Monday, February 5, 2018

TIBA MTANDAO KUBORESHA HUDUMA ZA AFYA NCHINI

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Dkt. Mpoki Ulisubisya akisisitiza jambo kwa wataalamu wa sekta ya afya wakati wa kongamano la ubunifu na utekelezaji wa huduma za tiba mtandao Tanzania lililofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa LAPF, Dodoma.
Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Eng. Peter Ulanga, akiwasilisha mada kuhusu umuhimu wa tiba mtandao nchini kwa wataalamu wa sekta ya afya (hawapo pichani) wakati wa kongamano la ubunifu na utekelezaji wa huduma za tiba mtandao Tanzania ambalo limeandaliwa na UCSAF lililofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa LAPF, Dodoma.
Kaimu Mkurugenzi wa TEHAMA, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eng. Peter Phillip Mwasalyanda (aliyeketi katikati), akisikiliza kwa makini kongamano la ubunifu na utekelezaji wa huduma za tiba mtandao Tanzania ambalo limeandaliwa na UCSAF lililofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa LAPF, Dodoma
Wataalamu wa sekta ya afya wakifuatilia kwa makini maelekezo ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Mpoki Ulisubisya (hayupo pichani) wakati wa kongamano la ubunifu na utekelezaji wa huduma za tiba mtandao Tanzania ambalo limeandaliwa na UCSAF lililofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa LAPF, Dodoma


Serikali imejipanga kutumia tiba mtandao kuboresha huduma za afya nchini kwenye hospitali zote za ngazi ya taifa, rufaa na wilaya ili kuwawezesha wagonjwa waishio sehemu mbali mbali nchini kupata huduma za afya kwa wakati na kwa ufanisi.

Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Mpoki Ulisubisya wakati akifungua kongamano la ubunifu na utekelezaji wa huduma za tiba mtandao Tanzania lililofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa jengo la LAPF, Dodoma.

Dkt. Ulisubisya amesema kuwa lengo la kongamano hilo ni kuwakutanisha watendaji wakuu wa hospitali za taifa nchini, madaktari bingwa wa sekta ya Afya, wakuu wa taasisi zinazoshughulika na sekta ya Afya, Wizara ya TAMISEMI, Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano; taasisi nyingine za Serikali; sekta binafsi na wabia wa maendeleo ili kujadiliana na kuwa na uelewa wa pamoja wa kufanikisha utekelezaji wa huduma za tiba mtandao ili kuboresha huduma za afya nchini.

Amesema kuwa tiba mtandao itawezesha na kuongeza ufanisi katika kufanya uchunguzi, utoaji wa tiba na madawa kwa wagonjwa wanaosumbuliwa na magonjwa mbalimbali yasiyoambukiza na yanayotokana na ajali za barabarani. “Hadi hivi sasa ni asilimia 37 tu ya wagonjwa wa kifua kikuu ndio wanaotambulika na kupatiwa huduma na Wizara ya Afya katika hospitali mbalimbali nchini. Hivyo, tiba mtandao itawezesha upatikanaji wa wagonjwa na ufikishaji wa huduma kwao kwa wagonjwa wengine asilimia 63”, amefafanua Dkt. Ulisubisya.

Ameongeza kuwa tiba mtandao itapunguza gharama za wagonjwa na wanaowahudumia kusafiri kufuata madaktari. Aidha, amewataka wakuu hao wa taasisi kuwaruhusu wataalamu wao, wa Wizara ya TAMISEMI na wa Wizara ya Afya, kushiriki mafunzo ya tiba mtandao ili kuongeza ufanisi wao katika kuhudumia wagonjwa.

Amewataka wataalamu wa afya na wakuu wa taasisi zinazohusika na masuala ya afya kununua vifaa tiba vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) vyenye viwango na ubora unaohitajika ili kuwezesha tiba mtandao na manunuzi hayo yazingatie na kufuata ununuzi wa pamoja wa huduma na bidhaa za Serikali. 

Vifaa vya kisasa vya TEHAMA vinavyohusika na tiba mtandao vitawawezesha wataalamu kufanya uchunguzi kwa mgonjwa, kupata majibu ya uhakika na kumpatia mgonjwa tiba inayostahili na ya uhakika. Aidha, amemuelekeza Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Eng. Ulanga, ambao ndio waanadaji na waratibu wa kongamano hilo, kushirikiana na TTCL kuhakikisha kuwa tiba mtandao inapatikana katika hospitali zote za rufaa na hospitali ambazo zina changamoto ya kijiografia ya kufikika kwa urahisi. Aidha, hadi hivi sasa huduma ya tiba mtandao inapatikana katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Bagamoyo, KCMC-Moshi, Bugando-Mwanza na Benjamin Mkapa, Dodoma. 

Naye Eng. Ulanga amesema kuwa UCSAF imeanzisha huduma ya tiba mtandao kwenye vituo 14 vya majaribio. Aidha, imeainisha orodha ya vituo 279 ikiwa ni pamoja na hospitali za taifa, rufaa na wilaya ambazo zitaunganishwa na kuwezeshwa kutoa huduma ya tiba mtandao nchini.

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Saratani ya Ocean Road, Dar es Salaam Dkt. Julius Mwaiselage, akiwa mmoja wa washiriki wa kongamano hilo amesema kuwa, tayari tulikuwa tunatumia huduma ya tiba mtandao kwa wagonjwa wetu kwa kushirikiana na hospitali nyingine zilizopo nchini India kwa kuwafanyia wagonjwa uchunguzi na kuona kama kweli mgonjwa husika anahitaji kupelekwa nje ya nchi kwa matibabu zaidi. 

“Uwepo wa huduma ya tiba mtandao kwenye hospitali zetu nchini, itatuwezesha kufanya uchunguzi na kutoa tiba kwa wagonjwa waliopo mikoani hivyo kuwapunguzia gharama wagonjwa za kuja Dar es Salaam na endapo watalazimika kuja basi watakaa kwa muda mfupi ukilinganisha na hapo awali”, amesema Dkt. Mwaiselage. Washiriki wengine wa kongamano hilo ni kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Bugando, MOI, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kiwete, Mloganzila, Aga Khan, Hospitali ya Rufaa Mbeya, NHIF, PATH na Shirika la Afya Duniani.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

No comments:

Post a Comment