Monday, January 8, 2018

NIDHAMU YA KUAHIDI NA KUTEKELEZA, MATUMIZI SAHIHI VYAONGEZA KASI YA UTEKELEZAJI MIRADI

Mkurugenzi wa Idara ya habari Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbas akizungumza na vyombo mbalimbali vya habari kwenye ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo wakati alipotoa taarifa ya utekelezaji wa miradi mbalimbali inayotekelezwa na serikali ya awamu ya Tano chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania Rais Dkt. John Pombe Magufuli na kutolea ufafanuzi wa masuala kadhaa, Pichani kushoto  Mkurugenzi Msaidizi upande wa usajiri wa Magazeti Ndugu Patric Kipangula  na Kulia Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Habari Maelezo, Rodney Thadeus 
Mkurugenzi wa Idara ya habari Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbas akifafanua jambo kwa Waandishi wa habari mapema leo katika ukumbi wa Idara ya Habari MAELEZO,alipokuwa akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi mbalimbali inayotekelezwa na serikali ya awamu ya Tano chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania,Dkt. John Pombe Magufuli. Pichani kushoto ni  Mkurugenzi Msaidizi upande wa usajiri wa Magazeti Ndugu Patric Kipangula  na Kulia Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Habari Maelezo, Rodney Thadeus .PICHA NA MICHUZI JR


NIDHAMU mpya katika ukusanyaji na matumizi ya fedha za umma na dhamira ya dhati ya kutekeleza ahadi kubwa kwa faida ya wananchi vimesaidia Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuendelea kutekeleza kwa mafanikio miradi mbalimbali mikubwa ya kitaifa. Baadhi ya mambo yaliyotekelezwa na kufafanuliwa leo kwa wanahabari ni kama ifuatavyo: 

Hali ya Uchumi

Kama alivyoeleza Dkt. Philip Isdor Mpango, Waziri wa Fedha na Mipango siku chache zilizopita, tunawahakikishia watanzania kuwa hali ya uchumi wa nchi yetu inaendelea kuwa imara kwa kiasi cha kuziridhisha taasisi mbalimbali za kimataifa.

Ripoti za Shirika la Fedha Duniani (IMF), Benki ya Dunia (WB) na Taasisi ya Goldman Sachs ya Marekani zimetabiri kuwa wakati uchumi wa dunia utakua kwa wastani wa asilimia 3.0 hadi 4.0, ukuaji wa uchumi wa Tanzania unatajwa kuendelea kuwa kati ya nchi tano bora za Afrika ukitarajiwa kukua kwa asilimia 6.5 hadi 7.0 katika mwaka 2018.

Ahadi ya Kuhamia Dodoma

Serikali ya Awamu ya Tano imeendelea kuonesha nidhamu ya kuahidi na kutekeleza ahadi ya kuhamia makao makuu, Dodoma. Kufikia mwishoni mwa Desemba, 2017, viongozi waandamizi wa Serikali wameshahamia Dodoma. Rais mwenyewe akitarajiwa mwaka huu.

Mbali na viongozi, jumla ya wafanyakazi 3,671 kutoka wizara na taasisi mbalimbali za umma wameshahamia makao makuu Dodoma. Awamu inayofuata baadaye mwaka huu itahusisha wafanyakazi wengine 2,460. Sekta binafsi ichangamkie fursa za Dodoma.

Viwanda Vyashamirisha Uchumi Mpya 

Moja ya ajenda kuu za Serikali ya Awamu ya Tano ni kujenga uchumi mpya wa viwanda. Kufikia mwaka jana viwanda zaidi ya 3,300 vilisajiliwa kupitia Msajili wa Makampuni (250), Kituo cha Uwekezaji (361), Mamlaka ya Usimamizi wa Maeneo Maalum ya Kiuchumi (41) na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO lililosajili viwanda vidogo vya kati ya mtu mmoja hadi 9 takribani 2,721). Ujenzi na uzalishaji katika viwanda hivi uko katika hatua mbalimbali.

Kati ya miradi hiyo iliyosajiliwa, viwanda vikubwa ni 652. Viwanda hivi vina jumla ya mtaji wa zaidi ya TZS trilioni 5 utakaowekezwa nchini na vitaajiri watu 50,625. Katika taarifa ya mwezi ujao tutaainisha baadhi ya viwanda vilivyokamilika na uzalishaji unavyoendelea.

Miradi Mikubwa ya Umeme

Katika sekta ya nishati, Serikali inaendelea kutekeleza miradi zaidi ya 20 ya kuhakikisha nchi ina umeme wa uhakika. Miongoni mwa miradi ya kimageuzi ni usimikaji wa mitambo ya umeme wa gesi Kinyerezi I (mtambo wa nyongeza wa megawati 185) na Kinyerezi II wa megawati 240. Mitambo hii kwa pamoja itaongeza megawati 425.

Mtambo wa Kinyerezi 1-nyongeza umefikia asilimia 50. Mtambo wa Kinyerezi II umekamilika kwa asilimia 87 ambapo Desemba, 2017, mtambo huo wa kisasa umeingiza megawati 55.94 katika gridi ya Taifa. Kiasi kingine cha megawati 27.94 kinatarajiwa kuingia kwenye gridi mwezi huu. Mitambo yote miwili itakamilika mwaka huu. 

Ujenzi Reli ya Kisasa “Standard Gauge”

Aidha, Serikali imeendelea kutekeleza mradi wa kihistoria wa ujenzi wa reli ya kisasa kwa kiwango cha kimataifa (Standard Gauge) kwa kuanzia na kipande cha kilometa 300 (Dar-Moro) kitakachogharimu TZS trilioni 2.7.

Kazi ya kusanifu njia yote itakayopita reli imeshakamilika na kwa sasa uandaaji wa tuta, ujenzi wa madaraja kabla ya kutandika reli yenyewe umeanza kwa kasi. Aidha, ujenzi wa kipande cha pili cha kilometa 442 (Morogoro-Makutupora, Dodoma) kitakachogharimu TZS TZS trilioni 4.3, mkandarasi ameshaanza maandalizi.

Ununuzi Mabehewa, Vichwa Waanza

Wakati ujenzi wa reli ukiendelea, Serikali kupitia Kampuni Hodhi ya Raslimali za Reli (RAHCO) imeshatangaza zabuni kwa ajili ya kupata makampuni yatakayotengeneza vichwa na mabehewa ya kisasa ya treni ya umeme na mafuta. Zabuni zitafunguliwa mwezi huu.

Katika zabuni hiyo Serikali inatarajia kununua vichwa 25 (23 vya umeme na 2 vya dizeli), mitambo 25 ya ukarabati wa reli na mabehewa 1,590 (kati ya hayo 1,530 yakiwa ni ya aina mbalimbali za mizigo kama vile kubeba makontena, nafaka, mafuta n.k), mabehewa 60 ni ya abiria (15 yakiwa ni daraja la kwanza na 45 daraja la kawaida).

Meli Mpya Zaleta Matumaini Maziwa Makuu 

Serikali iliahidi na sasa inatekeleza. Katika Ziwa Nyasa mwishoni mwa wiki iliyopita meli mbili mpya za mizigo za MV Njombe na MV Ruvuma zinazobeba mizigo tani 1,000 kila moja zimeanza safari kwenda bandari mbalimbali zikiwemo za nchi jirani. Serikali imetumia TZS Bilioni 11.252 na meli nyingine mpya ya abiria itakamilika Juni mwaka huu.

Katika Ziwa Victoria, kupitia kampuni ya Serikali ya Huduma za Usafiri Katika Maziwa, Marine Services Company LTD, mkandarasi wa kutengeneza meli mbili kubwa, mpya na za kisasa ameshapatikana. Aidha, tayari meli ya abiria ya MV Clarios na ya mizigo MV Umoja zilizofanyiwa ukarabati na kuwa za kisasa zimeshaanza kazi.

Katika taarifa zijazo tutaendelea kutoa maendeleo ya miradi hii mikubwa na kuainisha utekelezaji katika sekta na miradi mingine kwa wananchi. Kwa maelezo zaidi kuhusu taarifa ya leo ikiwemo picha za miradi zinazoambatana na taarifa hii tafadhali tembelea:

Twitter: TZ_Msemaji Mkuu

Imetolewa na:
Dkt. Hassan Abbasi,

Mkurugenzi, Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali.

No comments:

Post a Comment