Wednesday, January 31, 2018

MENGI AIPA TWCC JENGO LAKE KUENDELEZA UJASIRIAMALI

Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF) Dk Reginald Mengi, ambaye pia ni Mwenyekiti Mtendaji wa IPP LTD, amekipatia Chama cha Wafanyabiashara Wanawake Tanzania ( TWCC) jengo la maonyesho la IPP Ltd lililopo ndani ya viwanja vya maonyesho ya kimataifa ya Biashara jijini Dar es salaam, ili liwasaidie wanachama wa TWCC kuendeleza ujasiriamali.

Jengo hilo pamoja na kuendeleza ujasiriamali litakuwa eneo la maonesho na kufunzia na Dk Mengi amesema amelitoa ili kuunga mkono juhudi za serikali za kuwawezesha wanawake kiuchumi. Maamuzi ya kutoa jengo hilo yalifuatana na ombi lililotolewa na Mwenyekiti wa TWCC Jacqueline Maleko aliyetaka jengo hilo kupewa wanawake ili kuwaendeleza kiuchumi na kimafunzo.

 Akizungumza wakati wa kufungua Mkutano Mkuu wa mwaka wa Chama cha Wafanyabiashara Wanawake Tanzania (Tanzania Women Chamber of Commerce-TWCC), Dk Mengi aliwataka wanawake kuwa macho na kutumia fursa zilizopo kujiwezesha kiuchumi. 
Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini TPSF Dr. Reginald Mengi akifurahi jambo na Mwakilishi wa TRA, Rose Mahendeke (kushoto), Mkurugenzi Mtendaji wa Chemba ya Wajasiriamali Wanawake nchini TWCC, Bi. Noreen Mawalla (wa pili kushoto), Mwenyekiti wa Chemba ya Wajasiriamali Wanawake nchini (TWCC), Bi. Jaqueline Mneney Maleko (kulia) mara baada ya kuwasili kwenye ukumbi wa mikutano wa Benki Kuu kufungua Mkutano Mkuu wa mwaka wa Chama cha Wafanyabiashara Wanawake Tanzania – Tanzania Women Chamber of Commerce (TWCC) uliofanyika jana jijini Dar es Salaam.

Aliwataka wanawake kuthubutu na kuwa wajasiri katika kuangalia na kuzitumia fursa zilizopo sasa nchini badala ya kuzipita bila kuziona. Aidha Dk Mengi aliwataka wanawake wajiamini na kujihakikishia kwamba wanaweza kujiletea maendeleo, wawe wanyenyekevu katika biashara zao, na wawe na ndoto kubwa ya maendeleo huku wakianza kidogo kidogo badala ya kusubiri mtaji mkubwa. 

Katrika mkutano huo Dk Mengi alitoa ushuhuda wa jinsi yeye alivyoanza biashara zake na kusema alitumia fursa alizoziona kutengeneza dawa ya kung’arisha viatu baada ya kuchukua mkaa Kariakoo na kuusaga na kuchanganya na mafuta. Alisema alitengeneza dawa iliyoitwa ‘Sunshine’ na alivuna mapesa.
 Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF) Dr. Reginald Mengi, ambaye pia ni Mwenyekiti Mtendaji wa IPP LTD akizungumza wakati akifungua Mkutano Mkuu wa mwaka wa Chama cha Wafanyabiashara Wanawake Tanzania – Tanzania Women Chamber of Commerce (TWCC) unaondelea katika ukumbi wa mikutano wa Benki Kuu jijini Dar es Salaam.


Aidha alisema kwamba alianzia kutengeneza kalamu ndani ya sebule kabla hajaondoka na kutumia maeneo ya nje kutengeneza kalamu na kasha kuwa na kiwanda kikubwa. Alisema yeye alizaliwa katika umaskini akiishi katika nyumba ya msonge pamoja na wanyama na kuamua kuukataa umaskini. Alisema kilichomsaidia yeye ni kuwa na macho yanayoona Fursa na kuitumia vilivyo kwa kujiamini na kuthubutu. 

Alisema Mungu aliumba kila mtu kuwa namba Moja na ni vyema watu wote wakajiona kuwa namba moja na katika hilo kuthubutu huku wakihakikisha kwamba wanatumia vyema teknolojia iliyopo kwa kufanya matangazo ya biashara zao. Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wafanyabiashara Wanawake Tanzania TWCC, Bi. Noreen Mawalla akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara wanawake Tanzania TWCC Jacqueline Meney Maleko (hayupo pichani) kutoa neno la ukaribisho kwa mgeni rasmi na wanachama wa TWCC wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa mwaka wa TWCC uliofunguliwa jana jijini Dar es Salaam.

Aliwataka kutumia simu zao kuhakikisha kwamba wanauza na kuzitangaza bidhaa zao huku akiwataka wakue na kuacha kuogopa kuanzisha viwanda. Pia aliwataka kuwa wanyenyekevu katika biashara zao kwani ndio namna bora ya kuendeleza urafiki wa kibiashara kati yao na wadau wanaohitaji huduma au bidhaa zao. 

Alisisitiza utoaji wa bidhaa bora hata kama bidhaa hizo zimelenga kuwasaidia watu maskini na kuwataka kila senti wanayoipata katika biashara kuhakikisha inabaki hukohuko na isichanganywe na matumizi binafsi. Mapema akimkaribisha mgeni rasmi kwenye mkutano huo, Mwenyekiti TWCC, Jacquiline Maleko alipendekeza Chama chake kiwe na ushirikiano na uwakilishi mkubwa kwenye taasisi muhimu za biashara na kuyataka makampuni binafsi nchini yawe yananunua bidhaa za wanachama wao kabla ya kupendelea bidhaa za nje.  Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara wanawake Tanzania (TWCC), Bi. Jacqueline Mneney Maleko akizungumza machache kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi Dr. Reginald Mengi kufungua mkutano mkuu wa mwaka wa TWCC unaoendelea katika ukumbi wa mikutano wa Benki Kuu jijini Dar es Salaam.

Maleko pamoja na kumuomba Dk Mengi, kuipatia TWCC jengo lililopo Sabasaba pia aliitaka TPSF (sekta Binafsi) kuhakikisha kwamba inawazungumzia wanawake na kuwapa nafasi katika vikao vya maamuzi. Pia alifafanua kwamba chama hicho kinataka kushirikishwa katika baraza la biashara la kitaifa na mikoani kwa lengo la kutetea wanawake ambao asilimia 50 ya wafanyabiashara nchini ni wao. 

Maleko alisema chama hicho kilichoundwa mwaka 2005 na kwa sasa kikiwa na majukwaa 11 pote nchini, kimelenga kuunganisha nguvu za wanawake katika kuhakikisha wanashika uchumi kwa kutumia fursa zilizopo za nafasi mbalimbali za wanawake zilizowezeshwa kitaratibu, kama asilimia 5 ya mapato ya halamashauri kusaidia makundi maalumu na asilimia 30 ya zabuni ya manunuzi ya serikali kupewa makundi maalumu. Mkurugenzi wa Huduma za Uanachama wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF), Louis Accaro akifafanua jambo wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa mwaka wa Chama cha Wafanyabiashara Wanawake Tanzania – Tanzania Women Chamber of commerce (TWCC) unaondelea katika ukumbi wa mikutano jijini Dar es Salaam.

Alishauri asilimia hiyo tano kukopeshwa SACCOS yao wanawake ili waweze kukopa na kuendeshea biashara zao, akiamini kwamba fedha hizo zikifikishwa zitawatoa wanawake kiuchumi. Alisema kwa sasa wanawake wafanyabiashara wamekuwa wakikabiliwa na matatizo ya mila, desturi na taratibu za kisheria na hivyo wao ni kazi yao kuhakikisha kwamba sauti ya mwanamke inafika kila mahali ili mazingira ya biashara yaboreshwe. 

Maleko pia alisema kama serikali inaweza kutoa ruzuku kwa vyama vya siasa kwanini na wao wasipewe ruzuku hiyo ili waweze kuinua uchumi wa taifa. Pia waliomba nafasi katika maeneo ya Taasisi ya viwanda vidogo SIDO kutumiwa na wanawake kuanzisha viwanda vya kusindika vyakula ambapo pia wanaweza kufundishwa na watalamuwa SIDO wakiwa palepale. Meneja mikopo ya wanawake na uwezeshaji wanawake wa benki ya CRDB nchini, Rehema Shambwe akitoa salamu za benki hiyo kwa wajumbe wa TWCC wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa mwaka wa Chama cha Wafanyabiashara Wanawake Tanzania – Tanzania Women Chamber of Commerce (TWCC) unaoendelea katika ukumbi wa mikutano wa Benki Kuu jijini Dar es Salaam.


Mkutano huo wa mwaka ulifadhiliwa na Mamlaka ya Kodi na Mapato TRA, uilikuwa na wageni wengi wakiwemo watu wa CRDB ambao wanampango wa kuanzisha kituo cha kusaidia wanawake katika masuala ya biashara na ujasiriamali na Trade Mark ambao tayari wanaushirikiano na TWCC. 

Akizungumza katika mkutano huo Mkurugenzi Mkazi wa Taasisi ya Trade Mark East Africa Dr John Ulanga alisema Asasi yake ipo katika hatua za mwisho za kuingia mkataba mpya wa miaka 5 wenye thamani ya shilingi bilioni mbili na Chama hicho, baada wa ule wa mwanzo wa shilingi milioni 650 kuhitimishwa. Mkataba huo wa mwanzo ulishughulika na mafunzo kwa wajasiriamali katika nyanza zote kuanzia uzalishaji na ufungashaji na matumizi ya hati mbalimbali zinazogusa ujasiriamali.  Mwakilishi wa TRA ambao ndio wamefanikisha kufanyika kwa mkutano huo, Bi. Rose Mahendeke aktioa salamu za TRA kwa wajumbe wa TWCC walioshiriki ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa mwaka wa Chama cha Wafanyabiashara Wanawake Tanzania – Tanzania Women Chamber of Commerce (TWCC) unaoendelea katika ukumbi wa mikutano wa Benki kuu jijini Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkazi wa Taasisi ya Trade Mark East Africa Dr John Ulanga akitangaza kuhusiana na hatua za mwisho za kuingia mkataba mpya wa miaka 5 wa thamani ya shilingi bilioni mbili na TWCC, baada wa ule wa mwanzo wa shilingi milioni 650 kuhitimishwa wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa mwaka wa Chama cha Wafanyabiashara Wanawake Tanzania – Tanzania Women Chamber of Commerce (TWCC) unaoendelea katika ukumbi wa mikutano wa BOT jijini Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara wanawake Tanzania (TWCC), Bi. Jacqueline Mneney Maleko akishuhudia Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini TPSF Dr Reginald Mengi, ambaye pia ni Mwenyekiti Mtendaji wa IPP LTD akiweka kwa maandishi kukabidhi jengo la maonyesho la IPP ltd lililopo ndani ya viwanja vya maonyesho ya kimataifa ya Biashara jijini Dar es salaam, ili liwasaidie wanachama wa TWCC kuendeleza ujasiriamali. Kulia ni Mkurugenzi Mkazi wa Taasisi ya Trade Mark East Africa Dr John Ulanga. Picha juu na chini ni wajumbe wa TWCC wanaoshiriki mkutano mkuu wa mwaka unaoendelea katika ukumbi wa mikutano wa BOT jijini Dar es Salaam.   Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF) Dr. Reginald Mengi, ambaye pia ni Mwenyekiti Mtendaji wa IPP LTD akimkabidhi Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara wanawake Tanzania (TWCC), Bi. Jacqueline Mneney Maleko (katikati) kibali cha jengo la maonyesho la IPP ltd lililopo ndani ya viwanja vya maonyesho ya kimataifa ya Biashara jijini Dar es salaam, ili liwasaidie wanachama wake kuendeleza ujasiriamali. Kulia Mkurugenzi Mkazi wa Taasisi ya Trade Mark East Africa Dr John Ulanga. Picha juu na chini ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini TPSF Dr Reginald Mengi, ambaye pia ni Mwenyekiti Mtendaji wa IPP LTD akisalimiana na wajumbe wa TWCC walioshiriki ufunguzi wa Mkutano mkuu wa mwaka unaoendelea katika ukumbi wa mikutano BOT jijini Dar es Salaam. Mgeni rasmi Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini TPSF Dr Reginald Mengi, ambaye pia ni Mwenyekiti Mtendaji wa IPP LTD katika picha ya pamoja na wajumbe wa TWCC wanaoshiriki mkutano mkuu wa mwaka unaoendelea katika ukumbi wa mikutano BOT jijini Dar es Saalaam Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini TPSF Dr Reginald Mengi, ambaye pia ni Mwenyekiti Mtendaji wa IPP LTD akipokea zawadi kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa TWCC, Bi. Noreen Mawalla.

No comments:

Post a Comment