Wednesday, January 31, 2018

RAIS DKT MAGUFULI AZINDUA UHAMIAJI MTANDAO NA PASIPOTI MPYA YA TANZANIA YA KIELEKTRONIKIA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 31 Januari, 2018 amezindua mfumo wa uhamiaji mtandao (e-Immigration) ambao utasaidia kuimarisha ulinzi na usalama wa mipaka ya nchi, kudhibiti ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali na kuimarisha utoaji wa huduma za kiuhamiaji kwa raia wa Tanzania na wageni wanaoingia na kuishi hapa nchini kwa madhumuni mbalimbali.
Uzinduzi wa mfumo huo umefanyika katika ofisi kuu ya uhamiaji Jijini                 Dar es salaam na kuhudhuriwa na Mke wa Rais Mhe. Mama Janeth Magufuli, Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti     wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Seif Ali Iddi, na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa.
Wengine ni Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Jaji Mkuu    wa Zanzibar Mhe. Omar Othman Makungu, Spika wa Baraza la Wawakilishi     Mhe. Zubeir Ali Maulid, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano             wa Tanzania Mhe. Dkt. Tulia Ackson Mwansasu, Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili Mhe. Dkt. Ali Hassan Mwinyi na Rais Mstaafu wa Zanzibar Mhe. Amani Abeid Karume.
Kabla ya kuzindua mfumo wa uhamiaji mtandao Mhe. Rais Magufuli amekagua teknolojia iliyotumika katika mfumo huo ikiwa ni pamoja na kuchukuliwa alama za vidole na baadaye kupatiwa pasipoti mpya ya kielektronikia (e-Passport) ambayo pia imeanza kutolewa leo.
Pasipoti mpya za kielektronikia pia zimetolewa kwa viongozi wengine wakuu         wa Serikali, Bunge na Mahakama wa Tanzania Bara na Zanzibar, waliohudhuria uzinduzi huo.
Mhe. Rais Magufuli amempongeza Waziri wa Mambo ya ndani ya nchi              Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba na Idara ya Uhamiaji kwa kufanikisha mradi wa kuweka mfumo wa uhamiaji mtandao na kuanza kutoa pasipoti mpya                ya kielektronikia kwa gharama nafuu ya Shilingi Bilioni 127.2 ikilinganishwa           na makadirio yaliyowekwa awali ya Shilingi Bilioni 400.
“Hapa tumeokoa fedha nyingi za Watanzania, kuna watu walikuwa wamejiandaa kutupiga na kuchukua hizo Shilingi Bilioni 400, lakini tukatumia vyombo vyetu mbalimbali, tukafanya uchunguzi                na tumefanikiwa kutekeleza mradi huu kwa gharama nafuu” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Aidha, kwa kutambua kazi nzuri inayofanywa na idara ya uhamiaji baada                ya kupokea maelekezo yake ya kutakiwa kufanya mabadiliko makubwa, Mhe. Rais Magufuli ameahidi kutoa Shilingi Bilioni 10 kwa ajili ya kujenga ofisi ya makao makuu ya idara hiyo Mjini Dodoma.
“Kamishna Jenerali Dkt. Anna Makakala na timu yako mnafanya kazi nzuri, ndio maana nimewanunulia nyumba 103 kwa ajili ya wafanyakazi kule Dodoma na leo nitawapa fedha nyingine Shilingi Bilioni 10 mkajenge ofisi nzuri ya makao makuu, nyinyi endeleeni kuchapa kazi, endeleeni kukamata wahamiaji haramu na endeleeni kukusanya mapato vizuri” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mapema akitoa taarifa ya mfumo wa uhamiaji mtandao, Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Peter Makakala amesema mfumo huo ni muunganiko wa mifumo mbalimbali ambayo imesanifiwa kufanya kazi kwa pamoja, kutoa taarifa kwa watumiaji na wadau wa huduma za kiuhamiaji na kwamba kupitia mfumo huo idara ya uhamiaji inatarajia kutoa pasipoti za kielektronikia (e-Passport), viza           za kielektronikia (e-Visa), vibali vya ukaazi vya kielektronikia (e-Permit) na udhibiti wa mipaka wa kielektronikia (e-Border Management) kwa awamu nne hadi ifikapo mwisho wa mwaka huu 2018, pamoja na kutoa pasipoti ya kielektronikia ya Afrika Mashariki ya Tanzania.
Balozi wa Ireland hapa nchini Mhe. Paul Sherlock ameipongeza Tanzania kwa kufanikisha mradi huu na kueleza kuwa mfumo huu wa uhamiaji mtandao ni alama muhimu ya Taifa.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
31 Januari, 2018



















































1 comment:

  1. The global outbreak of Coronavirus has put many countries in lockdown, despite the situation our QuickBooks experts continue to address the QuickBooks issues & query. Need to contact QuickBooks Toll Free Phone Number for resolution of troubles.

    ReplyDelete