Saturday, March 17, 2018

KAMATI YA BUNGE YA HUDUMA ZA JAMII YAVUTIWA NA MIRADI YA TASAF MKOANI SIMIYU.


NA ESTOM SANGA- BARIADI

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii wamefanya ziara mkoani Simiyu na kuvutiwa na mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa Miradi ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii –TASAF-mkoani humo.

Wajumbe hao walianza ziara yao kwa kusomewa taarifa ya utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo ambapo Katibu Tawala wa Mkoa huo , Jumanne Sagini aliwajulisha Wajumbe hao kuwa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaotekelezwa na TASAF,umekuwa chachu muhimu katika kuleta maendeleo ya wananchi katika mkoa huo mpya.

Amesema kupitia Mpango huo Walengwa wameboresha maisha kwa kuendelea kujenga mkazi bora, kuchimba visima vya maji, uanzishwaji wa mashamba ya pamba ili kujiongezea kipato huku pia sekta za Afya na Elimu zikiendelea kunufaika na utekelezwaji wa Miradi ya TASAF.

Wakiwa katika Wilaya ya Maswa ,mkoani humo, Wajumbe hao walioongozwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe.Stephen Rweikiza, walipata fursa ya kutembelea baadhi ya kaya za Walengwa ambako walishuhudia mafanikio ya ujenzi wa Nyumba ya mmoja wa Walengwa wa TASAF ,Monica Kwilasa katika kijiji cha Shanwa ambaye ametumia sehemu ya ruzuku aliyopata kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kuboresha Makazi yake.

Kama Wahenga wasemavyo “ Kuona ni kuamini” Wajumbe wa kamati hiyo walionyesha kushangazwa na mafanikio ya Mlengwa huyo ambaye aliwajulisha namna alivyotumia fedha alizozipata kutoka TASAF kuanzisha biashara ndogo ndogo iliyomwongezea kipato na kumwezesha kujenga nyumba kwa matofali ya saruji na kuezeka kwa mabati.

Akizungumza na Walengwa na Wananchi katika eneo la shule ya Sekondari ya Nyalikulungu ambako pia TASAF imejenga majengo, Mwenyekiti wa Kamati Mhe. Rweikiza,amesema mafanikio yaliyoanza kupatikana katika utekelezaji wa Mpango huo ni kielelezo cha namna Serikali inavyopiga vita umaskini kwa kutumia mbinu mbalimbali ambazo amesema zinapaswa kuungwa mkono na wananchi. Zifuatazo ni picha za ziara hiyo ya kamati ya huduma za jamii ya bunge.
Wajumbe wa kamati ya Kudumu ya Bunge ya huduma ya Jamiii wakiwa mbele ya nyumba iliyojengwa na mmoja wa Walengwa kwa ruzuku ya TASAF Bi. Monica Mwalu, (aliyekamata karatasi) katika kijiji cha Shanwa wilayani Maswa . Aliyevaa kofia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Mkuchika.
Mmoja wa wajumbe wa kamati ya kudumu ya bunge ya huduma za jamii,Mhe. Venance Mwamoto (aliyevaa koti) akitoka ndani ya nyumba iliyojengwa na mmoja wa walengwa kwa ruzuku ya TASAF.
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii, Wakikagua moja ya Majengo yaliyojengwa na TASAF katika shule ya Sekondari ya Nyalikulungu katika wilaya ya Maswa mkoani Simiyu.
Waziri Mkuchika (aliyevaa kofia ) na baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya huduma za Jamii wakikagua zoezi la ilipaji wa ruzuku kwa Walengwa wa TASAF katika kijiji cha Shanwa Wilayani Maswa ruzuku ambayo imeanza kuboresha maisha yao kwa kiwango kikubwa.
Baadhi ya wanafunzi wa shule ya sekondari ya Nyalikulungu wilayani Maswa wakisikiliza hotuba ya Mwenyekiti wa kamati ya Kudumu ya Bunge ya huduma za jamii Mhe.Steven Rweikiza (hayupo pichani).
Baadhi ya Walengwa wa TASAF katika kijiji cha Shanwa wilaya ya Maswa wakisikiliza hotuba ya Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya huduma za jamii Mhe. Steven Rweikiza( hayupo pichani) wakati kamati hiyo ilipokagua miradi ya TASAF mkoani Simiyu.
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya huduma za Jamii, wakimsikiliza mmoja wa Walengwa wa TASAF Bi.Monica Mwalu mkazi wa kijiji cha Shanwa wilayani Maswa namna alivyotumia sehemu ya ruzuku kujiongezea kipato na kujenga nyumba (iliyoko nyuma yao) kuboresha makazi yake.

No comments:

Post a Comment