Wednesday, February 28, 2018

KESI YA MATUMIZI MABAYA YA MADARAKA INAYOMKABILI TIDO MHANDO MHANDO KUANZA KUSIKILIZWA MACHI 28

Na Karama Kenyunko, blogu ya jamii

KESI  ya matumizi mabaya ya madaraka inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi mkuu wa zamani wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Tido Mhando kuanza kusikilizwa Machi 28, mwaka huu

Hatua hiyo inakuja baada ya mtuhumiwa huyo leo Februari 28, kusomewa maelezo ya awali (PH), Katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Victoria Nongwa

Kabla ya kusomewa PH, Mhando alikumbushwa mashtaka yake yanayomkabili na Wakili wa Serikali Dismas Mganyizi.Katika maelezo hayo ya awali, Tido amekubali maelezo yake binafsi ya kwamba alikuwa Mkurugenzi  Mkuu wa TBC  mwaka 2006 hadi 2010 na kuwa alikuwa msimamizi katika shughuli za TBC lakini  siyo kwa shughuli zote.

Pia alikubali kutoa maelezo katika Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) lakini hakukiri na kuwa alifikishwa mahakamani Januari 26,mwaka 2018.Aidha Mhando alikana mashtaka yote yanayomkabili na ksi hiyo itaanza kusikilizwa kwa upande wa mashtaka kuketa mashahidi wao Machi 28,mwaka 2018.

Mhando anakabiliwa na mashtaka manne ya kutumia madaraka vibaya na moja la kuisababishia Serikali hasara ya Sh.milioni 887.1.

Inadaiwa kuwa Juni 16,mwaka  2008 akiwa  Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Mhando ambaye alikuwa Mkurugenzi wa TBC, kwa makusudi alitumia madaraka yake vibaya kwa kusaini mkataba wa kuendesha na utangazaji wa vipindi vya televisheni kati ya TBC na Channel 2 Group Corporation (BV1) bila ya kupitisha zabuni, kitu ambacho ni kinyume na Sheria ya Manunuzi na kuinufaisha BVl.

Katika shtaka la pili, Mhando anadaiwa kutumia vibaya madaraka yake Juni 20,mwaka 2008 aliposaini makubaliano kwa utangazaji wa digitali duniani kati ya TBC na BVl.

Katika shtaka la tatu, anadaiwa Agosti 11,mwaka 2008 na Septemba 2008 akiwa Dubai, Mhando alitumia vibaya madaraka yake kusaini mkataba wa makubaliano kwa ununuzi, usambazaji kufunga vifaa vya usambazaji na mnara wa utangazaji kati ya TBC na BVI na kuifaidisha BVI.

Katika shtaka la nne, anadaiwa kuwa  Novemba 16, mwaka 2008 akiwa Dubai, Mhando alitumia vibaya madaraka yake kusaini mkataba wa makubaliano kwa kuendesha miundombinu ya utangazaji (DTT Broadcast Infrastructure) kati ya TBC na BVI na kuinufaisha BVI.

Katika shtaka la mwisho,  anadaiwa kuwa kati ya Juni 16 na Novemba 16,mwaka 2008 akiwa UAE, Mhando aliisababishia TBCli hasara ya Sh.887,122,219.19.

No comments:

Post a Comment