aidha Mkuu huyo amewataka wenyeviti wa vijiji vyote kuhakikisha vilabu vya pombe vyote vinafunguliwa kuanzia saa 10 jioni baada ya watu kumaliza kazi zao na wazingatie hilo na kuendelea kuwachukulia hatua za kinidhamu wale wote wanaokiuka sheria hiyo kwani ndio chanzo cha kuwa vibaka na kurudisha nyuma maendeleo ya wananchi na Serikali kwa ujumla.

" Ni aibu sana kuona vijana wadogo ambao mnanguvu za kufanya kazi kuja kunywa pombe asubuhi mnashindwa kufanya kazi.Ofisa wa Polisi hakikisha unawakamata hawa wote wanaokunywa na waliolewa muda wa kazi, sisi tunakuja kuhimiza maendeleo, wao wanaendelea katurudisha nyuma.

" Niwaombe wazazi mkae na watoto wenu muwafundishe na kuwaonya hatuko tayari kuona Wilaya yetu inaendelea kuwa masikini, lazima tuhakikishe watu wanafanya kazi na muda wa kunywa pombe ni jioni, nikiwakuta tena nitawachukulia hatua kali za kisheria," amesema Kanali Ndagala.

Wakati huo huo Kanali Ndagala ameshiriki katika ujenzi wa shule ya sekondali katika kata ya Muhange pamoja na shughuli mbalimbali za maendeleo, ambapo aliahidi kuongeza mifuko kumi ya saruji na kuwahakikishia kuwa Serikali itawapelekea fedha kwaajili ya ujenzi wa shule hiyo.Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Muhange Ibrahimu Katunzi amempongeza Mkuu huyo wa Wilaya kwa namna anavyojitahidi kuhimiza maendeleo katika Wilaya hiyo ambayo ilikuwa nyuma kwa kila kitu.

Ambapo amefafanua kwa sasa inaendelea vizuri na miradi mingi inakamilika ikiwa ni pamoja na wananchi kujitolea kwa uaminifu kwa kuamini Serikali ni sikivu.Amesema atahakikisha anahimiza wananchi kushiriki katika shughuli za maendeleo na kufanya kazi ili huduma muhimu zilizokosekana katika Kata hiyo wanafanya kwa ushirikiano kuhakikisha zinapatikana.

Nao baadhi ya wananchi akiwamo Wistoni Jolamu amesema changamoto waliokuwa nayo ni watoto kutembea umbali mrefu kwa miguu na ukizingatia maeneo mengi kuna mapori hali inayo sababisha usalama wa watoto wao kuwa hatarini na wamelazimika kujenga shule hiyo ilikutatua Changamoto hiyo.
 Baadhi ya Wananchi waliokamatwa kufuatia unywaji pome asubuhi badala ya kujishughulisha na shughuli za kimaendeleo.
  MKUU wa Wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma Kanali Hosea Ndagala akijionea mazingira halisi ya unywaji pombe asubuhi subuhi kwa baadhi ya wananchi kwenye moja ya vilabu vyao vya pombe
 MKUU wa Wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma Kanali Hosea Ndagala akizungumza na Wananchi huku akiagiza kukamatwa kwa  watu wote wanaojihusisha na unywaji wa pombe za kienyeji nyakati za kazi huku akifafanua ulevi kupita kiasi ni moja ya mambo yanayochangia kukwamisha maendeleo.
 MKUU wa Wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma Kanali Hosea Ndagala akishiriki ujenzi na kuunga mkono shughuli za maendeleo ikiwemo ujenzi wa shule ya Sekondari katika eneo hilo.Amesema anasikitishwa kuona watu wana shindwa kufanya shughuli za maendeleo na kuanza kunywa pombe asubuhi na wengi wao wakiwa ni vijana.

No comments:

Post a Comment