Tuesday, December 5, 2017

BOHARI YA DAWA (MSD) YAPONGEZWA KWA USAMBAZAJI WA DAWA NCHINI

Na Dotto Mwaibale

BOHARI ya Dawa (MSD), imepongezwa kwa kushinda tenda ya kununua dawa Jumuhiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC)

Pongezi hizo zimetolewa Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili(MNH), Profesa Lawrence Mseru wakati akizungumza na Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laurean Bwanakunu na timu yake wakati wakiwa katika ziara ya kikazi ya kutembelea Hospitali za Mkoa wa Dar es Salaam kujua changamoto walizonazo za upatikanaji wa dawa na kuzitafutia ufumbuzi wa pamoja.

"Kwanza tunawapongezeni MSD kwa kufikia hatua ya kununua dawa katika Jumuhiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) hii ni hatua ya kujivunia kama nchi" alisema Profesa Mseru.

Mseru aliongeza kuwa licha ya kuwepo changamoto ndogo ndogo MSD imejitahidi katika huduma ya usambazaji wa dawa hapa nchini hivyo akaomba ushirikiano baina yao uendelee kudumishwa ili kutoa huduma nzuri zaidi ya kuwahudumia wananchi ukizingatia kuwa taasisi hizo zote zinafanya kazi ya Serikali.

Akizungumza katika ziara hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa, Mishipa ya Fahamu na Upasuaji wa Ubongo Muhimbili (MOI),Respicious Lwezimula alisema kazi kubwa inayofanywa na MSD inapaswa kuungwa mkono kwa kununua dawa na vifaa tiba.

"Tuna kila sababu ya kuwaunga mkono hawa wenzetu kwa kununua vifaa tiba na dawa kutoka kwao badala ya kununua kwenye maduka ya watu binafsi kikubwa tunawaomba bei yao iwe tofauti kidogo" alisema Lwezimula.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke, Amani Malima alisema suala la manunuzi ya dawa na vifaa tiba linachangamoto kubwa lakini MSD wamesaidia sana kuzipunguza kutokana na ushirikiano wanaofanya baina yao na wateja wao hawana budi kupongezwa.

Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laurean Bwanakunu amewaomba wateja wao hao kufanya Maoteo ya mahitaji yao sahihi na kuyawasilisha MSD kwa wakati kwa mujibu wa sheria yaani tarehe 30 Januari kila mwaka,hasa dawa na vifaa tiba vinavyonunuliwa kwa manunuzi maalumu.Bwanakunu alihimiza watoa huduma katika hospitali hizo kutambua jukumu walilonalo katika usimamizi wa matumizi ya dawa na vifaa tiba kwa wananchi.

Akizungumza katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Temeke na Taasisi ya Tiba ya Mifupa, Mishipa ya Fahamu na Upasuaji wa Ubongo Muhimbili (MOI), Bwanakunu alisema anazitambua changamoto zilizopo za usambaji wa dawa na vifaa tiba na kuwa MSD katika kukabiliana na changamoto hizo imepata msaada wa magari 220 kutoka Global Fund ambayo yataboresha usambazaji kutoka mara nne kwa mwaka hadi mara sita kwa mwaka.

Kuhusu vifaa vya Manunuzi maalumu Bwanakunu amesema hospitali zikiwa zinaomba kwa wakati mmoja ingerahisisha kuagiza vifaa hivyo mapema,badala ya kila hospitali kuleta kwa wakati wake."Vifaa hivi tunaagiza nje ya nchi na mchakato wake unachukua muda mrefu hivyo tukipata oda mapema itatusaidia kupunguza changamoto hiyo " alisema Bwanakunu.
 Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD), Laurean Bwanakunu (kushoto), akizungumza na viongozi wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa, Mishipa ya Fahamu na Upasuaji wa Ubongo Muhimbili (MOI) katika ziara yake ya kikazi ya kutembelea Hospitali za Mkoa wa Dar es Salaam kujua changamoto walizonazo za upatikanaji wa dawa na kuzitafutia ufumbuzi wa pamoja katika ziara iliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita jijini Dar es Salaam.
 Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa, Mishipa ya Fahamu na Upasuaji wa Ubongo Muhimbili (MOI), Respicious Lwezimula (kulia), akizungumza katika kikao hicho.
 Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD), Laurean Bwanakunu (wa tatu kushoto), akizungumza na viongozi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili katika ziara hiyo.

Kikao kikiendelea.
 Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD), Laurean Bwanakunu (wa nne kulia), akiwa na viongozi wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa, Mishipa ya Fahamu na Upasuaji wa Ubongo Muhimbili (MOI)
 Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke, Amani Malima, akizungumza na viongozi kutoka MSD. Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laurean Bwanakunu na Meneja wa MSD Kanda ya Dar es Salaam, Celestine Haule. 
Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD), Laurean Bwanakunu (katikati), akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke baada ya kufanya nao mazungumzo mwishoni mwa wiki iliyopita.

No comments:

Post a Comment