Thursday, February 1, 2018

Msanii Wastara awatoa hofu watanzania kuhusu matibabu yake


Na: Genofeva Matemu – WHUSM 

Msanii wa filamu nchini Bibi. Wastara Issa ameendelea kumshukuru Rais wa  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli kwa kuonyesha moyo wa kuguswa na tatizo linalomsumbua na kuweza kumpatia kiwango cha shilingi milioni 15 kwa ajili ya matibabu ya mguu pamoja na mgongo. 

Bibi. Wastara ametoa shukrani hizo jana  Jijini Dar es Salaam alipokua akizungumza na waandishi wa habari na kusema kuwa awali ilikua aondoke nchini tarehe 28 mwezi januari mwaka huu kwenda mjini Mumbai kwa ajili ya matibabu lakini kutokana na baadhi ya mipango kutokaa vizuri safari hiyo ilisogezwa hadi jumapili tarehe 4 Februari 2018 ambapo anatarajia kuondoka mida ya jioni na kufika Mumbai mapema alfajiri siku ya jumatatu ambapo ataanza matibabu siku hiyo hiyo. 

Bibi. Wastara amesema kuwa katika safari hiyo ataongozana na nesi mmoja kutoka hospitali ya TMJ pamoja na mtu mmoja kutoka katika familia yake ambapo matibabu yake yatafanyika katika hospitali ya Saifee iliyopo Mumbai na kutarajia matibabu hayo kuchukua takribani wiki tatu na zaidi. 

Aidha msanii Wastara Issa ameishukuru wizara inayosimamia tansia ya filamu kwa kumfariji katika kipindi hiki kigumu anachopitia huku akimshukuru Waziri mwenye dhamana na tasnia ya filamu nchini, Bodi ya Filamu Tanzania, Baraza la Sanaa la Taifa pamoja na watanzania wote kwa kuonyesha upendo wa dhati kwake. 

“Asanteni sana watanzania mmeonyesha moyo wa dhati kwangu kwa muda mrefu sasa, mmekua pamoja nami tangu kipindi cha matibabu ya Saduki hadi sasa, uzito wa neno asante kutoka kwangu leo hauwezi kulipa fadhila kwa dua na michango yenu kwangu, mwenyezi mungu aendelee kuifanya nchi yetu kuwa na amani na upendo” amesema msanii Wastara Issa 

Naye Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu Bibi. Joyce Fissoo amesema kuwa serikali kupitia bodi ya filamu inashukuru kwa kupata taarifa kamili ya safari ya msanii Wastari Issa ilipofikia kwani bodi ya filamu inapenda kumuona Wastara akiwa katika afya nzuri na kurudi katika hali yake ili aweze kuungana na wanatasnia wenzake kuendeleza tasnia ya filamu nchini. 

Bibi. Fissoo amesema kuwa Watanzania wengi wamekua wakiwasiliana na Wastara kwa njia mbalimbali, kumchangia na hata kufika kumuona, hivyo serikali inatambua kuwa msanii Wastara Issa yupo katika maandalizi ya safari ambapo awali alikua asafiri tarehe 28 mwezi januari mwaka 2018 lakini kutokana na taratibu za safari kutokukamili kumepelekea safari hiyo kusogezwa hadi tarehe 4 februari mwaka huu. 



Msanii wa Filamu nchini Bibi. Wastara Issa (wapili kulia waliokaa chini) akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake kuhusu maandalizi ya safari yake ya matibabu kuelekea Mjini Mumbai walipofanya naye mazungumza jana Jijini Dar es Salaam. Watatu kulia waliokaa ni Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu Bibi. Joyce Fissoo

No comments:

Post a Comment