Thursday, December 21, 2017

TAKUKURU TANGA YAWAFIKISHA MAHAKAMANI WAHASIBU WAWILI WA OFISI YA MKUU WA MKOA WA TANGA KWA MASHTAKA MATATU YA RUSHWA

TAASISI ya kuzuia na kupambana na rushwa mkoani Tanga(Takukuru) imewafikisha mahakamani wahasibu wawili wa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Tanga Josiah Mwaipela na Julius Idana kwa mashtaka matatu ya rushwa. 

Washtakiwa hao wamefikishwa mahakamani kwa makosa ya
uchepushaji,ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka kuhusiana na shilingi milioni 276,095,106.9 za mishahara ya watumishi ambaowalikoma utumishi wao wa umma kati ya Machi 3 ,2012 na Novemba 2013. 

Hayo yalisemwa na Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Tanga, Christopher Mariba wakati akitoa taarifa yake kwa vyombo vya habari ambapo alisema washtakiwa hao walifikishwa mahakamani jana Desemba 18 mwaka huu. Alisema washtakiwa hao walifikishwa mbele ya hakimu mfawidhi wa mahakama ya hakimu mkazi Tanga,Crisencia Kisongo na kusomewa mashtaka na waendesha mashitaka wa Takukuru Noel Gabba na Neema Kazoka. 

Alisema washtakiwa hao wanadaiwa kutenda makosa ya uchepushaji,ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka kuhusiana na shilingi milioni 276,095,106.9 za mishahara ya watumishi ambao walikoma utumishi wao wa umma kati ya Machi 3 ,2012 na Novemba 2013. 

Aidha alisema katika shitaka la kwanza upande wa mashtaka uliiambia mahakama kuwa kati ya machi 3,2012 na Novemba 1,2013 washtakiwa walifanya uchepuzi wa sh.milioni 276,095,106 ambazo ni mali ya serikali kwa malengo yasiyokusudiwa. Katika shtaka la pili upande wa mashtaka uliiambia mahakama kuwa kati ya machi 3,2012 na Novemba 1,2013 washtakiwa walifanya ufujaji na ubadhirifu wa sh.milioni 245,500,000 walizoaminiwa na kukabidhiwa na serikali. 

Alisema katika shtaka la tatu upande wa mashtaka uliiambia mahakama kuwa kati ya machi 3,2012 na Novemba 1,2013 washtakiwa kwa makusudi walitumia vibaya madaraka yao kwa kushindwa kuziweka sh.milioni 276,095,106.96 za mishahara isiyolipwa kwenye akaunti ya Benki kuu ya Tanzania (BOT). Kamanda huyo wa Takukuru alisema washtakiwa walikana mashtaka dhidi yao na upande wa mashtaka uliiambia Mahakam kuwa uchunguzi wa shauri umekamilika na uko tayari kuendelea na shauri kwa tarehe itakayopangwa na mahakama. 

“Kesi hiyo imeahirishwa hadi Januari 2 mwakani itakapokuja kwa ajili ya kusomewa maelezo ya awali “Alisema Kamanda huyo wa Takukuru. Hata hivyo alisema mshtakiwa wa kwanza Josiah Mwaipela aliachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti yaliyowekwa na Mahakama ambapo aliweka bondi ya mali isiyohamishika yenye thamani ya zaidi ya sh.milioni 69,023,776.74 iliyowekwa na mahakama na mdhamini mmoja. 

Aliongeza pia mshtakiwa wa pili Julius Idana alipelekwa gereza kuu la Maweni Tanga baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana ya kukabidhi fedha taslimu sh.milioni 69,023,776.74 au mali isiyohamishika yenye thamani hiyo pamoja na kuwa na mdhamini mmoja. 

Kamanda huyo wa Takukuru alisema kati ya kiasi cha sh.miloni 276,095,106.96 zilizofanyiwa uchepuzi na washtakiwa sh.milioni 25,602,855.31 ziliokolewa na Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa Takukuru na kurejeshwa serikalini.Habari kwa Hisani ya Blog ya Kijamii ya Tanga Raha 

No comments:

Post a Comment