Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe Hamad Rashid leo amezindua ugawaji endelevu wa vyandarua vyenye dawa ya muda mrefu kwa jamii hapa Zanzibar.
‘Leo kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, tunayo furaha kubwa kutangaza ugawaji wa vyandarua vyenye dawa ya muda mrefu kwa kila mama mjamzito ambaye ataudhuria kliniki kwa mara ya kwanza na watoto wanaopata chanjo ya surua. Vile vile kila Mzanzibari ataweza kupokea chandarua kutoka kituo cha afya kwa kutumia koponi ambayo ataipata kutoka kwa mjumbe wa sheha,’ alisema Hamad Rashid.
Kampeni Endelevu ya ugawaji vyandarua vyenye dawa ya muda mrefu una lengo la kufanya upatikanaji kwa rahisi vyandarua kupitia vituo vya afya. Ugawaji endelevu wa vyandarua ni mradi unaoendeshwa kwa pamoja na shirika la Johns Hopkins Center for Communication kupitia mradi wa VectorWorks kwa ufadhili wa Shirika la Misaada la Marekani – USAID .
,
kupitia Mfuko wa Raisi wa Marekani wa kudhibiti malaria na kuratibiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Kitengo cha kumaliza Malaria Zanzibar - ZAMEP . ‘Serikali inatoa shukrani kwa washirika wa Maendeleo ya afya, Watu wa Marekani, Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya WHO, Global Fund na wengine wote, aliongeza Mh Rashid.
‘Zanzibar imedhamiria kumaliza ugonjwa wa malaria kwa kusambaza vyandarua vyenye dawa ya muda mrefu jambo ambalo litafanya upatikanaji wake kuwa rahisi. Upatikanaji kwa urahisi wa vyandarua ni hatua moja muhimu kwenye kupambana na ugonjwa wa malaria’, alisema Mhe Rashid akiongeza kuwa kupitia mradi huu unaozinduliwa leo, kila mama mjamzito na watoto wenye umri wa mwaka mmoja watapata vyandarua bila Malipo yoyote. Vile vile alitoa wito kwa kila Mzanzibari kubadailisha chandarua chake cha zamani kwa kupata kopuni kutoka kwa Shehia kisha kutembelea kituo chochote cha Afya kupata chandarua.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Miradi kutoka VectorWorks Waziri Nyoni alisema ‘Tunayo furaha kufanya kazi pamoja na Kitengo cha kumaliza Malaria Zanzibar - ZAMEP kuendesha programu hii yenye lengo la kumaliza malaria Zanzibar. Ugawaji wa vyandarua vyenye dawa ya muda mrefu pamoja na koponi unaendeshwa na kitengo cha Serikali cha kusambaza vifaa tiba pamoja, Zanzibar Central Medical Store (CMS).
Kupitia mfumo huo, vyandarua na koponi zitakuwa zikipelekwa kwenye vituo vya afya na CMS, huku Mfumo wa Taarifa ukihusisha vitengo vingine vya afya kupitia HMIS, alisema Nyoni. Nyoni aliongeza kuwa VectorWorks pamoja na ZAMEP, HMIS, CMS wameandaa utaratibu ambao unahakikisha kila chandarua na kuponi inahesabiwa.
Leo tunasherekea hatua nyingine muhimu kwenye historia ya kumaliza malaria Zanzibar kwa kuzindua ugawaji endelevu wa vyandarua vyenye dawa ya muda mrefu kwa kila mama mjamzito na mtoto wenye umri wa mwaka mmoja wa kupata bure chandarua pamoja na kila Mzanzibari. Vyandarua hivi vitawapa usingizi mzuri lakini pia muhimu ni kinga dhidi ya malaria, aliongeza Nyoni.
Haya ni mafanikio makubwa kwa Zanzibar, alisema Mhe Rashid. ‘Tumepiga hatua kubwa dhidi ya mapambano na malaria kwa miaka mitano iliyopita. Tumeweza kupunguza ugonjwa wa malaria kuwa chini ya Asilimia moja. Lengo letu kama serikali kuendeleza juhudi hizi, na kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na washiriki wetu kwenye Maendeleo ya afya, malaria inaweza kuwa sio tishio kabisa kwa Zanzibar’, alisema Mhe Rashid.
Ugawaji wa vyandarua vyenye dawa ya muda unaongozwa na Wizara ya Afya Zanzibar kupitia Central Medical Stores, Kitengo cha kumaliza malaria Zanzibar (ZAMEP), Sekta ya afya ya uzazi na kitengo cha usimamizi wa taarifa. Kampeini imefadhiliwa na Shirika la Misaada la Marekani – USAID kupitia Mfuko wa Raisi wa Marekani wa kudhibiti malaria. Uratibu wa kitaalam wa programu hii unafanywa na mradi wa VectorWorks.
VectorWorks ni mradi wa miaka mitano (2014-2019) wenye lengo kuongeza upatikanaji wa vyandarua vyenye dawa ya muda mrefu na vidhiti vingine vya malaria. VectorWorks inaongwa na Johns Hopkins Center for Communication Programs –CCP. Washirika wa mradi ni pamoja na PSI Tanzania, Tropical Health na chuo kikuu cha Tulane.
Waziri wa Afya wa Zanzibar Hamad Rashid akiongea na waandishi wa habari jana Zanzibar baada ya kuzindua ugawaji endelevu wa vyandarua vyenye dawa ya muda mrefu ikiwa ni juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuendelea kupambana na ugonjwa wa Malaria chini ya ufadhili wa Shirika la Misaada la Marekani – USAID kupitia Mfuko wa Raisi wa Marekani wa kudhibiti malaria.
Waziri wa Afya wa Zanzibar Hamad Rashid akiongea na waandishi wa habari jana Zanzibar baada ya kuzindua ugawaji endelevu wa vyandarua vyenye dawa ya muda mrefu ikiwa ni juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuendelea kupambana na ugonjwa wa Malaria chini ya ufadhili wa Shirika la Misaada la Marekani – USAID kupitia Mfuko wa Raisi wa Marekani wa kudhibiti malaria.
Naibu Meneja wa Kitengo cha Kupambana na Malaria Zanzibar Faiza Bwanaheri akiongea na waandishi wa habari leo Zanzibar baada ya kuzindua ugawaji endelevu wa vyandarua vyenye dawa ya muda mrefu ikiwa ni juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuendelea kupambana na ugonjwa wa Malaria chini ya ufadhili wa Shirika la Misaada la Marekani – USAID kupitia Mfuko wa Raisi wa Marekani wa kudhibiti malaria. Kushoto ni Mkurugenzi wa Miradi kutoka VectorWorks Waziri Nyoni.
No comments:
Post a Comment