Monday, February 26, 2018

WATANZANIA KUPENYA SOKO LA KENYA

 Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Adolf Mkenda akifafanua jambo kwa washiriki wa kikao cha kujadili maandalizi ya wiki ya Tanzania nchini Kenya mapema hii leo jijini Dar es Salaam. Kuia ni Balozi wa Tanzania nchini Kenya Dk. Pindi Chana na katikati ni Mtendaji Mkuu wa TANTRADE Edwin Rutageruka.
Baadhi ya washiriki wa kikao cha kujadili maandalizi ya wiki ya Tanzania nchini Kenya wakimsikiliza Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Adolf Mkenda (hayupo pichani) wakati wa kikao hicho mapema hii leo jijini Dar es Salaam.
Picha na Eliphace Marwa - MAELEZO

Jonas Kamaleki- MAELEZO.

Serikali imetoa wito kwa  wafanyabiashara wa Tanzania kupeleka bidhaa zao katika soko la Kenya ili kupanua wigo wa masoko ya bidhaa zao.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Adolf Mkenda wakati wa kikao cha Maandalizi ya Wiki ya Tanzania nchini Kenya.

Prof. Mkenda alisema kuwa ni nia ya Serikali kuhakikisha watanzania wanapenya katika masoko ya kimataifa ili kuongeza pato la mtu binafsi na la Taifa kwa ujumla.“Hali ya biashara kwa sasa ni nzuri sana, hivyo vikwazo visiwepo kabisa kati ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki”, alsiema Prof. Mwaikenda.

Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Balozi, Dkt. Pindi Chana amesema kuwa watanzania inabidi wathubutu na kuingia katika soko la Afrika Mashariki hususan soko la Kenya.Amesema kuwa wafanyabiashara wa Kitanzania wasiogope kuingia katika masoko ya nje ya nchi, wajitahidi ili waweze kuongeza vipato kutokana na ukubwa wa soko lililopo nchini na Kenya kwa ujumla.

“Mkifanya biashara Kenya mtaongeza mitaji, ajira na kipato kwa ujumla kwani nchi hizi mbili zina zaidi ya watu milioni 90”, na hii inaendana na falsafa ya Mhe. Rais John Pombe Magufuli ya Uchumi wa Viwanda, hivyo hatuna budi kufuata maono ya Kiongozi wetu na kutengeneza na kuuza bidhaa za viwandani nje ya nchi”, alisema Balozi Pindi Chana.

Akizungumza katika kikao hicho, Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Juma Ali Juma amesema wazo la kufungua soko la Kenya ni zuri na kumpongeza Balozi Pindi Chana kwa ubunifu huo.

Aliongeza kuwa anafahamu kuwa zipo changamoto ndogo ndogo katika masoko lakini zinafanyiwa kazi ili kuhakikisha biashara kati ya Tanzania na Kenya inaenda vizuri.Bwana Juma alisisitza kuwa bidhaa zinazozalishwa nchini inabidi ziwe na ubora na kuwa na vifungashio bora ili kumvutia mteja kununua.

Naye  Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara nchini (TANTRADE), Edwin Rutageruka amesema watanzania waende Kenya wakijiamini kwani bidhaa zao zinahitajika sana.Aliwataka wafanyabiashara kujenga maghala mipakani ili kutunza bidhaa zao humo na kuziuza kwa bei nzuri wakati muafaka.

Akichangia mada katika kikao cha maandalizi, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF), Godfrey Simbeye aliwaomba seka binafsi wajitokeze ili kupeleka bidhaa zao nchini Kenya na kuitumia hiyo fursa katika kukuza biashara zao.

Simbeye aliiomba Serikali kuwapeleka waambata wa kibiashara kwenye balozi za Tanzania Duniani ili washughulikie suala la masoko na fursa nyingine za kibiashara.Kikao hiki cha maandalizi kimetokana na maono ya Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana ambaye amebuni wazo la kufanya wiki ya Tanzania nchini Kenya kwa ajili ya kutafuta soko la bidhaa za Tanzania ambayo itafanyika 26 Aprili, 2018 na itadumu kwa wiki moja.

No comments:

Post a Comment