Thursday, March 1, 2018

CCM ZANZIBAR YATOA AGIZO ZITO KWA VIONGOZI WA CHAMA NA SERIKALI.

NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.
TASNIA ya Habari ni sekta muhimu inayoziwezesha Serikali mbali mbali Duniani kuimarisha dhana ya Demokrasia kupitia matangazo na taarifa za utekelezaji wa Ilani ya Chama tawala, miongozo na mipango ya maendeleo ili wananchi wajue uwajibikaji wa serikali yao na kupima uhalisia wa sera zinazotekelezwa kama zinakidhi mahitaji yao.
Maelezo hayo yametolewa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Bi. Catherine Peter Nao katika mwendelezo wa ziara yake katika vyombo Zanzibar, aliwaagiza viongozi na watendaji wa Chama na Serikali kupanga utaratibu wa   kuzungumza na vyombo vya Habari mara kwa mara  ili waweze kuwaeleza wananchi utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku katika taasisi zao.
Catherine alisema kiongozi yeyote mwenye dhamana ya kutoa taarifa za Chama ama Serikali atakayekataa kuzungumza na vyombo vya habari atakuwa anaenda kinyume na falsafa ya CCM mpya na Tanzania mpya inayotaka Chama kirudi mikononi mwa wananchi kwa kuanza na hatua ya kuwapatia taarifa sahihi zinazohusu masuala ya maendeleo.
Alisema kiongozi anayetekeleza wajibu wake vizuri hawezi kuwa na hofu ya kuzungumza na vyombo vya habari, hivyo ni lazima watumishi hao wa umma kukubali mabadiliko ya zama mpya za utandawazi zinazotoa fursa ya wananchi kuhoji na kudadisi viongozi waliowapa dhamana nini wamefakanya katika maeneo yao.
“Serikali ya Mapiunduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Dk. Ali Mohamed Shein imefanya mambo mengi mazuri lakini cha kusikitisha wananchi wengi hawajui serikali yao nini inafanya kutokana na baadhi ya Viongozi wenye dhamana ya kuzungumza wapo kimya”, alisema Catherine.
 Agizo hilo limekuja baada ya Vyombo vya Habari mbali mbali nchini kulalamikia urasimu usikuwa na tija wa baadhi ya Viongozi na Watendaji wa Chama na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kutotoa ushirikiano kwa taasisi za kihabari hali inayosababisha baadhi ya vyombo hivyo kutoa taarifa za upande mmoja baada ya kukosekana ushirikiano kutoka kwa viongozi wa umma.
Pia aliwapongeza Mwenyekiti wa CCM Taifa Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein kwa juhudi zao za kusimamia na kutekeleza ilani ya CCM kwa kasi kubwa hatua inayoleta furaha ya kudumu kwa wananchi.
Hata hivyo Katibu huyo alisema licha ya kuwepo na changamoto mbali mbali za kiutendaji bado CCM inaendelea kubaki katika msimamo wake kwa mujibu wa Ibara ya tano ya Katiba ya CCM ya mwaka 1977 kwa kuhakikisha mwaka 2020 CCM inashinda katika Uchaguzi wa ngazi zote  na kubaki madarakani.
Alisema lengo la ziara hiyo ni kujitambulisha kwa vyombo hivyo ambavyo ni wadau wakubwa wa Chama Cha Mapinduzi ili waweze kufanya kazi kwa ushirikiano kwa maslahi ya wananchi.
Akizungumza Mkurugenzi wa Swahiba FM Radio, Maalim Kassim Mohamed Kassim alisema Vyombo vya habari vipo kwa ajili ya wananchi hivyo kiongozi yeyote aliyepewa dhamana na wananchi ana wajibu wa kutoa ushirikiano kwa taasisi hizo.
Naye Mhariri Mtendaji wa Shirika la Magazeti ya Serikali Zanzibar, Yussuf Khamis Yussuf amesema Shirika hilo litaendelea kutoa habari mbali mbali zinazohusu utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020, huku wakizingatia kanuni na miongozi ya maadili ya Tasnia ya habari.
Naye Meneja wa Chuchu Fm Salma Ahmed Alley, amesema pamoja juhudi za taasisi hiyo katika    kuelimisha, kuhabarisha, kukosoa na kuhamasisha amani na utulivu bado wanakabiliwa na  changamoto ya ukosefu wa matangazo ya biashara kutoka Serikalini na taasisi zingine hali inayosababisha baadhi ya wakati chombo hicho kuyumba kifedha.

No comments:

Post a Comment