Monday, January 29, 2018

SHUGHULI ZA KIBINADAMU ZAATHIRI UZALISHAJI UMEME NYUMBA YA MUNGU


Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili katika Kituo cha kuzalisha umeme cha Nyumba ya Mungu kilichopo Mkoani Kilimanjaro. Anayeshuhudia ni Mtumishi kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO)
Kaimu Meneja wa Kituo cha Nyumba ya Mungu TANESCO, Clarance Mahunda akitoa maelezo kuhusu utendaji wa kituo hicho kwa Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (wa pili kulia). Wengine katika picha ni Wafanyakazi wa Wizara ya Nishati Makao Makuu na wa Mkoa wa Kilimanjaro.
Kaimu Meneja wa Kituo cha Nyumba ya Mungu TANESCO, Clarance Mahunda akimweleza jambo Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (katikati). Wengine katika picha ni Watumishi wa Wizara ya Nishati na kutoka Mkoa wa Kilimanjaro.
Kaimu Meneja wa Kituo cha Nyumba ya Mungu TANESCO, Clarance Mahunda (katikati) akitoa maelezo kuhusu Bwawa la maji linalotumika kuhifadhia maji katika Kituo cha Nyumba ya Mungu. Kushoto ni Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu na kulia ni Katibu wa Naibu Waziri, Ngerenja Mgejwa.




Na Rhoda James, Kilimanjaro

Imeelezwa kuwa, shughuli za Kibinadamu zinazofanywa kuzunguka Kituo cha Kuzalisha Umeme cha Nyumba ya Mungu zimeendelea kuathiri uzalishaji wa nishati hiyo kutokana na kukosekana maji ya kutosha.

Hayo yalielezwa na Kaimu Meneja wa Kituo Clarance Mahunda wakati Waziri wa Nishati, Subira Mgalu alipofanya ziara Kituoni hapo mwishoni mwa wiki na kueleza kuwa, hivi sasa kituo hicho kinazalisha megawati 3.5 hadi 4 tofauti na uwezo wake wa kuzalisha megawati 8 kwa saa 24.“Shughuli za binadamu zikiwemo kulima, kuchunga ngo’mbe na uvuvi kumepelekea uzalishaji wa umeme katika kituo hiki kuwa hafifu, kitu ambacho kinasababisha ukosefu wa maji ya kutosha hivyo kuzalisha umeme pungufu,” alisema Mahunda.

Pia, Mahunda alimweleza Naibu Waziri wa Nishati kuwa, japokuwa zipo juhudi mbalimbali zambazo zimefanyika kuzuia athari hizo ikiwemo kushirikisha wadau mbalimbali kama Pangani Water Basin pamoja na taasisi mbalimbali za Serikali, lakini baado kituo hicho kinazalisha megawati 3.5 hadi 4. 

Aidha, Mahunda alieleza kuhusu utendaji wa Kituo hicho na kusema kuwa ni mzuri kutokana na kufanyika ukarabati mkubwa uliofanyika mwezi Oktoba na Novemba,2017 na hivyo kupelekea mashine zote kufanya kazi ipasavyo.Pia aliongeza kuwa, kwa sasa kituo hicho kinasafirisha umeme kwa njia mbili za Msongo wa Kilovoti 66 kuelekea Kiungi na njia nyingine ni Umeme kusafirishwa kwa Msongo wa Kilovoti 33 kupitia Mwanga na Mkuyuni.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati alizitaka Mamlaka kuanzia Serikali za Mtaa hadi Mkoa na wananchi wanaozunguka maeneo ya kituo hicho kuhakikisha wanatunza mazingira yanayozunguka kituo hicho kwa kulinda vyazo vya maji ili kupata maji ya kutosha wakizingatia umuhimu wa nishati ya umeme kwa maendeleo ya watu na Taifa.

“Nimeelezwa kuwa kina cha maji hakiruhusu mashine zote kuzalisha umeme, na hii ni kwa sababu ya shughuli za binadamu ambazo zinaendelea pembezoni mwa Bwawa la maji yanayotumika kuzalisha umeme huo,”aliongeza Mgalu.Mgalu aliongeza tatizo la shughuli za kibinadamu limeviathiri pia vituo vingine za kuzalishia umeme vya Hale na Pangani na hivyo kupelekea upungufu katika kuzalisha umeme kutokana na kina cha maji kupungua.

Aidha, Mgalu aliitaka TANESCO pamoja na Serikali za Mitaa kuendelea kuwaelimisha wananchi wanaozunguka maeneo hayo ili kuwezesha kituo husika kuzalisha umeme kwa viwango vinavyo takiwa.

No comments:

Post a Comment