Sunday, December 31, 2017

MKOA WA PWANI UMEUZA TANI 19,815 ZA KOROSHO NA KUPATA BIL.39-RC NDIKILO

MWENYEKITI wa kamati ya ulinzi na usalama mkoani Pwani, ambae pia ni mkuu wa Mkoa huo, mhandisi Evarist Ndikilo , akizungumza na baadhi ya wakulima wa korosho wakati alipotembelea ghala moja lililopo wilayani Mkuranga.Picha na Mwamvua Mwinyi



Na Mwamvua Mwinyi,Mkuranga

MKOA wa Pwani ,tayari umeuza tani 19,815 ambazo zimeingiza zaidi ya bilioni 39 tofauti na msimu uliopita ambapo uliuza tani 13,000 na kupata bilioni 33.##

Mkoa huo umejiwekea lengo la kuuza tani 25,000 hadi 30,000 kwa msimu huu ambao minada yake ya korosho ikiwa bado inaendelea .Mkuu wa Mkoa wa Pwani ,mhandisi Evarist Ndikilo ,aliyasema hayo Mkuranga ,wakati akizungumzia changamoto na mafanikio waliyoyapata msimu wa korosho 2017/2018 .

Alieleza ,mbali ya hayo wakulima wa korosho mkoani Pwani wakiwa bado wanadai zaidi ya bilioni tano.Mhandisi Ndikilo alisema ,kuuza tani 19,815 hadi sasa ni mwanzo mzuri wa kufikia malengo yao waliyojiwekea msimu huu.Alisema ,hatua hiyo imetokana na serikali kutoa pembejeo bure katika msimu huu na mfumo wa stakabadhi ghalani.

Alibainisha ,licha ya mafanikio hayo lakini kuna changamoto zimejitokeza tangu kuanza kwa minada mwaka huu ikiwemo uhaba wa magunia .Kero nyingine ni ile iliyojitokeza sasa ya kuchakachua ubora wa korosho unaofanywa na baadhi ya vyama vya msingi vya ushirika (Amcos).

“Changamoto ya magunia inaweza kuwa historia endapo tutakubaliana kwa kukaa na mikoa ya Lindi na Mtwara ili kuhamasisha wawekezaji waje wawekeze kiwanda cha magunia lengo likiwa ni kukabiliana na tatizo hili” alifafanua .Akizungumzia kuhusu tatizo la ubora wa korosho, mhandisi Ndikilo ,alisema baadhi ya Amcos zimejiingiza kwenye kuhujumu minada hiyo kwani baadhi yao wameweka michanga na mawe kwenye magunia ya korosho .

Alisema huo ni wizi,uhujumu uchumi na kuaibisha sifa ya nchi ya Tanzania nje ya nchi kwani magunia hayo yangefika India na nchi nyingine ingekuwa aibu na fedheha.Kutokana na upuuzi huo ndio maana nimeamua kutoa maagizo kuwa Amcos 10 zilizojihusisha na ubabaishaji huo viongozi wake wakamatwe na kuhojiwa.

Kwa mujibu wa mhandisi Ndikilo ,kuwepo kwa maghala makubwa itainua soko la korosho msimu ujao na kuondoa ubabaishaji wa maghala ya vichochoroni yanayoleta dosari .Alisema mfumo wa stakabadhi ghalani ni mkombozi kwa wakulima hivyo anawashangaa wale wanaobeza na kuyumbisha mfumo huo.

Mhandisi Ndikilo ,aliwataka wakulima wa korosho kuacha kukubali kurubuniwa na madalali ama wanunuzi wachache hali inayosababisha kukosa mapato kulingana na korosho zao.Serikali mkoani humo imewatoa shaka wakulima wa korosho ambao bado hawajalipwa fedha zao na kudai itasimamia makampuni na wanunuzi kulipa kwa wakati na changamoto zinazojitokeza

No comments:

Post a Comment