Friday, April 6, 2018

WAZIRI KIGWANGALLA AAGIZA KILA KIJIJI KUTENGA ENEO LA UHIFADHI WA MISITU, ATOA SIKU 7 KWA TFS KUWASILISHA MPANGO WA UVUNAJI

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga,Zainab Telack na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri wakipanda mti wa kumbukumbu wakati wa kilele cha kuadhimisha siku ya upandaji miti kitaifa iliyofanyika jana katika kijiji cha Mhunze wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga.

Na Hamza Temba, WMU, Kishapu, Shinyanga
.......................................................................................
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla amewaagiza Wakuu wa Mikoa nchini kuhakikisha Halmashauri zote nchini zinatenga maeneo katika kila kijiji kwa ajili ya uhifadhi wa misitu ikiwa ni pamoja na vijiji hivyo kuunda kanuni na taratibu zao wenyewe za kusimamia maeneo hayo. 

Ametoa agizo hilo jana katika kijiji cha Mhunze wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga wakati wa kuhitimisha kilele cha Maadhimisho ya Upandaji Miti Kitaifa yaliyofanyika mkoani humo kuanzia Aprili 03 mwaka huu.

Katika kufanikisha zoezi hilo ameuagiza uongozi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kuchagua mikoa 10 ya kuanza utekelezaji wa agizo hilo ikiwemo mikoa ya Shinyanga na Tabora ambayo inakabiliwa na changamoto kubwa ya uharibifu wa misitu.

Ameugiza pia we uongozi huo wa TFS kuweka mpango wa uhifadhi wa misitu ya asili katika maeneo hayo kwa kushirikiana na vijiji kupanga maeneo yanayostahili kuhifadhiwa sambamba na kuwapa elimu ya umuhimu wa uhifadhi wa maeneo hayo.

Wakati huo huo Dk. Kigwangalla ametoa siku saba kwa uongozi huo wa Wakala wa Huduma za Misitu kuwasilisha kwake mpango wa tathmini ya uvunaji wa mazao ya misitu wa nchi nzima kwa kuzingatia kiasi cha rasilimali misitu kilichopo na kiwango halisi kitakachotakiwa kuvunwa ambacho hakitazidi robo ya rasilimali iliyopo.

"Hatuwezi kuendelea tu kutoa vibali vya kuvuna misitu hatujui tunavuna wapi, tuna rasilimali kiasi gani, wavune kiasi gani, hapana, mnitengenezee mpango laa sivyo nitasitisha uvunaji, nikisema nasitisha uvunaji nitapeleka waraka kwa Wakuu wa Mikoa, na nina uhakika kwa nguvu walinayo hawashindwi kuzuia uvunaji. 

"Kwahiyo TFS nawapa siku saba mniletee mpango wa tathmini ya namna ambavyo tuna rasilimali kwenye kila mkoa, tujue mkoa flani una miti cubic mita kadhaa ya mbao kadhaa, ya kuni kadhaa, ya mkaa kadhaa na kwa mwaka huu tutaruhusu wavune kwenye msitu fulani  kiasi kadhaa, twende kisayansi, sio Meneja wa TFS anakaa Wilayani anatoa vibali watu wanaenda kuvuna,".

Dk. Kigwangalla amesema  takwimu za uharibifu wa misitu hapa nchini zinatisha jambo ambalo likiachwa liendelee bila kuchukua hatua nchi itageuka kuwa jangwa.

"Kwa mwaka tunakata miti kwa mahitaji mbalimbali kati ya ekari 800,000 na 1,200,000.
Ili kurejesha walau nusu ya miti tunayokata kwa mwaka tunahitaji kupanda miti 3,000,000 kwa mwaka mfululizo kwa miaka 17 ili kufidia kiasi cha uharibifu tunachofanya kwa nusu mwaka" alisema Dk. Kigwangalla.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk. Ezekiel Mwakalukwa ambaye alimuwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo alisema kumekuwepo na jitihada za kuandaa programu kubwa za kitaifa za uhifadhi wa mazingira katika maeneo mahususi yaliyoonekana kuzidiwa na tatizo la uharibifu wa mazingira. 

Alitaja Programu hizo kuwa ni Hifadhi Ardhi Dodoma (HADO), Hifadhi Ardhi Shinyanga (HASHI), na Hifadhi Mazingira Iringa (HIMA).

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack alisema mkoa wake kwa kushirikiana na uongozi wa mkoa wa Tabora umeanza kuchukua hatua za kurejesha uoto wa asili katika maeneo yao ikiwemo kuanzisha utaratibu wa kugawa miche ya miti kwa kila kaya pamoja na kuimarisha kamati za uhifadhi wa mazingira.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Taboba, Aggrey Mwanri alisema ushirikiano huo ni muhimu kwani utawezesha kukabiliana na changamoto zilizopo katika mikoa hiyo kwa kuweka mikakati ya pamoja wa kudhibiti vitendo vya uharibifu wa mazingira kwa kuzingatia sheria, taratibu na miongozo iliyopo.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga,Zainab Telack na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri wakipanda mti wa kumbukumbu wakati wa kilele cha kuadhimisha siku ya upandaji miti kitaifa iliyofanyika jana katika kijiji cha Mhunze wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiwahutubia wananchi wakati wa kuhitimisha kilele cha Maadhimisho ya Upandaji Miti Kitaifa yaliyofanyika kijiji cha Mhunze wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga jana.
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga,Zainab Telack na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri wakiteta jambo wakati wa kilele cha kuadhimisha siku ya upandaji miti kitaifa iliyofanyika jana katika kijiji cha Mhunze wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga.
 Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga,Zainab Telack akiwahutubia wananchi wakati wa maadhimisho hayo.
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga,Zainab Telack na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri wakiwasalimu wananchi wakati wa kilele cha kuadhimisha siku ya upandaji miti kitaifa iliyofanyika jana katika kijiji cha Mhunze wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga.
  Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk. Ezekiel Mwakalukwa ambaye alimuwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo akitoa maelezo kuhusu maadhimisho hayo.
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri wakielekea eneo la tukio la kupanda miti wakati wa kilele cha kuadhimisha siku ya upandaji miti kitaifa iliyofanyika jana katika kijiji cha Mhunze wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akishiriki kucheza ngoma wakati wa maadhimisho hayo.

No comments:

Post a Comment