Tuesday, April 3, 2018

PWANI KUJENGA VIWANDA VITATU VYA MADAWA NA BAADHI YA VIFAA TIBA

Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha

SERIKALI mkoani Pwani, imeitikia wito wa serikali ya awamu ya tano ya kujenga viwanda vya madawa na baadhi ya vifaa tiba ambapo inatarajia kuwa na viwanda hivyo vitatu hali itakayoondoa adha ya kuagiza madawa nje ya nchi .

Aidha imekemea tabia inayofanywa na baadhi ya wawekezaji ya kutoa ajira kwa watu kutoka nje ya nchi na kuwabania fursa hiyo wanaPwani ama watanzania.

Akielezea masuala ya uwekezaji na ajira ,wakati wa ziara yake ya kutembelea viwanda mjini Kibaha ,mkuu wa Mkoa wa Pwani,mhandisi Evarist Ndikilo alisema Viwanda vya madawa vitawezesha kuokoa mamilioni ya fedha yaliyokuwa yakitumika kununulia madawa nchi jirani na nje.

Alieleza viwanda vitatu vinajengwa Mkoani Pwani ikiwemo Kairuki Pharmaceuticals industry Ltd ,Zinga pharmaceuticals ambacho kitajengwa kwa ubia na waislael na kipo mbioni kuanza kujengwa na Bahari pharmaceuticals .

"Tunaikitia wito wa rais Dk.John Magufuli ,lakini pia tangu kipindi cha nyuma tumejipanga kujenga viwanda hivyo ,kupitia ziara hii tunawathibitishia wananchi tunaunga  mkono kauli ya serikali yetu"alifafanua Ndikilo.

Pamoja na hayo ,mkuu huyo wa mkoa alieleza ,zipo fursa mbalimbali  za uwekezaji  lakini vijana na wazawa wanashindwa kukimbilia fursa hizo.

Ndikilo alisema wazazi na vijana bado hawajatambua kujipanga kukuza elimu na ujuzi wao kwa ajili ya kujipatia ajira kirahisi.

Alitoa rai kwa wawekezaji ,kuacha kuwanyima ajira wazawa na watanzania ambao wanaujuzi na sifa za kufanya kazi .

" Haiwezekani tunajenga viwanda vingi lakini vijana ,waTanzania na wanaPwani hawanufaiki na ajira zinazopatikana,haikubaliki"alisisitiza Ndikilo.

"Sidhani kama Pwani ama Tanzania nzima haina wenye sifa na ujuzi,hivyo aliwataka wawekezaji hao watoe kipaombele kwa watanzania wenye uwezo .

Ndikilo alisema amepokea taarifa uwekezaji wa standard gauge eneo la Soga hawatoi ajira hata ya udereva jambo ambalo analichunguza na atakapopata uhakika watachukua hatua zinazostahili.

Aliwataka kununua vifaa vya ujenzi kama nondo ndani ya nchi ,kwani taarifa waliyompatia kwenye ujenzi wa Kairuki Pharmaceuticals industry Ltd kuwa wananunua nondo huko Uturuki .

Alisema kipo kiwanda cha Kiluwa ambacho kinatengeneza nondo zenye ubora hivyo wanunue katika viwanda vya ndani ya nchi.

Nae mkurugenzi  mtaalamu wa Kairuki Pharmaceuticals eng.Valency Assenga alisema ujenzi wa mradi huo ulianza machi 10 mwaka huu na mkandarasi ni Petra Construction Ltd Ltd na unatarajiwa kumalizika Novemba 2018.

Alielezea kazi zote zinaendelea kwani zipo hatua ya awali ya ujenzi na mpaka kukamilika ujenzi wa awamu ya kwanza kiwanda hicho kitagharimu bilioni 3.9 " #

Eng .Assenga alitaja changamoto kuwa ni miundombinu ya barabara,mradi kusuasua kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha na ucheleweshwaji wa uunganishwaji wa umeme.

Mkurugenzi wa halmashauri ya Mji huo ,Jennifer Omolo akizungumzia suala la mipango miji alisema wameanza zoezi la kupima mji muda mrefu  na wanaendelea na zoezi hilo .

Omolo aliwataka watu waache kujenga na kufanya biashara kiholela bila kupangwa ,na kuwashauri waone watalaamu wa mipango miji ofisi ya mkurugenzi ili  kupewa maelekezo ya kupata vibali .

No comments:

Post a Comment