Sunday, March 4, 2018

TPA MTWARA WAPEWA MIEZI MITATU KUTATUA CHANGAMOTO ZA UJENZI WA GATI

Meneja wa Bandari ya Mtwara, Bw. Nelson Mlali akiwasilisha taarifa kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (Hayupo Pichani), kuhusu mapato na matumizi ya bandari hiyo, wakati Waziri huyo alipotembelea bandari hiyo kukagua maendeleo ya mradi wa gati.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akiangalia eneo ambalo linajengwa maegesho ya kawaida ya mizigo katika bandari ya Mtwara, alipotembelea bandari hiyo kukagua maendeleo ya miradi inayotekelezwa katika bandari hiyo.
Muonekano wa hatua iliyofikiwa ya mradi wa Gati katika bandari ya Mtwara. Gati hiyo yenye urefu wa mita 300 inatarajiwa kukamilika mwaka 2019 na upanuzi wake utagharimu kiasi cha shiliingi zaidi ya bilioni 100.
Mhandisi wa Bandari ya Mtwara, Eng. Twaha Msita ambaye ni (katikati), akimwonyesha Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (kushoto), ramani ya eneo la mradi wa kuegesha mizigo ya kawaida, alipokagua maendeleo ya miradi inayotekelezwa katika bandari ya Mtwara. Kulia ni Kaimu Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Nchini (TPA), Karim Mattaka.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akitoa maelekezo kwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Nchini (TPA), Eng. Karim Mattaka (kushoto), alipokagua maendeleo ujenzi wa gati, Mkoani Mtwara.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akitoa maelekezo kwa Mkandarasi wa Kampuni ya M/s Dott Services ltd (kushoto), anaejenga Barabara ya Mtwara-Mnivata KM 50, alipokagua maendeleo ya ujenzi wake mkoani Mtwara. Kulia ni Meneja wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) Mkoani Mtwara, Eng Dotto Chacha. Wa pili kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Mtwara mjini Bw. Evod Mmanda.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akiongea na wakazi wa Nanguruwe Mkoani Mtwara alipokagua maendeleo ya ujenzi wa Barabara ya Mtwara-Mnivata KM 50 inayojengwa kwa kiwango cha Lami.


Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa, ametoa miezi mitatu kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Nchini (TPA), kuhakikisha inatatua changamoto zote zinazokwamisha mradi wa ujenzi wa gati mpya.

Prof. Marawa ametoa kauli hiyo baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Gati mpya inayojengwa Mkoani Mtwara kwa ubia wa kampuni mbili za Kichina za China Railways Major Bridges Engineering Group Co. Ltd (CRMBEG) na China Railways Construction Engineering Group (CRCEG) na kubaini mapungufu katika utekelezaji wa mradi huo.

“Hatuwezi kuendelea kuchelewesha mradi huu muhimu kwa wakazi wa Mtwara, wakati fedha zipo na mikataba imeshasainiwa, naiagiza TPA kuhakikisha kuwa inatatua changamoto hizo na kuzitafutia ufumbuzi ndani ya miezi mitatu ili mradi ukamilike kwa wakati,” amesema Waziri Prof. Mbarawa.

Ameongeza kuwa miradi inayotekelezwa na Wakandarasi wazawa chini ya usimamizi wa TPA isimamiwe kwa kuzingatia viwango na muda uliopangwa na kuahidi kurejea baada ya miezi mitatu kukagua maendeleo ya miradi hiyo.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mhandisi Karim Mattaka amemuhakikishia Prof. Mbarawa kuwa TPA itasimamia kwa karibu mradi huo na kuhakikisha mapungufu yote yanafanyiwa kazi kwa wakati.

“Nipende kukuhakikishia Waziri kuwa TPA tumejipanga vizuri kuhakikisha tunatatua changamoto zilizopo na kuanzia wiki ijayo tutaongeza kasi ya kutatua mapungufu yaliyopo ili mradi huu ukamilike kwa wakati,” amesema Mhandisi Mattaka.

Kwa upande wake Mkuu wa Bandari ya Mtwara, Bw. Nelson Mlali amesema kuwa kwa sasa mradi wa ujenzi wa gati namba mbili (2) umefikia asimilia 15 na utakapokamilika utawezesha Meli kubwa na za kisasa aina ya Panamax kuhudumiwa katika Bandari ya Mtwara ifikapo mwaka 2019.

Katika hatua nyingine Profesa Mbarawa amekagua ujenzi wa Barabara ya Mtwara hadi Mnivata KM 50 na kutoridhishwa na kasi ya ujenzi wa barabara hiyo na kuahidi kulipa madai ya Mkandarasi Kampuni ya M/s Dott Services ltd mapema iwezekanavyo ili mradi huo ukamilike kwa wakati.

‘Nimhakikishie Mkandarasi kuwa madai yake aliyowasilisha tunajipanga kuyalipa ili kasi iwe kubwa na mradi huu ukamilike kwa wakati kwa kuwa umesubiriwa na wananchi wa mkoa wa Mtwara kwa muda mrefu’ Amesisitiza Prof. Mbarawa.

Aidha, Mkandarsi wa Kampuni ya M/s Dott Services ltd amemhakikishia mhe. Waziri kuwa watahakikisha barabara hiyo inakamilika kwa wakati na kwa viwango kama ilivyoahidiwa.
Kwa upande wake Meneja wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) , Mkoani Mtwara, Eng. Dotto John ametanabahisha kuwa wakala umejipanga kuhakikisha unasimamia barabara hiyo kwa kuhakikisha viwango na ubora vinazingatiwa na kuhakikisha inakamilika kwa wakati.

Prof. Mbarawa yuko mkoani Mtwara kwa ziara ya siku moja kukagua maendeleo ya miradi ya Miundombinu ya Barabara na Bandari.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

No comments:

Post a Comment