Saturday, April 7, 2018

TAARIFA KWA UMMA KUHUSU UFAFANUZI WA TAKWIMU ZA VIFO VITOKANAVYO NA UZAZI NCHINI


JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA WAZEE NA WATOTO


TAARIFA KWA UMMA KUHUSU UFAFANUZI WA TAKWIMU ZA VIFO VITOKANAVYO NA UZAZI NCHINI

Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inapenda kutoa ufafanuzi wa takwimu za vifo vitokanavyo na uzazi nchini. Ufafanuzi huu unatokana na taarifa iliyorushwa na kituo cha Televisioni cha ITV katika moja ya taarifa zake za habari siku ya tarehe 29 Machi 2018 na baadaye kuanza kuzunguka katika mitandao ya kijamii inayosema “Shirika la Kimataifa la Idadi ya Watu-UNFPA limesema idadi ya vifo vya mama na mtoto vinavyotokana na uzazi hapa nchini imeongezeka hadi kufikia vifo 556 kwa kila vizazi hai elfu moja (1000) kutokana na changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya afya ikiwamo uhaba wa wauguzi na wakunga”.

Nikiwa Waziri mwenye dhamana ya Afya, napenda kuufahamisha umma kuwa taarifa hizo sio sahihi.  Na ukweli wake ni kuwa takwimu za tathimini iliyofanywa na Taasisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) mwaka 2015/2016 (Ikiwa ni miaka miwili na nusu iliyopita) ya Hali ya Afya za Watu Tanzania (TDHS - MIS) ni kuwa vifo vya akinamama vitokanavyo na uzazi ni 556 kwa kila vizazi hai 100,000 (laki moja) na si vifo 556 kwa kila vizazi hai 1,000 (efu moja). Aidha nasisitiza kuwa Takwimu hizi ni za miaka miwili na nusu iliyopita.

Ni muhimu ikafahamika kuwa Serikali ya awamu ya Tano tangu imeingia madarakani Novemba 2015, imewekeza sana katika sekta ya afya hususani katika eneo la afya ya mama na mtoto. Tuna imani kuwa endapo itafanywa Tathmini kama hii iliyofanywa na kusimamiwa na Taasisi ya Taifa ya Takwimu  (NBS) hakuna shaka kuwa itatuonesha hatua kubwa tuliyopiga katika kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi.
Serikali kwa kushirikiana na wadau wetu wa maendeleo tumechukuwa hatua mbalimbali zenye lengo la kupunguza vifo vitokanavyo na uzaziMikakati ambayo serikali ya Awamu ya Tano kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya Afya imewekeza na kuitekeleza  ili kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi ni pamoja na:-
1.    Kuandaa na kuanza utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Miaka 5 wa mwaka 2016 hadi 2020 unaolenga kuboresha afya ya uzazi, watoto na vijana pamoja na kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kufikia 292 kwa kila vizazi hai 100,000 ifikapo mwaka 2020. Mpango huu umezingatia maeneo makuu matatu: ambayo ni: huduma ya uzazi wa mpango, huduma wakati wa ujauzito na huduma wakati wa kujifungua. Utekelezaji wa mpango huu unaelekeza Sekta ya Afya katika kujikita kwenye afua muhimu za kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi.

2.    Kuongeza uwajibikaji kwa ngazi zote ili kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kwa kutaka kila kifo cha mama na mtoto kinachotokana na matatizo ya uzazi kitolewe taarifa ndani ya saa 24 katika kituo cha huduma au ngazi ya Jamii kifo kilipotokea na baadaye kujadiliwa kwa lengo la kubaini chimbuko la kifo hicho na kuchukua hatua stahiki hasa kwa kutatua changamoto zinazojitokeza. Hatua hii imeanza kutekelezwa toka Octoba 2016 na imekuwa chachu katika kuboresha huduma kwa akina mama wajawazito nchini.

3.    Wizara kwa kushirikiana na OR – TAMISEMI na wadau mbalimbali, inaendelea na kazi ya kukarabati Vituo vya Afya (Health Centres)  zaidi ya 220 katika Halmashauri mbalimbali nchini kwa kujenga na kukarabati majengo ya upasuaji (Theatre),  Wodi za Wazazi na Watoto,  Maabara ya damu na nyumba za watumishi ili kusogeza karibu na wananchi huduma za uzazi za dharura ikiwemo upasuaji wa kumtoa mtoto tumboni. Hadi Desemba 2015, ni Vituo vya Afya vya Serikali  (Health Centres) 117 tu (sawa na asilimia 21) kati ya vituo vya Afya vya 473 vinavyoweza kutoa huduma ya upasuaji wa dharura kwa wajawazito. Hakuna shaka kuwa jitihada hizi za Serikali ya Awamu ya Tano za kupanua huduma za upasuaji wa dharura zitaokoa maisha ya kinamama wajawazito na vichanga vyao.

4.    Huduma za Rufaa kwa wajawazito zimeendelea kuboreshwa ambapo Serikali imegawa magari ya kubebea wagonjwa (Ambulance) zaidi ya 100 katika kuimarisha juhudi za kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi katika mikoa ambayo takwimu zimeonesha kuwa ina vifo vingi zaidi vitokanavyo na uzazi.

5.    Serikali imeimarisha upatikanaji wa dawa zote muhimu zikiwemo dawa za uzazi salama kama oxytocin (inayozuia kupoteza damu wakati wa kujifungua) na dawa ya sindano ya magnesium sulphate (inayokinga na kutibu kifafa cha mimba). Aidha bajeti ya dawa imeongezeka kutoka shilingi bilioni 31 mwaka 2015 hadi bilioni 268 mwaka 2018/19 na upatikanaji wa dawa muhimu kwa ujumla hapa nchini upo juu kwa zaidi ya asilimia 85 kwenye vituo vyote vya kutolea huduma za afya hususani ngazi ya msingi ambako ndiko akina mama waliowengi wanajifungulia.

6.    Serikali imetoa kibali cha kuajiri watumishi wa afya zaidi ya 3500 ambao wamepelekwa kwenye mikoa na Halmashauri zenye changamoto kubwa ya upungufu wa watumishi.

7.    Serikali imeendelea kuboresha utoaji wa huduma katika vituo vya kutolea huduma za afya vinavyomilikiwa na Serikali. Tathmini ya awali ya kuhakiki Ubora wa Vituo vya Kutolea Huduma za Afya (Star Rating) iliyofanywa mwaka 2016 na Wizara ya Afya kwa vituo vya kutolea huduma za afya msingi 2,724 (Zahanati, Vituo vya Afya na Hospitali katika Halmashauri) zote katika Mikoa ya  Dar es salaam, Geita, Katavi, Singida, Mwanza, Pwani, Kigoma, Iringa, Kagera na Tanga ilionyesha kuwa jumla ya vituo 857 (31%) vilipata nyota sifuri (0) ukilinganisha  na Tathmini ya mara ya pili iliyofanywa mwaka 2017 ambapo ni vituo 138 tu (asilimia 4.87%) vilivyopata nyota sifuri. Aidha vituo 55 (3%) vilipata nyota 3 na zaidi  mwaka 2016 kulinganisha na tathmini ya mara ya pili ya mwaka 2017 ambapo vituo 612 (22.46%) vimepata nyota tatu na zaidi. Hii inaonyesha kuimarika kwa ubora wa huduma za afya ngazi ya msingi ambako ndiko akina mama waliowengi wanajifungulia.

8.    Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo wanaochangia Mfuko wa Pamoja wa Afya (Health Sector Basket Fund) imefungua akaunti kwenye vituo vya kutolea huduma za afya ikiwemo Zahanati na Vituo vya Afya na kuanzia Desemba 2017 imeanza kupeleka fedha moja kwa moja kwenye akaunti za vituo hivi badala ya kuzipeleke kwenye Halmashauri zao. Hatua hii imechangia kuboresha upatikanaji wa fedha kwa wakati katika ngazi zote za kutolea huduma na kusaidia Vituo kupanga mikakati ya utoaji wa huduma bora za afya kwa wananchi kwa kutatua changamoto zilizoko na hivyo kuleta ufanisi mkubwa. Pia tunazijengea uwezo kamati za usimamizi za vituo katika kuimarisha uwajibikaji na kuboresha huduma katika vituo husika.

9.    Aidha Serikali kwa kushirikiana na Wadau wa Maendeleo imeanzisha Mpango wa Malipo kwa Ufanisi (Result Based Financing-RBF) kwenye mikoa 8 ambayo ina kiwango kikubwa cha vifo vya kinamama wajawazito na watoto ambayo  ni Kigoma, Geita, Kagera, Shinyanga,  Mwanza, Tabora, Simiyu na Pwani. Matokeo ya utekelezaji wa mpango huu yanaonyesha kuongezeka kwa morale ya watumishi wetu wa afya  na kuimarika kwa ubora wa huduma za afya kwa wananchi hasa wanawake wajawazito na watoto.

Hitimisho
Suala ya kuboresha afya ya mama na mtoto ni mojawapo ya vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya 5 inayoongozwa na Mhe Rais Dr. John Pombe Magufuli. Ninaomba watanzania wenzangu tuendelee kushirikiana kwa pamoja katika kuboresha afya ya mama na watoto. Ni jukumu letu sote kuhakikisha kuwa hakuna mwanamke mjamzito atakayepoteza maisha kutokana na uzazi. Wizara itaendelea kusimamia utekelezaji wa mikakati mbalimbali tuliyoweka ikiwemo kufuatilia kila kifo cha mama mjamzito kinapotokea ili kutatua changamoto zinazojitokeza. Changamoto nyingi ambazo tumebaini zinapelekea vifo vya kina mama hutokana na ama kuchelewa nyumbani kwa mama na familia katika kufanya maamuzi ya kwenda kwenye Kituo cha kutolea huduma, au kukosa usafiri stahiki wa kwenda kituoni.
Kwa pamoja tunaweza kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi.


Imetolewa na


Ummy A. Mwalimu (Mb)
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto
6 Aprili, 2018



No comments:

Post a Comment