Saturday, April 21, 2018

DC SHINYANGA AKUTANA NA WANANCHI KIJIJI CHA NYAMBUI KUTATUA MGOGORO UJENZI WA MNADA TINDE

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro amekutana na wakazi wa kijiji cha Nyambui kilichopo katika kata ya Tinde halmashauri ya wilaya ya Shinyanga kwa ajili ya kutatua mgogoro wa eneo la ujenzi wa mradi wa mnada utakaotumika badala ya ule uliopo hivi sasa. 

Mkuu huyo wa wilaya amefika katika kijiji hicho kutatua mgogoro huo leo Ijumaa Aprili 20,2018 akiwa ameambatana na maafisa mbalimbali wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga. 

Akizungumza wakati wa kikao hicho,Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro aliiagiza halmashauri kupima eneo hilo na kuboresha miundo mbinu ya mnada mpya huku akisisitiza wananchi wazawa kupewa kipaumbele katika maeneo ya biashara. 

“Niiagize halmashauri kuwa sasa tunapokwenda kuuboresha huu mnada,ni lazima kwanza tuwape kipaumbele wazawa wa eneo hili kwa sababu walikuwepo tangu mwanzoni,wakaiachia serikali kwa ajili ya maendeleo, tukishamaliza basi maeneo yanayobaki tutawapa wageni watakaokuja kufanya biashara hapa bahati nzuri majina yenu tunayo hivyo kazi itakuwa rahisi’,alieleza Matiro. 

“Tunataka tufanye mnada hapa na mnada huu unatupa pesa kama halmashauri,hivyo miundo mbinu kama choo,maji,ofisi lazima viwekwe kwenye utaratibu kabla mnada huu mpya haujaanza na tutakuja kukagua ili tuone kama yale tuliyoagiza yanafanyika? kazi ya kwanza inayotakiwa hapa ni kupima eneo na kuweka mpango kazi”,aliongeza. 

Baadhi ya wananchi wa kijiji hicho wanadai kutolipwa fidia ya ardhi na nyumba wakati wa ujenzi wa barabara ya Tinde – Kahama uliokuwa unasimamiwa na Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) ambao baada ya kukamilisha ujenzi walikabidhi eneo hilo kwenye halmashauri ambayo iliamua eneo hilo litumike kwa ajili ya ujenzi wa mnada mpya. 

Hata hivyo inaelezwa kuwa baada ya wananchi kuona halmashauri hailiendelezi eneo hilo huku mnada uliopo ukiendelea kuwa mchafu waliamua kuvamia eneo la ujenzi wa mnada huku wengine wakidai hawajalipwa fidia kupisha eneo hilo hivyo kukwamisha ujenzi huo. 

Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Ardhi na Maliasili wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, Thomas Tukay alisema jumla ya wananchi 67 wa kijiji cha Nyambui walilipwa shilingi milioni 30.4 kwa ajili ya fidia ya majengo na ardhi wakati wa ujenzi wa barabara ya Tinde – Kahama mwaka 2004 hivyo wanaodai hawajalipwa ni waongo. 

Aliongeza kuwa halmashauri hiyo iliamua kuanzisha mradi wa mnada mpya katika kitongoji cha Mwandu ili mnada wa mwanzo uliopo katika kitongoji cha Ngaka uhamie hapo Mwandu na kule Ngaka iwe sehemu ya kituo cha mabasi na malori. 

Mwenyekiti wa kijiji hicho,Richard Mpanga alisema wananchi wapo tayari kushirikiana na serikali endapo itaweka miundombinu rafiki katika mnada huo mpya. 

“Ule mnada wa kwanza ambao ni wa siku nyingi ni mchafu,hata vyoo hakuna watu wanajisaidia ovyo kwenye mlima ulipo jirani, ukiletwa hapa wananchi wanaweza kupata magonjwa,hivyo halmashauri itengeneze kwanza miundo mbinu ndiyo mnada uhamie hapa”,alisema. 

Nao wakazi wa eneo hilo waliitupia lawama halmashauri kwa kutosimamia kikamilifu mnada uliopo huku wakidai baadhi ya viongozi wa halmashauri kutokuwa waadilifu na kukwamisha mradi huo.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akizungumza na wananchi wa kijiji cha Nyambui kata ya Tinde halmashauri ya wilaya ya Shinyanga leo Aprili 20,2018 - Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akizungumza na wakazi wa Nyambui na kuwataka kushirikiana na serikali katika miradi ya maendeleo - Kulia ni mwenyekiti wa kijiji cha Nyambui Richard Mpanga ,Kushoto ni Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Ngasa Mboje
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akizungumza na wakazi wa Nyambui ili kutatua mgogoro wa eneo la ujenzi wa mnada
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akisisitiza jambo. Kushoto ni diwani wa kata ya Tinde Japhar Kanolo
Mkuu wa Idara ya Ardhi na Maliasili wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, Thomas Tukay akifafanua jambo wakati wa kikao hicho
Mwenyekiti wa kijiji cha Nyambui Richard Mpanga akifafanua kuhusu mgogoro wa eneo la mradi wa mnada na changamoto za mnada uliopo sasa.
Katibu tawala wilaya ya Shinyanga, Boniface Chambi akizungumza katika kikao hicho 
Diwani wa kata ya Tinde Japhar Kanolo akielezea kuhusu mgogoro wa eneo la mnada
Mkazi wa kijiji cha Nyambui aliyejulikana kwa jina la Mohammed akichangia hoja wakati wa kikoa hicho cha utatuzi wa kikao
Mkazi wa kijiji cha Nyambui Katale Kadama akielezea kuhusu mgogoro wa eneo la mnada na jinsi la kuutatua 
Mkazi wa Nyambui,Walesi Kiabo Kilatu akichangia hoja wakati wa kikao hicho
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akizungumza na wakati wa Nyambui akitatua mgogoro wa eneo la ujenzi wa mnada.
Kushoto ni diwani wa kata ya Tinde Japhar Kanolo akimweleza jambo mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akijadiliana na baadhi ya wananchi wa Nyambui kuhusu mgogoro wa eneo la mradi wa mnada.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akiendelea kuzungumza na wakazi wa Nyambui. Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog

No comments:

Post a Comment