Sunday, May 20, 2018

CHUMBA CHA KUHIFADHIA MAITI KITUO CHA AFYA INYALA MKOANI MBEYA KUKAMILIKA MWEZI JULAI

Na Dotto Mwaibale, Mbeya

KITUO cha Afya cha Inyala, kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya Vijijini, mkoani Mbeya kipo katika hatua za mwisho za kukamilisha jengo litakalotumika kuhifadhia maiti ili kuondokana na changamoto ya kusafirisha maiti kwenda kuhifadhiwa Hospitali ya Rufaa ya mkoa.

Hayo yalibainishwa jana na Kaimu Mganga Mfawidhi wa Kituo hicho cha Afya cha Inyala, Alvin Mutiganzi wakati akipokea dawa za mgawo wa mwisho wa mwaka wa fedha wa 2017/2018 kutoka Bohari ya Dawa (MSD) Kanda ya Mbeya.

Mutiganzi alisema tayari majokofu ya kuhifadhia maiti hizo yaliyonunuliwa na MSD yalifika kituoni hapo mwezi Februari mwaka huu, na yana uwezo wa  kuhifadhi maiti sita kwa wakati mmoja.

Alisema, ujenzi huo unatarajia kukamilika mwezi Julai mwaka huu na kuanza kutoa huduma mara moja.Kukamilika kwa ujenzi wa jengo hilo kutasaidia kutoa huduma ya kuhifadhi maiti kutoka vijiji 50, vinavyopata huduma katika kata ya Inyala na maeneo mengine ya jirani.

"Kukamilika kwa ujenzi wa jengo la kuhifadhia maiti kwenye hiki kituo chetu cha afya kwetu ni jambo la faraja kwani hii ndio ilikuwa changamoto yetu kubwa ambapo kwa sasa tunalazimika kwenda kuhifadhi maiti Hospitali ya Mkoa na Ifisi ambapo gharama zake ni zaidi ya shilingi 60,000 kwa kwenda na kurudi kwa maiti moja.

Mutiganzi aliongeza kuwa kwa mwezi, kituo hicho kinaweza kupokea maiti watatu hadi wanne ambao hulazimika kuwasafirisha kwenda hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Mbeya na kwamba wagonjwa wanaofika kutibiwa ni 40.
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Kituo cha cha Afya cha Inyala, Alvin Mutiganzi (kushoto), akitoa maelekezo ya ujenzi wa jengo la kuhifadhia maiti kwa maofisa wa Bohari ya Dawa (MSD) na waandishi wa habari waliotembelea kituo hicho mkoani Mbeya jana. Kulia ni Msaidizi wa Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Victoria Minja na Ofisa Huduma kwa Wateja wa MSD Kanda ya Mbeya, Michaely Mwakuna.
Ofisa Huduma kwa Wateja wa MSD Kanda ya Mbeya, Michaely Mwakuna (kulia), akitoa maelezo ya jinsi ya ugawaji wa dawa na vifaa tiba za mgawo wa mwisho wa mwaka wa fedha wa 2017/2018. 
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Kituo hicho cha Afya cha Inyala, Alvin Mutiganzi, akikagua moja ya boksi la dawa baada ya kupokea. Kulia ni Mariam Pamboma mkazi wa Inyala ambaye alishuhudia makabidhiano hayo na kushoto ni Muuguzi wa kituo hicho cha Afya na wa pili kutoka kulia ni mjumbe wa kamati ya afya wa Kijiji cha Inyala, Jairos Emanuel.
Dawa zikikaguliwa. Katikati ni Ofisa Mauzo wa MSD Kanda ya Mbeya, Rhoda Joseph.


Maboksi yenye dawa kutoka MSD yakiwa yamepangwa kabla ya zoezi la ugawaji kuanza.
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Kituo hicho cha Afya cha Inyala, Alvin Mutiganzi, akitia saini kwenye fomu maalumu baada ya kukabidhiwa dawa.
Mjumbe wa Kamati ya Afya ya Kijiji cha Inyala, Jairos Emanuel akitia saini baada ya kushuhudia makabidhiano ya dawa.
Ofisa Huduma kwa Wateja wa MSD Kanda ya Mbeya, Michaely Mwakuna, akibandika fomu yenye orodha ya dawa zilizokabidhiwa katika ubao wa matangazo katika kituo hicho cha afya.

No comments:

Post a Comment