Monday, March 5, 2018

BARAZA LA MADIWANI NA MBUNGE CHALINZE WACHARUKIA WAPIGAJI KWENYE VIZUIA VYA USHURU

Na Mwamvua Mwinyi, Chalinze.

MADIWANI wa Halmashauri ya Chalinze, pamoja na mbunge wa jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete wamewasimamisha wakusanyaji wa ushuru kwenye baadhi ya vizuia, kutokana na kudaiwa kujihusisha na wizi na upotevu wa vifaa  ili kupisha uchunguzi .

Pia, wameitaka halmashauri hiyo kutumia walinzi wenye silaha kwenye vizuia vikubwa vya ukusanyaji ushuru ikiwemo wa kokoto ili kukabiliana na wizi unaotokea mara kwa mara.

Maamuzi hayo ,yamefanyika baada ya madiwani hao kulalamikia wizi na hujuma zinazofanywa na wakusanyaji kwa kushirikiana na baadhi ya watendaji wa halmashauri wasio waaminifu.

Ridhiwani alisema ,kizuia cha Lugoba ni kero sanjali na Mpaji ,Mbwewe na Lunga ambapo kizuizi cha Lugoba kimeshavamiwa zaidi ya mara moja na matukio hayo yanaendelea kujitokeza hivyo wahusika lazima wachunguzwe.

“Mashine za ukusanyaji wa mapato zinaibiwa kirahisi rahisi ,hakuna kinachoendelea hivyo mchezo huu unavyoendelea halmashauri inapata hasara ”alifafanua Ridhiwani.

Aidha Ridhiwani aliitaka halmashauri hiyo kupitia mikataba mbalimbali na kufanyia marekebisho baadhi ya sheria ili kukabiliana na watu wanaotumia mianya ya mikataba na sheria hizo kufanya ubadhilifu.

Alieleza mikataba hiyo haina makali katika kuwawajibisha watumishi ambao wamehusika na upotevu wa vifaa ama mali za halmashauri.

“Vifaa viwili vimepotea lakini hakuna hatua za kuwawajibisha watumishi hao,“limetokea tukio la wizi kwenye kizuizi cha Lugoba hakuna hatua zilizochukuliwa badala yake wahusika wanaendelea na kazi ,”Na waliopoteza vifaa vinavyotoa taarifa za makusanyo kwenye vyanzo hivyo ,” alisisitiza Ridhiwani.

Alisema kuwe na vipengele vya mtumishi endapo anatuhumiwa kwa upotevu wa fedha ama mali achukuliwe hatua stahiki ili kuongeza uwajibikaji kazini.

Nae mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Saidi Zikatimu alisema matukio ya wizi kwenye kizuia cha Lugoba yamekithiri kwani tukio la kwanza wezi walifanikiwa kuiba kiasi cha sh. mil 2.5#.

Alielezea kwamba, wezi hao walirudia kuiba mara ya pili lakini hata hivyo hawakuweza kufanikiwa kuiba baada ya kudhibitiwa.

“Kutokana na hilo, madiwani wameshtuka na kuamua kulalamika kuwa inawezekana kuna mchezo unaofanyika baina ya wakusanyaji na baadhi ya watendaji wa halmashauri” alisema Zikatimu.

Zikatimu alisema, atakaebainika kuhusika na wizi huo na kusababisha hasara na kushuka kwa mapato ya halmashauri baada ya uchunguzi kukamilika atachukuliwa hatua za kisheria.

Alisema watakaobainika watafukuzwa kazi na kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma zitakazowakabili.

Diwani wa Kata ya Lugoba, Rehema Mwene alifafanua ili kudhibiti hali hiyo haina budi kukawekwa walinzi wenye silaha badala ya kutumia walinzi wasio na silaha.

Alisema wapo walinzi katika baadhi ya vizuizi wanalinda na silaha za jadi ikiwemo marungu ,kwa hali hiyo haiwezekani watu walinde mamilioni ya fedha kwa rungu.

“Wezi wanacheza na wakati ,wanatumia silaha za kisasa,sasa endapo walinzi wetu wakiendelea kulinda na mapanga na marungu ni hatari na tutaibiwa kila siku”alisema Rehema.

Kwa upande wake, diwani wa Kata ya Pera, Lekope Laini alieleza ,ziwepo sheria zitakazowabana watendaji wanaokwenda kinyume na sheria na taratibu ili kunusuru mapato yanayopatikana.

Kwa mujibu wa mkurugenzi wa halmashauri ya Chalinze, Edes Lukoa amepokea maamuzi yote  na kuahidi kuyafanyia kazi.

Alisema halmashauri imeshaanza kutumia walinzi toka Suma Jkt kwenye kituo cha Msata hivyo wataendelea kuangalia uwezekano wa kuweka walinzi walio waaminifu na wenye silaha kwenye meneo mengine.

Lukoa ,alisema lengo la halmashauri ni kuinua mapato na sio kudidimiza mapato ,ili hali kutatua kero za kijamii zinazowakabili wananchi wa halmashauri hiyo.
 Mwenyekiti wa halmashauri ya Chalinze Saidi Zikatim akuzungumza jambo wakati wa baraza la madiwani la Chalinze lililofanyika ukumbi wa mikutano wa halmashauri ya Chalinze
Mbunge jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete akuzungumza jambo wakati wa baraza la madiwani la Chalinze lililofanyika ukumbi wa mikutano wa halmashauri ya Chalinze.
 Baadhi ya madiwani wa halmashauri ya Chalinze ,wakionekana pichani kusikiliza kwa makini jambo wakati wa baraza la madiwani.

No comments:

Post a Comment