Monday, February 5, 2018

RAIA WAWILI WA UINGEREZA KORTINI WAKITUHUMIWA KWA MASHTAKA TISA,YAMO YA KUISHI NCHINI BILA VIBALI

Na Karama Kenyunko, blogu ya jamii.

RAIA wawili wa Uingereza na Mkurugenzi Mkuu wa Afri Transport, wamepandishwa katika kizimba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ili kujibu mashitaka tisa yakiwamo ya kufanya Kazi, kuishi na kupata vibali mbali mbali kwa njia ya uongo.

Wamepandishwa kizimbani leo Mahakamani hapo ya Hakimu Mkazi Godfrey Mwambapa na majina ya washtakiwa hao ni Mohammed Mabeeenullah Kashmiri (72) na Saleem Kashmiri (50) ambao wanashtakiwa pamoja na Mtanzania Mohammed Ameenullah Kashmiri (82) .

Katika kesi hii Ammeenullah ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Afri Transport anashtakiwa kwa kosa la kuajiri raia hao wa Ungereza bila ya kibali na kuwasaidia kupata vibali baada ya kutoa vibali vya ufeki.

Akisoma hati ya mashtaka, Mwendesha Mashtaka kutoka  Uhamiaji, Gerald Mardai amedai, Oktoba 25 mwaka jana, katika Makao Makuu ya ofisi za Uhamiaji Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam mshtakiwa Ameenullah, alikamatwa akitoa taarifa za uongo kwa ajili ya kuwapatia vibali raia hao wa Uingereza kufanya kazi nchini.

Pia aliwasaidia kupata vibali vya kuishi nchini kinyume na sheria baada ya kutoa taarifa ya uongo dhidi yao. Mshtakiwa Ameenullah anashtakiwa kwa kuwaajiri raia hao wawili wa Uingereza huku akijua kuwa raia hao hawana kibali cha kuwaruhusu kufanya Kazi nchini na bila kuwa na kibali cha kuishi nchini.

Aidha Mtanzania huyo anadaiwa kuwasaidia raia hao kutenda kosa kinyume na sheria za uhamiaji.Kwa upande wa raia wa Ungereza wao wanakabiliwa na shtaka la kujipatia nyaraka kwa kutoa taarifa za uongo, kutengeneza taarifa za uongo ili wajipatie vibali vya kuishi nchini.

Pia wanadaiwa kujiingiza katika ajira bila ya kuwa na vibali vya kufanya kazi na kujiingiza katika ajira bila ya kuwa na vibali vya kuishi nchini.
Washtakiwa wamekana kutenda makosa hayo na wako nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya dhamana.

 Mahakama  imemtaka kila mshtakiwa kuwa na wadhamini wawili watakaosaini bondi ya Sh.milioni 20.Pia wametakiwa kuwasilisha hati zao za kusafiria mahakamani na wasisafiri nje ya nchi bila ya kibali cha Mahakama.

Kesi imeahirishwa Februari 19, mwaka huu.

No comments:

Post a Comment