Na Ripota Wetu,Globu ya jamii
WASANII wa muziki wa kizazi kipya a.k.a Bongo Fleva Nassib Abdul ' Diamond' na Faustina Charles 'Nandy' kila mmoja ameonekana kujutia kitendo cha kusambaza picha chafu mtandaoni ambazo ni kinyume na maadili ya Mtanzania huku akiwaomba vijana kutoitumia mitandao vibaya.
Diamond na Nandy kila mmoja kwa wakati wake walisambaza picha chafu mtandaoni hali iliyosababisha Serikali kushindwa kuvumilia na hivyo Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam liliamua kuwakamata na kisha kuwahoji kabla ya leo kuzungumza na waandishi wa habari wakiwa Mamakala ya Mawasiliano Tanzania(TCRA).
Kwa upande wa Diamond amesema anajua kitendo cha kusambaza video ambayo imekwaza wengi na kwamba tukio hilo sasa limemfundisha kuwa anatakiwa kuwa mtumiaji mzuri wa mtandao na si kuweka picha ambazo hazina maadili ya kitanzania na kuomba vijana wengine kuacha tabia ya aina hiyo.
"Nikiri binafsi ninao mashabiki wengi mtandaoni ambao wanafuatilia kila ninachokifanya na wakati mwingine wanaiga kutoka kwangu.Niwaombe waitumie mitandao ya kijamii vizuri kwani unaweza kufanya jambo kwenye mtandao ukadhani upo kama chumbani kumbe ni tofauti.Mtandao hakuna tofauti na kufanya jambo barabarani kwani kila mtu ataona.
"Kosa la kusambaza picha chafu mtandaoni limenifanya nijifunze mambo mengi tu na TCRA wametueleza madhara yake na kubwa zaidi sheria na kanuni ambazo ni mpya zinazoweza kumbana anayetumia mtandao vibaya,"amesema Diamond.
Amefafanua yeye na wasanii wengine wangi wanayo tabia ya kuamini wanaweza kufanya chochote hasa kinachohusu sanaa ya muziki kumbe haiko hivyo kwani pamoja na kufanya muziki bado Serikali nayo inawajibu wa kusimamia maadili yetu.Amesema anatambua juhudi ambazo zinafanywa na Serikali katika kuhakikisha wasanii wa Tanzania wanapiga hatua na kuwa na maendeleo yanayotokana na kazi yao lakini matendo ambayo baadhi ya wasanii wanafanya yanaweza kukatisha tamaa viongozi wanaopigania maslahi ya wasanii nchini.
"Kikubwa ni vijana kuacha kutumia mitandao vibaya na kwa wasanii lazima tuunge mkono jitihada za Serikali kwa kuwa mabalozi wa kukemea matendo mabaya yanayofanyika mtandaoni,"amesema.Kwa upande wa Nandy ameendelea kuomba radhi kwa kitendo cha picha zake za faragha kusambaa mtandaoni na kusisitiza haikuwa dhamira yake na hivyo anaomba msamaha kwa Watanzania wote na hasa mashabiki wake.
"Naomba radhi kwa kilichotokea na sikuwa na tafuta kiki kama baadhi ya watu wanavyodhani, ni tukio ambalo haikuwa dhamira yangu, hivyo naomba nisamehewe,"amesisitiza Nandy wakati anazungumza akiwa TCRA.
No comments:
Post a Comment