Wednesday, December 27, 2017

MBUNGE WA KIBITI AWATAKA WANANCHI NA VIJANA KUJITUMA ILI KUJIPATIA KIPATO

MBUNGE wa jimbo la Kibiti ,mkoani Pwani Ally Ung’ando wa katikati akiwa kwenye ziara yake ya jimbo ya siku 21 ambayo ameianza katika kata ya Rualuke
MBUNGE wa jimbo la Kibiti ,mkoani Pwani Ally Ung’ando akizungumza na wakazi wa vijiji vilivyopo kata ya Rualuke wakati wa ziara yake ya jimbo ya siku 21 ambayo ameianza katika kata ya hiyo.Picha na Mwamvua Mwinyi

Na Mwamvua Mwinyi,Kibiti

MBUNGE wa jimbo la Kibiti mkoani Pwani ,Ally Ung’ando amewataka wananchi jimboni hapo kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano kwa kujishughulisha kimaendeleo ili kupiga hatua kiuchumi.

Amewaomba kushirikiana kwenye miradi ya maendeleo badala ya kuiachia serikali ama viongozi pekee suala ambalo linakwamisha jitihada mbalimbali zinazoendelezwa.Ung’ando aliyasema hayo kijiji cha Rungungu kata ya Rualuke katika ziara yake ya siku ya kwanza aliyoianza kwenye kata hiyo ambapo anatarajia kuendelea na ziara hiyo kwa siku 21 katika kata Tisa na vijiji vyote jimboni hapo.

Aliwataka vijana kuacha kujisahau kufanya kazi na kujiunga vikundi ili waweze kuwezeshwa kirahisi.“Vijana mjitume ,acheni kuishi kimazoea kwani maendeleo yoyote yanaletwa kwa kujituma ” alisema mbunge huyo.Hata hivyo ,alikemea tabia inayofanywa na baadhi ya wakulima wa korosho ambao wanauza korosho zao kwa mfumo usio rasmi wa kangomba .

Ung’ando alisema mfumo unaotambulika ni mfumo wa stakabadhi ghalani lakini wakulima wamekuwa wakiuza korosho zao kiholela .“Niwaombe muache kuuza korosho zenu kwa madalali ,hawawasaidiii,mtakuja kupata hasara na mkumbuke serikali haitohusika na mtu anauza korosho zake kiholela,msije kuipa lawama serikali wakati wenyewe mnataka njia nyepesi zinazowakandamiza ” alisema.

Pamoja na hayo ,aliwasihi wazazi na walezi kuwapeleka watoto wao shule kupata haki ya elimu .Ung’ando alisema serikali chini ya Rais John Magufuli inatoa elimu bure kwa wanafunzi wa msingi hadi kidato cha nne lakini wazazi wamekuwa wakiwanyima fursa hiyo watoto wao.Katika ziara hiyo pia anatoa mifuko ya saruji 100 kwa kila kata,ambayo itakayosaidia kusukuma maendeleo ya kata hizo.

Ung’ando alianza ziara yake ya jimbo desemba 26 kwa kuzungumza na kusikiliza kero kwa wapiga kura wake katika vijiji vya Rungungu,Kilola Tambwe na Nyamatanga kata ya Rualuke,Ziara itaendelea desemba 28 kupisha ziara ya naibu waziri wa Nishati Mh,Subira Mgalu ambae yupo jimbo la Kibiti kwa ajili ya kuangalia changamoto ya nishati ya umeme .

No comments:

Post a Comment