Thursday, March 1, 2018

MBUNGE LUCY MAYENGA AKUTANA NA AKINA MAMA WAFANYABIASHARA NDOGO NDOGO MJINI SHINYANGA

Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Shinyanga, Lucy Mayenga (CCM) amefanya ziara ya kukutana na akina mama wafanyabiashara ndogo ndogo zaidi ya 250 wanaofanya shughuli zao katika Soko Kuu, Mtaa wa Sukari na Nguzo Nane mjini Shinyanga kwa lengo la kusikiliza shida zao na kujadili namna ya kuboresha biashara zao.

Mhe. Mayenga amefanya ziara hiyo leo Alhamis Machi 1,2018 akiwa ameambatana na Afisa Maendeleo ya Jamii Manispaa ya Shinyanga,Octavina Kiwone, Afisa Biashara wa Manispaa hiyo,Sunday Deogratius, Mwenyekiti wa UWT wilaya ya Shinyanga Mjini Shumbuu Katambi na madiwani wa viti maalum Zuhura Waziri na Mariam Nyangaka.

Alisema lengo la kukutana na akina mama hao ambao wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa mitaji na mazingira yasiyo rafiki ni kutoa elimu na kubadilishana mawazo kuhusu ya namna ya kuondoka katika hali waliyonayo ili wapige hatua kimaendeleo.

“Nimeanzisha utaratibu huu wa kukutana na akina mama bila kujali itikadi za vyama vya siasa,dini wala rangi kwani maendeleo hayaangalii mambo haya, wanawake wana nafasi kubwa katika kuleta mabadiliko katika jamii hivyo lazima tushirikiane na tujumuike pamoja kumaliza changamoto zinazowakabili ili tujikwamue kiuchumi”,alieleza.

Mhe. Mayenga aliwahamasisha akina mama kuunda vikundi ambavyo watavitumia kuomba mikopo katika halmashauri ya manispaa ya Shinyanga kwani serikali haiwezi kutoa pesa kwa mtu mmoja mmoja.

Aidha aliwaomba akina mama hao kuunda umoja na kila mmoja kuwa anachangia shilingi 1000 kila siku,fedha ambazo zitasaidia katika kupata mitaji mikubwa na kuinua vikundi vyao ili waweze kuinuka kiuchumi.

Katika kuunga mkono wazo hilo,Mhe. Mayenga alitoa mchango wa shilingi milioni 2.5 kwa ajili akina mama hao,kati ya fedha hizo shilingi milioni moja ni kwa akina mama katika Soko kuu,shilingi moja,Soko la Nguzo Nane na shilingi laki tano kwa ajili ya akina mama wanaofanya biashara ya mboga mboga katika mtaa wa Sukari mjini Shinyanga.

Katika hatua nyingine alizitaka halmashauri za wilaya kufuatilia vikundi vinavyopewa mikopo ili iwe na tija kwa wakopaji na kuwakumbusha akina mama wajibu wa kufanya kazi kwani serikali awamu ya tano inayoongoza na rais John Magufuli inataka kila mtu afanye kazi.

Kwa upande wake, Afisa Maendeleo ya Jamii Manispaa ya Shinyanga,Octavina Kiwone alisema halmashauri hiyo inasajili bure vikundi huku akiwataka kuaminiana na kushirikiana pamoja na kuwa na nidhamu ya fedha.

“Kwenye biashara hakuna urafiki,pesa haina urafiki hivyo ili ufanikiwe katika biashara yako lazima uwe na nidhamu ya fedha na pia muwe makini na taasisi zinazotoa mikopo kwani siyo rafiki sana kwa wafanyabiashara”,alieleza Kiwone.
Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Shinyanga, Lucy Mayenga (CCM) akizungumza na akina mama wanaofanya biashara zao katika Soko Kuu Mjini Shinyanga waliokutana naye katika ukumbi wa CCM mkoa wa Shinyanga leo Alhamis Machi 1,2018 kwa ajili ya kutoa elimu na kubadilishana nao mawazo namna ya kuboresha biashara wanazofanya - Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Shinyanga, Lucy Mayenga akizungumza na akina mama zaidi ya 100 wanaofanya biashara zao katika Soko Kuu mjini Shinyanga.
Mfanyabiashara katika Soko Kuu Mjini Shinyanga,Winfrida Rwehumbiza akimshukuru Mbunge Lucy Mayenga kwa kuwafikia akina mama wafanyabiashara wenye mitaji midogo.
Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Shinyanga, Lucy Mayenga akizungumza na wafanyabiashara katika Mtaa wa Sukari mjini Shinyanga.
Afisa Maendeleo ya Jamii Manispaa ya Shinyanga,Octavina Kiwone akitoa elimu ya vikundi kwa wafanyabiashara wa mbogamboga katika mtaa wa Sukari mjini Shinyanga
Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Shinyanga, Lucy Mayenga akinunua tende katika mtaa wa Sukari mjini Shinyanga wakati wa ziara yake ya kukutana na wafanyabiashara wadogo wadogo.
Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Shinyanga, Lucy Mayenga akichukua fungu la bamia katika mtaa wa Sukari
Lucy Mayenga akizungumza na akina mama wanaofanya biashara zao katika Soko la Nguzo Nane mjini Shinyanga. Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog

No comments:

Post a Comment