Monday, February 26, 2018

BALOZI SEIF AKUTANA NA KAMISHNA MPYA WA POLISI ZANZIBAR NA BAADAYE AKUTANA NA MABALOZI DR. SLAA NA MBOWETO

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kulia akizungumza na Kamishna Mpya wa Polisi Zanzibar Mohamed Haji Hassan alipofika Ofisini kwake Vuga kujitambulisha rasmi baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo.
Balozi wa Tanzania Nchini Sweeden Dr. Wilbrod Slaa Kushoto akisalimiana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipofika yeye na Mwenzake Balozi Muhidin Ali Mboweto anayekwenda Nigeria walipofika kuaga rasmi. Kati kati yao ni Balozi wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Nchini Nigeria Muhidin Ali Mboweto.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kati kati akizungumza na Balozi wa Tanzania Nchini Nigeria Balozi Muhidin Ali Mboweto Kushoto na Balozi wa Tanzania Nchini Sweeden Dr. Wilbrod Slaa Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Dr. SlaaKulia na Balozi Seif Kulia wakifanyiana mzaha walipokuwa wakikumbushana utumishi wao wakati walipokuwa Wabunge wa Bunge la Jamuhuri ya M,uungano wa Tanzania mara baada ya mazungumzo yao.


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kulipa ushirikiano wa kina Jeshi la Polisi Nchini katika kuona Amani ya Taifa pamona na Raia wake inaendelea kudumu muda wote.

Alisema Zanzibar ina changamoto nyingi zikiwemo za Kisiasa, Dawa za Kulevya na ukosefu wa Maadili unaopelekea kuibuka kwa kasi zaidi ya Udhalilishaji wa Kijinsia ambazo zinahitaji kushughulikiwa ipasavyo ili kuleta ustawi na Utulivu.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar wakati akizungumza na Kamishna Mpya wa Polisi Zanzibar Mohamed Haji Hassan aliyefika kujitambulisha Rasmi baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli hivi karibuni.

Balozi Seif alisema masuala ya udhalilishaji pamoja na Dawa za kulevya hivi sasa yamekithiri na kuleta sura mbaya ndani ya Jamii kiasi cha kulazimika kutungwa sheria ili kujaribu kupambana na kadhia hiyo inayotoa picha mbaya katika uso wa Dunia.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliviagiza vyombo vya Dola kuwasaka na baadae kuwashughulikia ipasavyo wale wote wanaohusika na uingizaji wa Dawa za Kulevya Nchini kwa vile wao ndio chanzo cha balaa zote zinazotokea katika Mitaa mbali mbali Nchini.

Hata hivyo Balozi Seif alikemea tabia ya baadhi ya Maofisa wa Vyombo vya Dola kujaribu kufifilisha kesi za Dawa za kulevya kwa kuwapa afuweni Watuhumiwa huku wakizingatia zaidi kupokea Rushwa badala ya kuwaonea huruma wale wanaoathirika kutokana na wimbi la Dawa hizo.

Alifahamisha kwamba tabia hii hupelekea mwenye hatia kuachwa huru na hatimae kuonekana kudunda Mitaani kifua mbele huku akianza majisifu na kutia hofu Wananchi wanaomuelewa madhambi yake.

Akigusia suala la Kisiasa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimueleza Kamishna Mpya huyo wa Polisi Zanzibar kwamba ni vyema vyombo vya Dola kwa kushirikiana na Wananchi wema wakaelewa kwamba vurugu na Fujo si jambo la kupewa nafasi.

Balozi Seif alisema Zanzibar licha ya kipindi cha Kampeni za Uchaguzi inahitaji kuendelea kubakia kuwa ya amani muda wote ili Raia wake wafanye shughuli zao za kujitafutia riziki bila ya vikwazo vyovyote.

Alimpongeza Kamishna wa Polisi wa Zanzibar kwa wadhifa aliopewa na Taifa ambao anastahiki kuusimamia katika misingi ya Maadili na nidhamu ili lengo la kupewa nafasi hiyo likamilike ipasavyo.

Mapema Kamishna wa Polisi Zanzibar Mohamed Haji Hassan alisema suala la Amani ndio kazi kubwa na ya msingi atakayohakikisha anaisimamia kwa nguvu zake zote kwa kushirikiana na Viongozi na askari wenzake ili kutoa fursa kwa Wananchi waendeshe maisha yao kama kawaida.

Kamishna Mohamed alisema changamoto zilizopo pamoja na udhaifu wa baadhi ya Maafisa na Askari wa Jeshi hilo unaweza kuondoka au kupungua kwa kiasi kikubwa kama nguvu za ushirikiano zitapewa nafasi pana zaidi kwa pande zote husika.

Aliiomba Serikali licha ya uchumi duni lakini bado upo umuhimu wa kufikiria kununua mashine za kisasa za uchunguzi wa Dawa za Kuelevya hasa katika maeneo ya Uwanja wa Ndege na Bandarini.

Kamishna Mohamed alisisitiza kwamba katika jitihada za kukabiliana na wimbi la uingizaji, uuzaji na utumiaji wa Dawa za kulevya ipo haja ya Wananchi kuendelea kulipa ushirikiano wa karibu zaidi Jeshi la Polisi katika mbinu za kuvurugu soko la uuzaji wa Bidhaa hiyo haramu.

Hata hivyo Kamishna Mohamed Haji Hassan alieleza kwamba Viongozi wa Dini bado wana nafasi ya kuwaelimisha Waumini wao hasa Vijana kujiepusha na wimbi hilo la Dawa za Kulevya kwa kutumia Kongamano, semina pamoja na Hotuba.

Alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba makosa mengi yanatokea na kuripotiwa lakini ikichunguza kwa undani inatokana na Watu kukosa Doria za Kiimani.

Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alikutana kwa mazungumzo na Mabalozi Muhidin Ali Mboweto anayeiwakilisha Tanzania Nchini Nigeria na Dr. Wilbrod Slaa anayekwenda Nchini Sweeden walipofika Ofisini kwake kumuaga rasmi wakielekea katika vituo vyao vya kazi walivyopangiwa.

Katika mazungumzo yao Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaeleza Mabalozi hao kwamba nafasi ya Ubalozi ni fursa nzito ya Uwakilishi wa Nchi inayopaswa kutumikiwa kwa uzalendo wa hali ya juu.

Balozi Seif aliwaeleza Mabalozi hao wa Tanzania kwamba Nigeria na Sweeden ni Nchi zenye Historia kubwa ya ushirikiano na Tanzania inayopaswa wasimamizi hao wa Diplomasia kuangalia maeneo ambayo yanaweza kuendelea kudumisha Uhusiano huo.

Alisema zipo sekta ambazo Nigeria na Sweeden zinaweza kuisaidia Zanzibar Kitaaluma akitolea Mfano eneo la Utalii, Umeme Mbadala na hata masuala ya Uhifadhi wa Nyaraka kwa vile Mataifa hayo tayari yameshapiga hatua kubwa Kitaaluma.

Mapema Balozi wa Tananzania Nchini Sweeden Dr. Wilbrod Slaa kwa niaba ya mwenzake Balozi Muhidin Ali Mboweto anayekwenda Nigeria alisema wanajitambua kwamba wao ni Wawakilishi wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

Dr. Slaa alimueleza Balozi Seif kwamba utumishi wao wa Kidiplomasia watauelekeza zaidi katika Diplomasia ya Kiuchumi kama Dunia ilivyobadilika kujikiota zaidi katika eneo hilo.




Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
26/2/2018.

No comments:

Post a Comment