Friday, March 2, 2018

DC MATIRO AWARUDISHA KAZINI WATUMISHI WA AFYA WALIOTUMBULIWA ZIARA YA NAIBU WAZIRI MAVUNDE

Watumishi wa afya 22 katika hospitali ya Kolandoto manispaa ya Shinyanga wamerudishwa kazini na mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro mara baada ya kutumbuliwa na uongozi wa hospitali hiyo kutokana na kutoa malalamiko yao mbele  Naibu Waziri wa Kazi, Ajira na Vijana Athony Mavunde alipofanya ziara yake Februari 27,2018.


Watumishi hao walifukuzwa kazi siku moja baada ya ziara ya Naibu Waziri huyo kwenye hospitali hiyo ambayo aliifanya  Februari 27 mwaka huu mara baada ya kutoa malalamiko yao juu ya kunyanyaswa na hospitali hiyo ambapo kesho yake wale waliojifanya wazungumzaji 'kiherehere' wakatimuliwa kazi na kutolipwa stahiki zao zote.


Akiongea Machi 1, 2018 na uongozi wa hospitalini hapo mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro alisema mara baada ya kupewa taarifa hizo juu ya watumishi hao kuwa wametimuliwa kazi baada ya kusema ukweli kwenye ziara ya Naibu Waziri huyo, jambo hilo limemkera na kuamua kufika kwenye hospitali hiyo kuwarudisha kazini.

“Kuanzia sasa watumishi wote mliowafukuza kazi wanarudi kazini na ninatoa siku 14 wawe wameshalipwa haki zao zote wanazodai, ikiwamo malimbikizo ya mishahara, makato ya NSSF,TUGHE, pamoja na kulipwa mishahara kiwango cha serikali, na msipofanya hivyo ndani ya siku hizo tutawachukulia hatua,”alisema.
"Kwanza hospitali hii mmeidharau serikali kwa sababu haiwezekani kiongozi mkubwa kama yule Naibu waziri anafanya ziara ya kusikiliza na kutatua kero za watumishi, halafu ninyi kesho yake mnawafukuza kazi, huo ni utovu wa nidhamu”,alisema Matiro.
Naye mmoja wa watumishi hao walifukuzwa kazi Elizabeth Zabron alisema baada ya kutoa malalamiko yao juu ya kunyanyaswa kwenye mishahara na madai mbalimbali, muda mfupi tu baada ya kuondoka Naibu Waziri huyo wakaona majina ya watu 22 yakiwa yamebandikwa kwenye ubao wa matangazo wakiitwa kesho kuonana na uongozi wa hospitali hiyo.
Alisema baada ya kwenda kuonana na uongozi huo wakajua tayari kilio chao kimesikika cha kulipwa mishahara na madai yao, ambapo wakashangaa wanaambiwa kuwa wamefukuzwa kazi na wanatakiwa kusaini barua hizo bila ya kuzisoma, ndipo wakagoma na kuamua kwenda kushitaki kwa mkuu huyo wa wilaya ili wapate haki zao.
Barua hizo kwa ndani zilikuwa zimeandikwa kuwa "unafukuzwa kazi na hutakiwa kulipwa haki yako yoyote na kutakiwa kuondoka eneo la kazi mara moja".
Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo Dkt .Maganga Dohoi alikiri kuwafukuza kazi watumishi hao na kudai kuwa bodi ya hospitali hiyo ilikaa na kuagiza watumishi wote wasio na sifa ya kuwa na vyeti vya kidato cha nne lakini wana taaluma ya uuguzi wafukuzwe kazi, ndipo naye akafuata maagizo hayo.
Hata hivyo mmoja wa wajumbe wa Bodi ya hospitali hiyo Magezi Magedi ambaye pia ni ofisa utumishi wa halmashauri ya manispaa ya Shinyanga, alikana kukifahamu kikao cha kufukuza watumishi hao , na kudai kama suala la kufukuza kazi kuna taratibu zake zinatakiwa kufuatwa na siyo kuwafukuza hovyo hovyo. 
Alisema  hospitali hiyo isitumie kivuli cha serikali kufukuza watumishi hao ikiwa suala la vyeti vya darasa la Saba lilikuwa la watumishi tu wa serikali.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akizungumza na watumishi wa afya katika hospitali ya Kolandoto waliotimuliwa kazi.-Picha na Marco Maduhu - Shinyanga News blog & Malunde1 blog
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akionyesha masikitiko namna walivyotendewa ndivyo sivyo watumishi hao wa afya katika hospitali ya Kolandoto kwa kutimuliwa kazi kisa wametoa malalamiko yao mbele ya Naibu waziri wa Kazi,Ajira na Vijana Anthony Mavunde.
Mmoja wa watumishi waliofukuzwa kazi Elizabeth Zabroni akielezea kisa cha kufukuzwa kazi
Emmanuel Makungu naye alidai wamekuwa wakilipwa mishahara lakini hawapewi Salary Slip wala kusaini popote na kutokujua umeingia mshahara wa mwezi gani na pia michango ya NSSF wamekuwa wakiambiwa imeingizwa lakini wakifuatilia hakuna pesa yoyote iliyowekwa pamoja na fedha za likizo kutopewa, na kubainisha kuwa walipotoa malalamiko yao mbele ya Naibu Waziri wa Kazi,Ajira na Vijana Antony Mavunde iliwapate haki zao wakaonekana kuwa kikwazo na kutimuliwa kazi.
Sara Mkem akionyesha kusikitishwa na uongozi wa hospitali hiyo kwa kuwafukuza kazi kisa wametoa matatizo yao mbele ya Naibu Waziri huyo ili yapate ufumbuzi, na kuonekana kuwa kero na kutimuliwa kazi, bila hata ya kujali utu wao pamoja na kulazimishwa kusaini barua bila ya kuzisoma  na kudai uongozi huo una roho ya kinyama kwani huenda ina dhamira ya kutaka arudi uraiani akauawe na watu wabaya kwa kumkata viungo vyake.
Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo Dkt Maganga Dohoi akijitetea kwa mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro
Baadhi ya watumishi waliofukuzwa kazi na uongozi wa hospitali ya Kolandoto wakiwa kwenye kikao na mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro na uongozi wa hospitali hiyo kutatua suala lao la kufukuzwa kazi mara baada ya kutoa kilio chao kwa Naibu Waziri wa Kazi,Ajira na Vijana Antony Mavunde juu ya manyanyaso wanaoyapata .
Watumishi wa afya waliofukuzwa kazi katika hospitali ya Kolandoto wakiwa kwenye kikao cha kutatuliwa matatizo yao na mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro mara baada ya kumpelekea matatizo yaliyowakumba ya kutimuliwa kazi kinyemela bila ya kufuata sheria za kazi.
Kikao kikiendelea.
Watumishi wa afya katika hospitali ya kolandoto waliofukuzwa kazi kenyemela wakiwa wameshika bango la kutaka haki yao
 Ofisa utumishi wa halmashauri ya manispaa ya Shinyanga,Magezi Magedi ambaye pia ni mjumbe wa bodi ya hospitali hiyo ya Kolandoto akikana kukifahamu kikao cha kufukuza kazi watumishi hao na wala tangu achaguliwe kuwa mjumbe wa bodi hiyo hajawahi kuitwa hata kikao kimoja  na kudai kama suala la kufukuza kazi watumishi hao kuna taratibu zake zinatakiwa kufuatwa, na siyo kuwafukuza hovyo hovyo na kuwalazimisha kusaini barua bila ya kuzisoma. 
 Ofisa kazi mkoa wa Shinyanga Revocatus Mabula alisema taratibu za kuwafukuza kazi watumishi hao zilikiukwa ambapo hawakupewa notes na walistahili kupewa haki zao zote ndani ya siku 14,kulipwa kiinua mgongo,malimbikizo ya likizo zao zote pamoja na kusafirishwa mahali walipotoka makwao na siyo kuambiwa tu wamefukuzwa kazi na hawatolipwa pesa yoyote.
Katibu wa Chama Cha Wafanyakazi TUGHE, Tabu Mambo alisema hawajahi kuona mchango wowote wa watumishi hao waliofukuzwa kazi licha ya kuambiwa kuwa wanalipiwa na kubainisha kuwa walipokuwa wakifika kuzungumza na watumishi hao walikuwa wakikosa ushirikiano kutoka kwa viongozi wao, na wale watumishi ambao walioonekana kuwa wanajua kuongea ndiyo kidogo walikuwa wakitolewa michango hiyo.
Picha na Marco Maduhu - Shinyanga News blog & Malunde1 blog

No comments:

Post a Comment