Sunday, November 26, 2017

Waziri Mhagama aitaka Halmashauri ya Bahi kukamilisha ujenzi wa Soko la Kigwe


Na. MWANDISHI WETU – DODOMA

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu, Bunge, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Bahi kuhakikisha inamaliza ujenzi wa soko la Kigwe kwa kuhakikisha wanajenga vyoo na vibanda vidogo vitakavyo saidia soko hilo lililojengwa na Programu ya Miundo Mbinu ya Masoko, Uongezaji Thamani na Huduma za Kifedha Vijijini (MIVARF).

Ameyasema hayo alipofanya ziara yake Wilayani Bahi Novemba 21, 2017 kwa lengo la kujionea namna uboreshaji wa soko hilo ambalo tayari limekamilika kwa asilimia 90 na kukabiliwa na changamoto za vibanda na vyoo vya kudumu.

“Ninaiagiza Halmashauri hii kuhakikisha inaleta timu ya wataalamu kupima viwanja na kuvigawa kwa wananchi pamoja na kumalizia ujenzi wa Vyoo vya soko ili lianzae utekelezaji wake haraka na kuhakikisha umeme unafungwa ndani ya soko hili”.

Kwa upande wake Mbunge wa Bahi Mhe. Omary Badwel alieleza ujenzi wa soko ni jambo ja muhimu linalogusa wanakigwe wote kwani tangu enzi za mkoloni kumekuwa na changamoto ya soko na kuwataka wananchi kulitunza na kuhakikisha linakuwa msaada kwao wote.

“Soko hili toka utawala wa mkoloni kulikuwa na soko bovu hivyo hatua ya kulikamilisha litavutia wengi na kukuza uchumi wa wana Kigwe wote.”Alisisistiza Badwel

Kwa upande wake mkazi wa Kigwe Bi.Anastazia Mkatato alieleza kuwa kujengwa kwa soko hilo litatatua changamoto iliyopo ya kukosa soko la kudumu kwani yaliyopo ni madogo yanayomilikiwa na watu binafsi.

“Ninaishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Programu ya Miundo Mbinu ya Masoko, Uongezaji Thamani na Huduma za Kifedha Vijijini iliyoamua kutujengea soko hapa Kigwe na hii itatupa nafasi ya kuuza mazao na bidhaa kwa wingi kupelekea kukuza uchumi wetu.”Alieleza Anastazia.

Naye Mratibu wa Mradi Taifa Bw.Walter Swai alieleza kuwa soko hili ni muhimu kwa wana Kigwe na maeneo jirani , hivyo tutaendelea kuunga mkono jitihada za kuhakikisha vifaa vinawekwa ikiwemo Meza za kuuzia mbidhaa sokoni.

“Tayari Ofisi yangu itachukua changamoto hii ya kukosekana kwa meza za kuuzia na kuitatua ndani ya mwezi mmoja hivyo niwaahidi kutekeleza haya.”Alisisitiza Bw.Swai

Ujenzi wa soko la Kigwe umegharimu jumla ya zaidi ya shilingi milioni 68 ambapo Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Programu ya Miundo Mbinu ya Masoko, Uongezaji Thamani na Huduma za Kifedha Vijijini (MIVARF) ilitoa kiasi cha zaidi ya shilingi Milioni 50 pamoja na Mfuko wa jimbo kuchangia jumla ya shilingi Milioni 15. Dhumuni la mradi ni kuwa na eneo rasmi la kufanyia biashara na kuwezesha wajasiliamali wa Kigwe na kujikwamua kiuchumi na kukuza maendeleao yao.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akisisitiza jambo kwa wananchi wa Kigwe alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa soko la Kidwe Wilayani Bahi Dodoma.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akisalimiana na Mbunge wa Bahi Mhe. Omary Badwel alipowalisi kukagua ujenzi wa Soko la mazao la Kigwe Lililopo Bahi Dodoma.
Afisa Mtendaji Kata Bw. John Mchiwa akikabidhi taarifa ya Ujenzi wa Soko Kigwe kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu, Bunge, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama alipofanya ziara Bahi kuona maendeleo ya ujenzi huo.
Mbunge wa Bahi Mhe. Omary Badwel akitoa maelezo kuhusu ujenzi wa soko la Kigwe lililofadhiliwa na Programu ya Miundo Mbinu ya Masoko, Uongezaji Thamani na Huduma za Kifedha Vijijini (MIVARF) kwa kushirikiana na Halmashauri wakati wa ziara ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Mhe. Jenista Mhagama Wilayani Bahi Dodoma.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama (kushoto) akiteta jambo na Mkurugenzi wa Wilaya ya Bahi Bi. Rachel Chuwa wakati wa ziara yake Kigwe.
Mratibu Taifa wa Programu ya Miundo Mbinu ya Masoko, Uongezaji Thamani na Huduma za Kifedha Vijijini (MIVARF) Bw. Walter Swai akisalimiana na baadhi ya wakazi wa Kigwe walipotembelea Kijiji hicho kuona ujenzi wa soko la Kigwe unavyoendelea.(PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU – DODOMA)

No comments:

Post a Comment