Wednesday, March 7, 2018

CHUO CHA UTUMISHI WA UMMA TANZANIA (TPSC) KUWAJENGEA UWEZO WATUMISHI WA UMMA JIMBO LA PUNTLAND NCHINI SOMALIA


Aliyekuwa Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Angellah Kairuki (wa Pili Kulia) na Waziri wa Kazi,Vijana na Michezo wa Puntland Abdurahman Ahmed Abdulle wakisaini mkataba wa Makubaliano ya ushirikiano wa kuboresha sekta ya utumishi wa umma jimboni Puntland ambapo serikali kupitia Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) itaendesha mafunzo hayo kwa kushiriakana na Chuo Kikuu cha Puntland. Kulia Mkuu wa TPSC Dk. Henry Mambo. 

Wataalamu waandamizi kutoka Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC), wapo nchini Somalia kwa ajili ya kazi ya kuandaa mafunzo ya kuboresha utumishi wa umma katika Jimbo la Puntland nchini Somalia. 

Kazi hiyo inafanyika kwa ushirikiano kati ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania na Chuo Kikuu cha Taifa cha Puntland kilichopo Jimbo la Puntland nchini Somalia. Mkuu wa Chuo Dkt Henry Mambo alisema kwamba watumishi hao waliondoka nchini tarehe 3 mwezi Machi mwaka huu na wanatarajia kurejea chini tarehe 11 mwezi huu. Dkt Mambo alisema mafunzo hayo yanafanyika ikiwani ushirikiano kati ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania na Chuo kikuu cha Taifa cha Puntland kilichopo Jimbo la Puntland nchini Somalia. 

Alifafanua kuwa ushirikiano huo ni matokeo ya hati ya makubaliano iliyosainiwa mwezi Mei, 2017 Makao Makuu ya Chuo cha Utumishi wa Umma Jijini Dar es Salaam na wakuu wa vyuo hivyo viwili, Dr. Henry Mambo ambaye ni Mkuu wa TPSC na Bw. Mohamud Hamid Mohamed ambaye ni Mkuu wa Chuo kikuu cha Taifa cha Puntland. Makubaliano hayo yalishuhudiwa na aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejiment ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Angellah Kairuki na Waziri wa Kazi, Vijana na Michezo wa Puntland Mh. Abdirahman Ahmed Abdulle. 

Kwa mujibu wa makubaliano hayo Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania kitashirikiana na Chuo Kikuu cha Puntland kuandaa na kuendesha mafunzo mbalimbali ya muda mfupi na mrefu ili kuwajengea uwezo watumishi wa umma wa Puntland. Maeneo yaliyopewa kipaumbele katika uandaaji wa mafunzo ni pamoja na;Rasilimali watu (Human Resources Management), Utawala wa Fedha (Financial Management), Masuala ya Manunuzi (Procurement Management), 

Mengine ni Tekonolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT), Mipango, Tathmini na Ufuatiliaji, (Planning, Monitoring and Evaluation), Sera,Tafiti pamoja na Utunzaji wa Kumbukumbu. Mpango huo wa Puntland unafadhiliwa na Benki ya Dunia ambao unatarajiwa kufadhili zoezi zima la uandaaji wa mafunzo hayo. 

No comments:

Post a Comment