Sunday, January 28, 2018

CHUO CHA KODI KUWAJENGEA UWEZO MAWAKALA WA FORODHA ZANZIBAR

Mkuu wa Chuo cha Kodi Prof. Isaya Jairo (Kulia) pamoja na Mwenyekiti wa Chama cha Mawakala wa Forodha Zanzibar (ZFB) Omar Hussein Mussa wakibadilishana hati za makubaliano ya ushirikiano katika kuwajengea uwezo wanachama wa ZFB.

Mkuu wa Chuo cha Kodi Prof. Isaya Jairo (Kulia) pamoja na Mwenyekiti wa Chama cha Mawakala wa Forodha Zanzibar Omar Hussein Mussa wakizungumza na wajumbe wa Kamati ya Makubaliano kutoka Chuo cha Kodi (Kulia) na Zanzibar (kushoto) kabla ya kusaini hati za makubaliano katika chumba cha mikutano ITA.


Mkuu wa Chuo cha Kodi Prof. Isaya Jairo (wa pili kushoto), Mwenyekiti wa Chama cha Mawakala wa Forodha Zanzibar (ZFB) Omar Hussein Mussa (wa pili Kulia) pamoja na Mwenyekiti wa Chama cha Mawakala Tanzania (TAFFA) Stephen Ngatunga (wa kwanza kulia) katika picha ya pamoja na wajumbe wa kamati ya ushirikiano mara baada ya kusaini makubaliano ya kuwajengea uwezo mawakala wa Forodha Zanzibar. (PICHA ZOTE NA OLIVER NJUNWA).

…………………………………………………………………………………..

Na Oliver Njunwa- Dar es Salaam

Chuo cha Kodi (ITA) pamoja na Chama cha Mawakala wa Forodha Zanzibar (ZFB), vimeingia katika makubaliano ya kushirikiana katika kuwajengea uwezo Mawakala wa Forodha Zanzibar.

Akizungumza mara baada ya hafla fupi ya kutiliana saini makubaliano hayo, iliyofanyika hivi karibuni katika Chuo cha Kodi jijini Dar es salaam, Mkuu wa Chuo hicho Prof. Isaya Jairo amesema kwamba, makubaliano hayo ni muhimu kwani kila upande una watalaam wa kutosha kuwasaidia Mawakala wa Forodha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

“ITA inajivunia utaalam wake wa kufundisha na ZFB ina utaalamu katika masuala ya kiforodha. Kwa hiyo wote kwa pamoja tutashirikiana ili malengo ya makubaliano haya yaweze kufikiwa”, alisema Prof. Jairo.

Prof. Jairo aliongeza kuwa, katika makubaliano hayo, Chuo cha Kodi kitatoa mafunzo ya muda mfupi na utaalamu wa masuala ya forodha kwa ZFB ili kuhakikisha kuwa kunakuwa na Mawakala wa Forodha wanaofanya kazi kwa weledi.

Mkuu wa Chuo cha Kodi pia amesema kwamba lengo la vyuo sio kupata fedha bali kutoa wataalamu wa kutosha ambapo uwezo wa Chuo hupimwa kwa idadi ya wanafunzi wanaohitimu na aina ya sifa walizonazo.

Aidha, Prof. Jairo ameiomba ZFB kulinda hadhi ya jina la Chuo cha Kodi kwani kina jina zuri kutokana na uzoefu wake wa kutekeleza makubaliano ya ushirikiano na taasisi mbalimbali ndani na nje ya nchi.

“ITA ina makubaliano na Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania (TAFFA) pamoja na Bodi ya Mapato ya Zanzibar (ZRB) na kwa nchi za nje ina makubaliano na Malawi, Zambia, Botswana na iliisadia Sudan Kusini kuanzisha Mamlaka ya Mapato nchini humo”, alisema Prof. Jairo.

Makubaliano hayo yamefanyika katika Chuo cha Kodi Dar es salaam Ijumaa tarehe 26 Januari 2017 na kutiwa saini kati ya Mkuu wa Chuo cha Kodi Prof. Isaya Jairo na Mwenyekiti wa Chama cha Mawakala wa Forodha Zanzibar Omar Hussein Mussa na kushuhudiwa na Rais wa Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania (TAFFA) Stephen Ngatunga.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Mawakala wa Forodha Zanzibar ZFB, Omar Hussein Mussa amesema kwamba makubaliano hayo ni msingi mzuri wa kupata Mawakala wa Forodha wenye weledi na hivyo kupunguza changamoto zinazojitokeza katika tasnia ya uwakala wa forodha.

“Makubaliano haya ni jambo jema na yatakuwa endelevu kwa kuwa sisi tuko tayari kuhakikisha yanaleta mabadiliko katika utendaji wa mawakala wetu wa Forodha”, alisema Bw. Mussa.

Kwa upande wake Rais wa Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania Stephen Ngatunga ambaye alihudhuria hafla hiyo, amekipongeza Chuo cha Kodi pamoja na ZFB kwa makubaliano hayo muhimu na kusema kwamba anafarijika kuona jitihada zake zimefanikiwa kwani yeye alichangia kufanikisha suala hilo.

Katika makubaliano hayo, Chuo cha Kodi kitasimamia kiwango cha taaluma itakayotolewa kwa kuzingatia vigezo vya Baraza la Taifa la Mafunzo ya Ufundi (NACTE) na Tume ya Vyuo Vikuu (TCU). Aidha, Chuo hicho pia kitasimamia udahili, mitihani, kutoa walimu na vyeti baada ya kuhitimu wakati Chama cha Mawakala wa Forodha Zanzibar kitapokea ada, kutoa wanafunzi, madarasa pamoja na vitendea kazi.

Chuo cha Kodi ni sehemu ya Mamlaka ya Mapato Tanzania ambacho kilipata ithbati kutoka Baraza la Taifa la Mafunzo ya Ufundi kutoa mafunzo ya muda mfupi na mrefu kwa watumishi wa TRA pamoja na wadau mbalimbali katika fani za Kodi na Forodha.

No comments:

Post a Comment