Friday, February 2, 2018

UGENI MAHAKAMA YA JUU NCHINI GUATEMALA WAKUTANA NA JAJI MKUU WA TANZANIA

Na Mary Gwera
Katika mwendelezo wa Utekelezaji wa Mpango Mkakati wake wa miaka mitano (5) (2015/2016-2019/2020), Mahakama ya Tanzania inaendelea na jitihada za kupata uzoefu na ujuzi kutoka katika Mahakama mbalimbali duniani zilizopiga hatua katika maboresho ya huduma ya utoaji haki kwa wananchi.

Haya yamejidhihirisha kufuatia ugeni wa Maafisa wa Mahakama waliowasili kutoka nchini Guatemala kwa mualiko wa Mahakama ya Tanzania kushiriki katika Hafla ya Siku ya Sheria nchini, iliyofanyika Februari 01, 2018 vilevile Mahakama ya Tanzania kupata maoni na ushauri zaidi wa jinsi ya kuendelea kuiboresha Mahakama nchini kwa manufaa ya wananchi ambao ndio walengwa Wakuu.

Akiwatambulisha wageni hao kwa Mhe. Jaji Mkuu wa Tanzania, Februari 1 katika Ofisi ya Mhe. Jaji Mkuu, Mahakama ya Rufani Dar es Salaam, Mtendaji Mkuu, Mahakama ya Tanzania, Mhe. Hussein Kattanga alisema kuwa takribani miaka mitatu sasa baadhi ya Maafisa wa Mahakama nchini walifanya ziara nchini Guatemala kwa lengo la kujifunza ni kwa namna gani Mahakama nchini Guatemala imefanikiwa katika utoaji wa huduma zake.

“Mhe. Jaji Mkuu, tulichojifunza na tukaona ni vyema kuiga kutoka Guatemala ni pamoja na huduma ya Mahakama inayotembea ‘mobile court’, ufanyaji kazi wa Mahakama kwa masaa 24, kuweka mbele matumizi ya teknolojia katika shughuli zake  n.k, hivyo tumeona ni vyema pia kwa Mahakama nchini kupata utaalamu/uzoefu kutoka kwa wenzetu jinsi ya kuweza kutekeleza haya,” alisema Bw. Kattanga.

Mahakama ya Tanzania imeonyesha nia ya dhati katika suala zima la maboresho, hivyo basi ujio wa Wageni hawa ambao watakuwepo nchini kwa takribani siku 5, utawezesha Wataalamu wa Mahakama kupata uzoefu na ujuzi zaidi wa namna gani Mahakama zinazotembea zinavyofanya kazi n.k.
Aidha; kwa upande wake, Jaji Mkuu aliyemaliza muda wake wa Mahakama nchini Guatemala, Mhe. Osvaldo Mendez alisema kuwa Mahakama nchini humo amepiga hatua kubwa katika suala zima la Matumizi ya TEHAMA hali ambayo imesaidia kurahisisha utendaji na kutoa haki kwa wakati.

“Mahakama yetu pia inafanya kazi masaa 24, na tunatoa huduma hii katika Miji mikubwa mitano nchini Guatemala na tunafanya kwa ushirikiano na Wadau wetu wa Mahakama kama Waendesha Mashitaka ‘Prosecutors’ n.k ili kufanikisha kumaliza mashauri hayo kwa muda muafaka,” alieleza Mhe. Mendez.

Mpango Mkakati unaotekelezwa na Mahakama umegawanyika  katika nguzo kuu tatu ambazo ni Utawala na Menejimenti bora ya Rasilimali, Upatikanaji na utoaji wa Haki kwa wakati na kuimarisha imani ya Jamii na Ushirikishaji wa wadau katika shughuli za Mahakama; nguzo zote zikilenga katika uboreshaji wa huduma za Mahakama.
  Jaji Mkuu wa Tanzania (pichani) akiwa katika mazungumzo na Wageni hao (hawapo pichani), katika mazungumzo yao Mhe. Jaji Mkuu amefurahishwa na hatua iliyofikiwa na Mahakama nchini Guatemala.
 Jaji Kiongozi, Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Ferdinand Wambali akiongea jambo na Wageni hao, Mhe. Wambali aliwaelezea Wageni hao juu ya Mfumo wa Mahakama nchini.
  Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (aliyeketi mbele) akiwa pamoja na baadhi ya Wahe. Majaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Jaji Kiongozi, Mtendaji Mkuu na Ugeni kutoka Mahakama nchini Guatemala pindi Wageni hao walipomtembelea Mhe. Jaji Mkuu ofisini kwake jijini Dar es Salaam.
 Mtendaji Mkuu, Mahakama ya Tanzania, Mhe. Hussein Kattanga akizungumza jambo katika kikao hicho.
 Jaji Mkuu aliyemaliza muda wake wa Mahakama nchini Guatemala, Mhe. Osvaldo Mendez akizungumza jambo.
 Mtaalamu kutoka Benki ya Dunia, Bw. Waleed Malik akiongea jambo katika kikao hicho.
Picha ya pamoja baada ya mazungumzo.


(Picha na Mary Gwera, Mahakama)

No comments:

Post a Comment