Thursday, December 7, 2017

JAFO ATANGAZA WALIOCHAGULIWA KUJIUNGA KIDATO CHA KWANZA 2018

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Seleman Jafo akiongea na Waaandishi wa habari kuhusu matokeo ya uchaguzi wa wanafunzi wa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2018 katika ukumbi wa Mikutano wa Tamisemi Mjini Dodoma.
Baadhi ya waandishi wa Habari wakifuatilia taarifa ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Seleman Jafo kwenye mkutano i kuhusu matokeo ya uchaguzi wa wanafunzi wa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2018 katika ukumbi wa Mikutano wa Tamisemi Mjini Dodoma.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Seleman Jafo akifafanua jambo wakati akiongea na Waaandishi wa habari kuhusu matokeo ya uchaguzi wa wanafunzi wa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2018 katika ukumbi wa Mikutano wa Tamisemi Mjini Dodoma.

…………….

Angela Msimbira – OR-TAMISEMI

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Seleman Jafo amesema kati ya wanafunzi 662,035 waliofaulu mtihani wa kumaliza elimu ya msingi wanafunzi 650,862 sawa na asilimia 98.31 wamechaguliwa kujiunga na masomo ya kidato cha kwanza katika awamu ya kwanza mwaka 2018

Akitangaza matokeo ya uchaguzi wa wanafunzi wa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2018 Tanzania Bara kwenye kikao na waandishi wa habari leo katika ofisi za Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe Jafo amesema kuwa idadi wa wanafunzi mwaka huu imeongezeka kwa wanafunzi 124,209 ambapo ni sawa na asilimia 23.58 ikilinganishwa na wanafunzi 526,653 waliochaguliwa awamu ya kwanza kuingia kidato cha kwanza mwaka 2016.

Amesema kuwa wanafunzi 1912 wenye uhitaji maalum (pupils with special needs) waliofaulu mitihani ya darasa la saba wamechaguliwa kujiunga na masomo ya kidato cha kwanza mwaka 2018 kwenye shule za sekondari za Serikali.

Mhe. Jafo amefafanua kuwa wanafunzi 11,173 sawa na asilimia 1.69 ya waliofaulu hawakupata nafasi ya kuchaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika awamu ya kwanza ya uchaguzi kutokana na uhaba wa miundombinu ya elimu hususani vyumba vya madarasa kwenye baadhi ya Halmashauri ya Mikoa ya Lindi (170), Mbeya (3,092), Rukwa (4,091), Manyara (1,268), Katavi (976) na Simiyu (1,576).

Amesema kuwa Halmashauri ambazo zimeshindwa kuwapangia wanafunzi wote waliofaulu nafasi ya kujiunga na kidato cha kwanza ni Halmashauri za Lindi wanafunzi (80) Mbeya (207),Halmashauri ya Jiji la Mbeya ( 1,227), Mbarali (1,578), Kalambo (166), Nkasi (1,318), Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga (1,054), Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga (1,553), Babati (581). Hanang (687), Mpanda (262), Nsimbo (714), Halmashauri ya Mji wa Bariadi (369) na Halmashauri ya Wilaya ya Busega (1,207).

Mhe. Jafo amewaagiza Wakuu wa Mikoa ambayo haijakamilisha ujenzi wa miundombinu hasa ya vyumba vya madarasa kuhakikisha wanakamilisha hadi kufikia mwezi februari, 2018 ili wanafunzi watakaochaguliwa kwenye awamu ya pili wapate nafasi ya kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2018.

“Lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa wanafunzi wote waliofaulu mtihani wa darasa la saba wanapata nafasi ya kujiunga na masomo ya kidato cha kwanza nimeshatoa maelekezo kwa wakuu wa mikoa kuhakikisha kuwa wanafunzi wote wanapata nafasi ya kujiunga na kidato cha kwanza kwa mwaka 2018” Amesema Jafo

Mhe. Jafo amesisitiza kuwa walezi na wanafunzi ambao watakosa nafasi katika awamu ya kwanza ya uchaguzi kuwa wavumilivu wakati mikoa inajiandaa kwa ajili ya kuwapokea wanafunzi wote kuanza na masomo ya kidato cha kwanza.

Amewaagiza waalimu na watendaji wa elimu katika ngazi zote nchini kuongeza bidii katika usimamiaji na ufuatiliaji wa utoaji wa elimu nchini na kushirikiana na wadau wa elimu kukamilisha majengo na kuandaa mazingira ya kuwapokea wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza 2018 bila vikwanzao vikiwemo michango na ada ili kutekeleza sera ya utoaji wa elimu msingi bila malipo.

Aidha amewaomba Wazazi, Walezi na jamii kwa ujumla kushirikiana na Wilaya, Halmashauri na shule, kuhakikisha kwamba wanafunzi wote waliochaguliwa wanaandikishwa , wanahudhuria na kubaki shuleni hadi watakapohitimu elimu ya Sekondari.

2 comments:

  1. Kwa yamkini idadi hiyo ya watoto wanaokosa nafasi katika awamo ya kwanza yawezekana zaidi ya 50% watapata nafasi maana ni idadi kubwa inakwenda katika shule za binafsi

    ReplyDelete
  2. where is link to the names of selected students

    ReplyDelete