Sunday, January 28, 2018

WAZIRI MKUCHIKA AVUTIWA NA MIRADI YA TASAF



Waziri wa nchi ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Mkuchika akitoka katika jengo la zahanati ya kijiji cha Mwahango katika halmashauri ya wilaya ya Singida lililojengwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF kwa kushirikiana na wananchi wa eneo hilo.
Mwonekano wa jengo la zahanati ya kijiji cha Mwahango katika halmashauri ya wilaya ya Singida iliyojengwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF kwa kushirikiana na wananchi wa eneo hilo ikiwa ni mkakati wa TASAF wa kuboresha huduma za Afya kwa walengwa wake na wananchi wa eneo hilo.
Waziri Mkuchika akipanda mche wa mti katika eneo la Zahanati ya kijiji cha Mwahango katika halmashauri ya wilaya ya Singida iliyojengwa na TASAF na wananchi .
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Mkuchika (aliyesimama mbele ya kamera) akiwahutubia baadhi ya watumishi wa sekretarieti ya mkoa wa Singida wakati alipofanya ziara ya kikazi mkoani humo.
Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Mkuchika akikagua jengo la zahanati ya kijiji cha Mwahango katika wilaya ya Singida jengo lililojengwa na TASAF ikiwa ni mkakati wa kuwasogezea huduma ya Afya wananchi na Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini.


Estom Sanga-Singida

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora mhe. George Mkuchika amepongeza hatua ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF kubuni utaratibu mzuri wa kuwashirikisha wananchi katika ujenzi wa miradi ya maendeleo kwenye maeneo yao.

Mhe. Mkuchika amesema utaratibu huo siyo tu kwamba unapunguza gharama bali unawafanya wananchi kuithamini miradi hiyo na kuitunza kutokana na kutumia nguvu na jasho lao katika kuitekeleza.

Waziri huyo ameyasema hayo mwishoni mwa juma baada ya kutembelea kijiji cha Mwahango katika halmashauri ya wilaya ya Singida ambako alikagua jengo la zahanati lililojengwa na TASAF kwa kuwashirikisha wananchi kijijini hapo.

Aidha Mhe. Mkuchika ameupongeza mkoa wa Singida kwa kusimamia zoezi la uandikishaji Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kwa uaminifu na hivyo kupunguza kwa kiwango kikubwa idadi ya Watu wasiostahili kujumuishwa kwenye Mpango huo kinyume cha utaratibu.

Akiwa kijijini hapo Waziri Mkuchika alipata ushuhuda wa mafanikio waliyoyapata baadhi ya Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya masikini ambao wameweza kuboresha maisha yao katika nyanja za makazi, lishe,uanzishaji wa miradi ya kiuchumi ,kusomesha watoto na kujiunga na mfuko wa bima ya afya ya jamii na hivyo kupata huduma ya matibabu katika kipindi chote cha mwaka.

Taarifa ya utekelezaji wa shughuli za TASAF mkoani Singida imeonyesha kuwa, mafanikio makubwa yamepatikana tangu kuanza utekelezaji wa Mpango wa kunusuru kaya maskini mkoani humo hususani katika kuamsha ari ya wananchi kuuchukia umaskini kwa vitendo.

Hata hivyo taarifa hiyo imeiomba serikali kupitia TASAF kukamilisha zoezi la kuvijumuisha vijiji vingine ambavyo wananchi wao hawakupata fursa ya kunufaika na huduma za Mpango katika awamu ya kwanza ya utambuzi iliyofanyika mkoani humo mwaka 2014.

Waziri Mkuchika amesema serikali inalifanyia kazi suala hilo kwa juhudi zaidi kwani utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya maskini umefanyika kwa asilimia 70 tu kutokana na ufinyu wa fedha ,hata hivyo kutokana na Mpango huo kuwagusa wananchi wanaokabiliwa na umaskini moja kwa moja, utaratibu mzuri unaaandaliwa ili wananchi wote wanaostahili kujumuishwa kwenye Mpango waweze kutambuliwa hususani katika vijiji ambavyo havinufaiki na Mpango huo kwa sasa.

No comments:

Post a Comment